Ingawa tendo la ndoa lisipofanywa kwa kuzingatia kanuni
na taratibu, sambamba na umakini, linaweza kusababisha maradhi, lakini kwa
wanandoa, tendo hilo linatajwa kuwa na
manufaa mengi kiafya tofauti na faraja
ya kawaida iliyozoeleka kwa wengi.
Imefahamika kuwa tendo hili likifanyika ipasavyo
husaidia kuondoa msongo wa mawazo, maradhi ya moyo, maumivu ya kichwa
yasiyokoma na kupunguza kasi ya saratani ya tezi dume.
Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (Muhas), Dk Yahya
Kishashu anasema inategemea tendo linafanywa na nani na mhusika yupo kwenye
mazingira gani.
“Kwa mfano, tendo la ndoa linaondoa msongo wa mawazo
iwapo unayetenda naye unampenda na
amekupa maandalizi mazuri. Sidhani kama alimradi utende hilo tendo na
yeyote litakusaidia,” anasema mtaalamu huyo.
Anaongeza kuwa
ndiyo maana baadhi ya watu wanatoka nje ya ndoa zao kwa sababu si mara
zote tendo la ndoa linawafurahisha wanandoa.
“Wakati mwingine tendo hilo laweza kuwa karaha kwao,”
anasema.
MAZOEZI
Si hivyo tu, utafiti uliofanyika Canada hivi karibuni umebainisha kuwa kufanya tendo
la ndoa kwa kipindi cha dakika 25 kwa wanamume kunachoma kalori 100 na kwa
wanawake kalori 69.
Tendo hilo likifanyika kwa nusu saa, linaweza kupunguza
kalori za mwili kuliko kutembea kwenye mashine ya mazoezi ya ‘treadmill’.
“Ni sawa na kucheza mpira wa tenisi au kutembea ukipanda
mlima kwa dakika 20 au kucheza gofu kwa kasi kwa dakika 33 au zoezi la yoga kwa
dakika 40,” sehemu ya utafiti hiyo inasema.
Utafiti huo wa
Canada ulishabihiana na kampeni
iliyofanywa na Taasisi ya Moyo ya Uingereza ambayo ilisema kuwa dakika 30 za tendo la ndoa kwa siku ni muhimu
kama mazoezi ya kutembea kwa mashine.
Kwa undani zaidi utafiti huo ulichambua na kusema kuwa,
tendo la ndoa, lina manufaa kwa moyo na
mapafu.
Inaelezwa kuwa vichocheo
vinavyotoka baada ya tendo la
ndoa vinasaidia kupunguza kiwango cha msongo wa mawazo na kuongeza uzalishaji wa seli mpya za ubongo.
Kuhusu mazoezi,
Dk Kishashu anasema anakubaliana na utafiti huo na kusema kuwa ni kweli tendo
hilo linasaidia kupunguza kalori, lakini linapofanyika mara nyingi zaidi
linazeesha.
Hata hivyo, wanasayansi wanalipa uzito mdogo tendo hilo
katika muktadha wa ujenzi wa hisia na mwili na kuwa halisisitizwi vya kutosha
kama aina mojawapo ya mazoezi.
TIBA
KWA MOYO, MAPAFU NA UBONGO
Inaelezwa kuwa tendo la ndoa, linasaidia kuondoa msongo
wa mawazo hivyo kupunguza hatari ya maradhi ya moyo.
Si hivyo tu, bali tendo hilo husaidia mapafu kufanya
kazi yake vyema, kuingiza na kutoa hewa chafu.
Kitaalamu, upo mchakato uitwao ‘Neurogenesis’ ambao
husaidia kulinda seli za ubongo zinazokufa kutokana na uzee. Kuna eneo kwenye
ubongo linaloitwa ‘hippocampus’ ambalo ni eneo linalotengeneza kumbukumbu.
“Kazi kubwa inafanyika kwenye ubongo, wakati wa tendo la
ndoa, kiasi kikubwa cha viamsha raha huanzia kwenye ubongo na kuleta taarifa
kwenye maeneo mengine ya mwili.
Ndiyo maana watu wengi hupotea kiufahamu wakati wa
kilele” anasema Dk Gosh, ambaye ni mtafiti.
Hata hivyo, wanaume ambao wanaendelea na tendo la ndoa
mara kwa mara hadi wanapofikisha miaka 50 na zaidi, kwa maana ya kutoa mbegu za
kiume mara kumi kwa mwezi, wapo katika hatari ndogo ya kupata saratani ya tezi
dume. Inaelezwa kuwa mbegu za kiume
hazitakiwi kukaa mwilini kwa muda mrefu.Zinatakiwa zitolewe mara kwa mara ili
kuzifanya seli mpya zizalishwe. Ni kama kusafisha mpira, inasaidia kusitisha
ujenzi wa seli za zamani ambazo zaweza kuwa chanzo cha saratani.
Kwa wanawake, tendo la ndoa husaidia kuundwa kwa misuli
ya nyonga ambapo misuli hiyo ikiwa imara huondoa hatari ya kushindwa kuzuia
mkojo,(urine incotinence) jambo linaloathiri mwanamke mmoja kati ya wanne wenye
umri wa miaka zaidi ya 50.
“ Wakati wa tendo la ndoa, kwa kawaida sakafu ya nyonga
za mwanamke hubana na kuachia. Hii husababisha misuli hiyo kuwa imara’ anasema
mtafiti huyo.
Hata hivyo,
utafiti wa Chuo Kikuu cha Nottingham nchini Uingereza unaeleza kuwa, wanaume wanaofanya tendo hilo na kumwaga
mbegu mara 20 hadi 30 kwa mwezi, wapo katika hatari ya kupata saratani ya tezi
dume kwa sababu ya umri wao .
KUONDOA
MAUMIVU YA KICHWA
Utafiti mwingine umebaini kuwa, wanawake wenye umri
mdogo hukumbwa na msongo wa mawazo iwapo hawatafanya tendo la ndoa kwa muda
mrefu.
Wanawake hao, wanapofika kilele cha tendo hilo, damu
hutembea kutoka kwenye ubongo, jambo
ambalo huondoa maumivu ya kichwa.
Dk Innocent Mosha, Mchunguzi wa magonjwa wa Hospitali ya
Taifa Muhimbili anasema kuwa inawezekana
kuwa tendo la ndoa likasaidia kuondoa msongo wa mawazo iwapo mtu hajalifanya kwa muda mrefu na yupo katika
hali kubwa ya uhitaji.
“Kama mtu hajafanya tendo hilo muda mrefu na hivyo
amelikamia, basi akilifanya litamwondolea msongo wa mawazo,” anasema
Anasema mtu
ambaye anahitaji kufanya tendo hilo na hajalipata, aghalabu huwa na msongo wa
mawazo lakini kama huliwazi hawezi kuwa na msongo.
Kwenye utafiti huo, wanawake 83 wenye maradhi ya kichwa
walipata nafuu kubwa baada ya kumaliza tendo la ndoa.
UKARIBU/
UPENDO
Mwanasaikolojia, wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Modesta Kimonga anasema ni kweli kuwa tendo
la ndoa linaleta faraja inayoondoa msongo wa mawazo.
Anasema hali hiyo
inatokana na nadharia au mfumo wa
uambatano katika saikolojia au ‘attachement theory’
“Hii ‘attachment theory’ ipo kwa watoto wanaponyonya
maziwa ya mama zao, na kwa watu wazima ni kwenye tendo la ndoa ambalo linaleta
faraja na ukaribu,” anasema.
Anaongeza:
“Faraja hupatikana baada ya wanandoa kutenda tendo hilo na huweza
kuondoa kabisa mawazo kichwani au huzuni.”
Watafiti walibaini kuwa vichocheo vya ‘oxtocin’
vinavyotolewa wakati wa tendo hilo husaidia hisia za upendo na mshikamano
kwenye uhusiano ya muda mrefu.
Lipo ongezeko kubwa la kemikali ya ‘oxtocin’ kwa
wanawake na wanaume baada ya kumaliza tendo la ndoa ambalo husaidia kukuza
uhusiano na ukaribu wao.
WANAUME
KULALA BAADA YA TENDO LA NDOA
Utafiti wa jarida la Sayansi ya Mishipa ya Fahamu na Tabia uliochapishwa mwaka 2012
umebaini kuwa, dawa za usingizi hufanya kazi sawa na tendo la ndoa kwa wanaume.
Eneo la mbele la
ubongo ‘pre –frontal cortex’, ambalo linahusiana na ufahamu, au umakini wa kiakili, huzima au
kufungwa baada ya kumaliza tendo hilo.
Kwa baadhi ya
utafiti, wanaume kumaliza tendo la
ndoa, ni sawa na kunywa dawa za usingizi
za ‘diazepam’ zenye ukubwa wa miligramu mbili.
Pia, vichocheo vinavyotoka baada ya tendo hilo kama
‘melatonin,’ ‘oxytocin’ na ‘vasopresin’, zinamsababisha mwanaume apate usingizi
mzito.
KWA HISANI YA GAZETI LA MWANANCHI

0 comments:
Post a Comment