![]() |
| Kijana akiwa amekamata kisu katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui, Februari 10, 2014. |
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bi. Catherine
Samba-Panza amesema kuwa serikali yake “itaingia vitani” dhidi ya wanamgambo wanaofanya
mauaji dhidi ya raia wenzao Waislamu nchini humo.
Katika hotuba yake aliyoitoa jana, alisema kuwa: “wanamgambo
wanadhani kuwa kwa sababu mimi ni mwanamke basi nitakuwa dhaifu. Sasa (wanamgambo
wa) ant-Balaka, ambao wanataka kufanya mauaji, watawindwa na kusakwa.”
Rais Samba-Panza aliongeza kuwa wanamgambo hao
wamepoteza maana ya harakati yao na kugeuka kuwa wauaji, wanyang’anyi na
kueneza ghasia.
Taifa hilo lenye watu wapatao milioni 4.6 lilifubikwa na
ghasia za kidini baina ya Wakiristo na Waislamu mwaka jana.
Hapo jana shirika la Amnesty International lilitoa
ripoti yake likisema kuwa kuna mauaji ya kiholela yanayoendeshwa dhidi ya jamii
ya Kiislamu nchini humo huku walinda amani wa kimataifa wakishindwa
kuyakomesha.
Shirika hilo la haki za binadamu limesema kuwa
limeorodhesha kwa uchache mauaji 200 dhidi ya Waislamu yaliyofanywa na
wanamgambo wa Kikristo katika eneo la magharibi la nchi hiyo.
"Mauaji ya kiholela dhidi ya jamii ya Kiislamu
yamekuwa yakifanyika katika eneo la magharibi la Jamhuri ya Afrika ya Kati,
ambalo ndilo lenye wakazi wengi zaidi nchini humo, tangu mapema Januari 2014,” Amnesty
imesema na kuongeza: “Jamii zote za Kiislamu zimelazimika kukimbia, na maelfu
ya raia Waislamu, ambao hawakufanikiwa kutoroka, wameuawa na wanamgambo
waliojipanga wa anti-Balaka.”
Zaidi ya watu 1,000 wameuawa katika Jamhuri ya Afrika ya
Kati tangu mwezi Desemba baada ya wanamgambo wa Kikristo kufanya mashambulizi
yaliyoratibiwa dhidi ya kundi la Seleka lenye Waislamu wengi, ambalo
liliiangusha serikali mwezi Machi mwaka 2013.
Umoja wa Afrika umeshatuma kikosi askari 5,400 kati ya
6,000 wanaotakiwa kusaidia kutuliza ghasia hizo. Askari wengine 1,600 kutoka
Ufaransa wameshatua katika nchi hiyo.

0 comments:
Post a Comment