Milio ya risasi imesikika leo ndani na nje ya msikiti wa
Masjid Mussa katika mji wa Mombasa nchini Kenya kufuatia hatua ya polisi
kuvamia msikitini hapo kutokana na kile walichosema kuwa ni kupokea taarifa
kwamba kuna vijana wa Kiislamu waliokuwa wakipewa mafunzo ya kijeshi na kasumba
za misimamo mikali.
Hatua hiyo ya polisi iliibua ghasia ndani ya msikiti huo
wa Masjid Mussa uliopo katika maeneo ya Majengo na katika mitaa ya jirani.
Polisi walifyatua gesi ya kutoa machozi na kumekuwepo na taarifa kuwa risasi za
moto zilitumika kuudhibiti umati wa watu waliokuwa wakiwarushia mawe polisi.
Milio ya risasi iliendelea kusikika saa nne baada ya
polisi kuingia mahali hapo na mwangwi wa milipuko ulitanda katika mitaa ya
jirani.
Shirika la habari la Reuters limemkariri mkuu wa polisi
katika mkoa wa Mombasa, Robert Kitur akisema kuwa polisi walivamia eneo hilo
baada ya kutonywa juu ya uwepo wa vijana hao. Na kwamba maafisa wa polisi
walipofika hapo walishambuliwa. Hata hivyo, maelezo ya mkuu huyo wa polisi
hayajathibitishwa na vyanzo huru.
"Tumewakuta wakiwajaza vijana kasumba za misimamo
mikali na mafunzo mbalimbali,” Kitur aliwaambia waandishi wa habari jirani na
msikiti huo wakati operesheni hiyo ikiendelea.
Waislamu wengi katika mitaa ya Mombasa wanahisi
kunyanyapaliwa na serikali ya Kenya na operesheni zinazofanywa na serikali hiyo
katika kukabiliana na kile inachodai kuwa ni mitandao ya mafunzo ya kijeshi
zimekuwa zikiibua ghasia katika mji huo wa kitalii.
Lakini maafisa usalama nchini humo wanadai kuwa Masjid
Mussa imekuwa ikitoa mafunzo kwa wanamgambo ambao huenda kuungana na wapiganaji
wa al Shabaab nchini Somalia.
Mwezi Agosti 2012 watu waliojifunika nyuso walimuua kwa
kumpiga risasi Imamu wa Msikiti huo, Sheikh
Aboud Rogo, aliyekuwa akitoa mahubiri hapo na ambaye serikali za Marekani na
Kenya zilikuwa zikimshutumu kutoa mafunzo na kufadhili waasi wa al Shabaab
nchini Somalia wenye mafungamano na mtandao wa wapiganaji wa al Qaeda.
Mwaka mmoja baadaye, mrithi wa sheikh Rogo, Sheikh
Ibrahim Rogo aliuawa katika shambulizi kama hilo. Matukio yote mawili yaliibua
ghasia katika mji huo.
Waumini katika msikiti huo wanawatuhumu wanausalama
kuhusika na vifo hivyo, shutuma ambazo polisi wamekuwa wakizikanusha.
Kamanda Kitur anasema kuwa askari wamewakamata zaidi ya
watu 100 katika operesheni ya leo na maafisa wawili wamejeruhiwa.
CHANZO: http://www.reuters.com/article/2014/02/02/us-kenya-riot-idUSBREA110A220140202

0 comments:
Post a Comment