![]() |
| Eneo la Kaskazini mwa Nigeria limewekwa katika hali ya hatari, lakini mashambulizi yameendelea kugharimu maisha ya wakazi wa eneo hilo. |
Watu wanaodaiwa kuwa wapiganaji wa kundi la Boko Haram la
nchini Nigeria wamewaua watu wasiopungua 90, wakiwemo watoto na wanawake,
katika shambulizi kwenye kijiji kimoja kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa mashuhuda, shambulizi hilo limetokea
katika kijiji cha Izghe katika jimbo la Borno leo hii.
Mashuhuda hao wanasema kuwa wanamgambo wenye silaha na
mabomu, walikizunguka kijiji hicho na kukishambulia kwa risasi. Aidha, inadaiwa
kuwa walizichoma moto nyumba kadhaa.
“Wakati huu ninapozungumza na wewe, maiti za watu waliouawa
bado zimelala mitaani,” mkazi wa kijiji
hicho, Abubakar Usman alisema na kuongeza: “tulikimbia kuwazika, kwa hofu
kwamba wauaji bado wanasabiri porini.”
Kamishna wa polisi katika jimbo la Borno, Lawal Tanko,
amethibitisha kutokea kwa shambulizi hilo lakini akasema kuwa maelezo ya kina
juu ya shambulizi hayo hayajathibitishwa.
Shambulizi hilo ni jipya kabisa katika mfululizo wa
wimbi la ghasia katika eneo hilo la kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Mnamo Januari 26, wanamgambo wakiwa na mabomu na silaha
nyingine, walikishambulia kijiji cha Kawuri katika jimbo la Borno katika siku
ya gulio.
Kwa mujibu wa wanausalama, katika tukio hilo watu 52 waliuawa
na kijiji kuchomwa moto.
Siku hiyo hiyo, wanamgambo walilichoma kanisa moja
katika kijiji cha Wada Chakawa katika jimbo la Adamawa. Walifyatua mabomu na
kuyatupa kanisani, yakaua watu kadhaa, kabla ya kuzichoma nyumba na kuwachukua
wakaazi wa kijiji hicho kama mateka katika mzingiro huo uliodumu kwa muda wa
saa tano.
Mwenyekiti wa kijiji, Maina Ularamu alisema kuwa polisi walikusanya
miili 45, ikiwemo ya maafisa wawili wa polisi.
Mnamo Mei 2013, Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan,
alitangaza hali ya hatari katika majimbo matatu kaskazini mashariki mwa nchi
hiyo, ambayo ni Borno, Yobe, na Adamawa. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha
kuwa zaidi ya watu 1,200 wamepoteza maisha katika ghasia nchini humo tangu hali
hiyo ya hatari ilipotangazwa.
Kundi la Boko Haram – yaani “Taaluma kutoka Magharibi ni
Haramu” – linasema kuwa lengo lake ni kuiondosha serikali ya Nigeria.
Kundi hilo linadai kuhusika na mashambulizi kadhaa
katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo tangu mwaka 2009.

0 comments:
Post a Comment