Miongoni mwa vitu vizuri sana kuhusu mitandao ya kijamii
ni uhuru na urahisi wa kubadilishana taarifa. Hata hivyo, uhuru huo una gharama
zake. Katika ulimwengu wa mitandao ya kijamii isiyochujwa, sio kila taarifa ni
ya kweli.
Picha ni rahisi sana kubadilishwa, kurekebishwa na
kutumika nje ya muktadha uliokusudiwa. Ili kuepuka kuangukia katika mtego wa
kudanganywa na ufundi mbalimbali wa upotoshaji wa taarifa, tunahitaji
kuyafumbua macho na akili zetu zaidi.
1. Una uhakika kuwa ni kweli?
Wakati fulani zinapotokea taarifa motomoto na za ghafla
kama vile janga fulani, tukio la kusikitisha, mijadala ya kisiasa, vurugu,
ghasia, mauaji, maandamano na kadhalika, akili zetu hutahamaki na kuwa na
mwelekeo wa kuamini kile tunachokiona kwenye vyombo vya habari, iwe
televisheni, kompyuta, simu, magazeti na kadhalika.
Hata hivyo, jambo la busara ni kujizuia na kuziangalia
tena hizo picha ili kuwa na uhakika kuwa ni picha halisi au ni za kweli.
Picha unayoiona inawezekana ikawa haijahaririwa na ikawa
picha halisi, lakini una uhakika kuwa imeoneshwa kwenye muktadha halisi au
tukio halisi? Inawezekana ilipigwa wakati tofuati na kwenye tukio tofauti na
hilo unaloliona. Sasa kwa kuwa uwezo wa kugundua ni kipi sahihi na kipi sio
sahihi unaweza kuwa umetamalakiwa na mshtuko au taathira ya tukio hilo, tumia
muda wa ziada kupata uhakika na uthibitisho wa kile unachokiona.
2. Ni nani aliyetuma hiyo picha?
Je, unamjua mtu aliyetuma hiyo picha? Je, unamuamini? Kama
humjui, basi njia nzuri ya kujua kama mtu huyo anaaminika au la kwa kuangalia ujumbe
au picha za nyuma alizowahi kuzituma kwa watu. Kama akaunti yake ni mpya kwako,
basi kuwa makini! Kama picha ya kwenye ubao wa wasifu wake (profile) haikupi
taswira nzuri, basi ni bora kuwa na tahadhari.
3. Je, picha imefanyiwa mabadiliko na
marekebisho?
Unapoitazama picha kwa mara ya kwanza unaweza kudhani ni
picha halisi, lakini itazame tena. Je, unaona hitilafu zozote kwenye kivuli au
jinsi inavyoakisi? Njia bora kabisa ni kuangalia iwapo picha hiyo imefanyiwa mabadiliko
ni kuangalia mwanga.
Kuna njia rahisi ya kuiangalia picha hiyo iwapo unatumia
programu ya ‘Photoshop’. Bonyeza Image
> Adjustments > Hue/Saturation na kisha hamisha viwango vya Hue/Saturation kwenda kwenye ‘maximum’.
Iwapo unaona mabadiliko yoyote ya rangi yasiyoendana nayo au ncha zozote za
kidigitali kwenye picha hiyo, basi picha hiyo itakuwa ilifanyiwa mabadiliko
fulani.
4. Tazama nyuma ya picha
Tazama vizuri vitu vinavyoonekana kwenye hiyo picha:
angalia kwenye hiyo picha kama kuna magari, majengo, maandishi, nguo, mabango,
watu, na kadhalika. Tazama kitu chochote hapo kinachoweza kukupa shaka juu ya
usahihi na uhalisia wa picha hiyo. Thibitisha kuhusu hali ya hewa na mwanga wa
jua wakati wa tukio husika.
5. Una uhakika kuwa hujawahi kuiona hiyo
picha siku za nyuma?
Tafuta kwenye Google Images na TinEye ili
kuhakikisha kama picha hiyo iliwahi kutumika katika tukio linguine.
6. Ongeza uelewa wako kuhusu mitandao ya
kijamii
Kila mtu au taasisi inayosambaza taarifa hufanya juhudi
ya kuhakikisha watu wanayakubalia mawazo na fikra zake. Hakuna mtu asiyekuwa na
upande anaouegemea katika utoaji wa taarifa zake. Kila mtu ana itikadi zake, na
wakati fulani ukweli unaweza kupotoshwa kwa makusudi au hata kwa bahati mbaya.
Ili kuujua vizuri ulimwengu, tunahitaji kutafuta njia
madhubuti za kuelewa jinzi mitandao ya kijamii inavyofanya kazi. Tunatakiwa kujifunza
jinsi kile tunachokiona kinavyoweza kuwa sivyo kilivyo. Teknolojia ni nyenzo
kubwa ya ugunduzi na kuudhibiti ukweli. Kabla ya kuihamisha taarifa au
kubonyeza kitufe cha kuwaonesha watu kuwa waipenda, tafakari kwanza na
ujiulize: “Je hii taarifa ninayotaka kuisambaza ni taarifa sahihi au nami ni
sehemu ya utani wa mizaha ya mtandaoni
au kampeni ya upotoshaji wa taarifa?”
0 comments:
Post a Comment