![]() |
| Askari wa Jeshi la serikali ya Sudan Kusini |
Umoja wa Mataifa (UN) umelituhumu jeshi la Sudan Kusini
kwa vitendo vya kuwabaka na kuwachoma moto mabinti wakati wa mapambano ya hivi
karibuni katika jimbo moja la mpakani.
Wachunguzi wa kikosi cha Umoja huo nchini Sudan (UNMISS)
wameeleza hayo katika ripoti iliyochapishwa leo Jumanne.
Ripoti hiyo imetokana na ushuhuda wa waathirika na
mashuhuda 115 kutoka katika jimbo la Unity kaskazini mwa nchi hiyo.
Jimbo hilo lipo kaskazini mwa Sudan Kusini, karibu na
mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Sudan.
Hivi karibuni eneo hilo limeshuhudia mapigano makali
kabisa tangu kuibuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miezi 18
katika taifa hilo changa kabisa ulimwenguni.
UN imesema kuwa mapigano hayo, hususan katika wilaya ya
Mayom aambayo ilikuwa eneo muhimu la uzalishaji wa mafuta, yalizuka mwezi
Aprili baina ya vikosi vya serikali na waasi.
“Manusura wa mashambulizi haya waliripoti kuwa askari wa
serikali na waasi kutoka wilaya ya Mayom waliendesha kampeni dhidi ya wakaazi
ambayo iliwaua raia, kuharibu vijiji na kuwafanya zaidi ya watu 100,000
kuyakimbia makazi yao,” imesema ripoti hiyo.
“Baadhi ya tuhuma mbaya kabisa zilizokusanywa na maafisa
wa UNMISS zilijikita kwenye utekaji na dhulma za ngono dhidi ya wanawake na
mabinti, baadhi yao wakiripotiwa kuchomwa moto wakiwa hai katika makazi yao,”
iliongeza.
Hata hivyo, jeshi la Sudan Kusini halijajibu tuhuma
hizo. Huko nyuma nchi hiyo iliwahi kukanusha madai ya ripoti kama hizo.
UN imesema kuwa ripoti hiyo imekabidhiwa kwa maafisa wa
serikali, ambao hawajaeleza chochote kuhusu utafiti huo.
![]() |
| Watoto wakimiminika katika eneo la ugawaji chakula katika jimbo la Unity, Sudan Kusini. |
Sudan Kusini ilitumbukia katika ghasia mwezi Desemba
mwaka 2013, baada ya mapigano kuzuka baina ya askari watiifu kwa Rais Salva
Kiir na waasi wanaoongozwa na aliyekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo, Riek
Machar, katika mji mkuu Juba.
Ghasia hizo zimesababisha vifo vya maelfu ya watu na
mamilioni wengine kuyakimbia makazi yao.
Sudan Kusini ilipata uhuru wake Julai 2011 baada ya raia
wake kupiga kura kwa wingi kujitenga na Sudan.


0 comments:
Post a Comment