Kesi ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe dhidi ya chama chake hicho
inatarajiwa kuanza kutajwa leo katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini alifungua
kesi hiyo dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa Chadema,
akiiomba mahakama hiyo ikizuie chama kujadili uanachama wake, hadi rufaa
anayokusudia kuikata Baraza Kuu la chama kupinga kuvuliwa nyadhifa,
itakaposikilizwa.
Katika kesi hiyo namba 1 ya 2014, Zitto pia aliiomba
mahakama hiyo imwamuru Katibu Mkuu wa Chadema ampatie mwenendo na taarifa za
Kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kilichomvua nyadhifa zote alizokuwa nazo ndani
ya chama na iwazuie walalamikiwa kumwingilia katika utekelezaji wa majukumu
yake kama Mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Kesi hiyo ambayo inasikilizwa na Jaji John Utamwa
imepangwa kuanza kutajwa leo kabla ya kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa
rasmi.
Tayari mahakama imeshatoa amri ya zuio la muda kwa
Chadema kumjadili na au kuchukua uamuzi wowote kuhusu uanachama wake.
Uamuzi huo ulitolewa Januari 7 na Jaji Utamwa, kutokana
na maombi ya Zitto, kupitia kwa Wakili wake Albert Msando.
Awali mawakili wa Chadema, Mwanasheria Mkuu wa chama
hicho, Tundu Lissu na Mkurugenzi wake wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu,
Peter Kibatala walipinga maombi hayo wakidai kuwa hayajakidhi matakwa ya kupewa
zuio la muda.
Katika uamuzi wake, Jaji Utamwa alikubaliana na hoja za
Wakili Msando kuwa maombi hayo yametimiza matakwa yote ya kupewa zuio hilo.
0 comments:
Post a Comment