![]() |
| Eneo ulipotokea mlipuko wa bomu katika mji wa Taba kusini mwa Sinai leo Februari 16, 2014. |
Mlipuko mkubwa wa bomu katika eneo la Sinai nchini
Misri, umewaua watu wasiopungua 5 wakiwemo watalii wanne kutoka Korea ya Kusini
na kuwajeruhi wengine kadhaa.
Maafisa wa usalama katika eneo hilo wamesema kuwa watu
hao walipoteza maisha baada ya bomu kulipuka ndani ya basi la watalii leo katika
mji wa Taba kwenye Peninsula ya Sinai.
Mamlaka za eneo hilo zinasema kuwa watalii wanne kutoka
Korea ya Kusini na dereva wa basi hilo walipoteza maisha papo hapo.
Kwa uchache watu 30 walijeruhiwa na kukimbizwa katika hospitali
iliyokuwa eneo la jirani kwa matibabu.
"Kulikuwa na viungo vya miili na maiti. Niliiona maiti
ya mtu mmoja aliyeonekana kuwa ni Mkorea, huku akiwa hana mguu,” alisema
daktari anayeendesha kituo kimoja cha afya katika eneo hilo.
Siku za hivi karibuni eneo la Peninsula ya Sinai limekuwa
likikumbwa na matukio mbalimbali, ambapo wanamngambo wamekuwa wakifanya
mashambulizi dhidi ya vikosi vya usalama na kuyalenga maeneo mengine.
Kwa kawaida, Mabedui katika Peninsula hiyo wamekuwa
wakiwateka wageni na kuwatumia nyenzo ya kuzungumza na mamlaka za serikali
kutaka ziwaachie huru ndugu zao
waliofungwa.
Tukio la leo linakuja wakati makundi ya wanamgambo yakiwa
yamedai kuhusika na mashambulizi na milipuko kadhaa tangu kuondolewa madarakani
kwa Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo, Mohammed Mursi, aliyeondolewa
na jeshi Julai 3, 2013.
Katika kulishughulikia suala hilo, serikali iliyowekwa
madarakani na jeshi, ilianzisha operesheni maalumu, ikatuma vikosi vya askari
wenye zana nzito za kijeshi katika eneo hilo.
Watu kadhaa wameshapoteza maisha wakati wa mapambano ya
wanamgambo na jeshi la Misri katika eneo hilo la Sinai.

0 comments:
Post a Comment