![]() |
| Profesa Kaisi: Daktari wa kwanza kuzalisha kwa njia ya upandikizaji. |
NI Daktari alieonyesha moyo wa kuendelea na kazi licha
ya kupata maradhi ya kiharusi yaliyomsababishia kupooza mkono na mguu.
Hapana shaka kuwa maelfu ya wanawake nchini waliowahi
kupata huduma zake wanamkumbuka bado kwa msaada mkubwa aliowapa na kuwasaidia
kushika mimba, kuwapa ushauri wa kitaalamu au hata kuwazalisha.
Licha ya kustaafu, atabakia kukumbukwa kwa mengi hapa nchini, hasa kwa
mchango wake kwenye sekta ya afya ya mama na mtoto.
Huyu si mwingine, bali ni Profesa Malise Kaisi, Daktari Bingwa wa
Magonjwa ya Wanawake na Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha
Sayansi ya Tiba (Muhas). Nafika nyumbani
kwake maeneo ya Mikocheni jijini Dar es Salaam na ninamkuta akiwa amejipumzisha.
Anaanza kwa kunipa historia yake fupi
ya kikazi.
ATOA DAMU KUOKOA WAGONJWA
Nia ya daktari yeyote duniani, ni kuokoa maisha ya
mgonjwa. Hiyo ndiyo faraja ya wataalamu wa afya walio wengi.
Akiwa ni daktari ambaye anaipenda kazi yake, Profesa
Kaisi amewahi kujitolea damu kuwaokoa wagonjwa wake katika dakika ambazo
pengine walikuwa kwenye bonde la uvuli wa mauti.
“Unajua wakati ule, damu ilikuwa ni tatizo kubwa.
Hakukuwa na benki ya damu kama ilivyo sasa, hivyo unapopata mgonjwa anayehitaji
damu na yupo mikononi mwako, lazima ujitoe mhanga” anasema
Anakumbuka mwaka 1970 ambapo alimpokea mgonjwa aliyepata
ajali mbaya na alihitaji damu. Ilibidi ajitolee damu yake ili kumwokoa mgonjwa
yule.
“Nikiwa Newala mwaka 1970 huo huo, mgonjwa wangu
aliyekuwa anajifungua aliishiwa damu sana na ikabidi nitoe damu yangu haraka
sana na kumuwekea na alipona,” anasema
Mara nyingine
akiwa ndiyo kwanza ameripoti kwenye kituo kipya cha kazi huko Mtwara, alifika na
kumkuta mgonjwa akiwa kwenye hali mbaya na hakuwa na mtu wa kumpa damu hivyo
alikuwa akisubiriwa kufa, yeye alitoa damu yake na mgonjwa akapona.
“Cha muhimu ni kufahamu
kama una maambukizi au la. Ukishajijua, unatakiwa utoe damu kama wewe ni
daktari,” anasisitiza Profesa Kaisi.
AZALISHA KWA KUTUMIA IVF
Profesa Kaisi, ni daktari wa kwanza Mtanzania kuzalisha
kwa njia ya IVF hapa nchini na
kufanikiwa kusababisha mimba zaidi ya
11 kutungwa kwa njia hiyo.
IVF ni mchakato
wa utungishwaji wa mimba kwa upandikizaji wa mbegu za mwanamke na mwanaume
kwenye nyumba ya uzazi ya mwanamke.
Anasema akiwa na daktari kutoka Korea , Otman Bauer,
walifungua Kliniki ya majaribio mwaka
1989 ambayo ilikuwa ikiwasaidia wanawake
walioshindwa kushika ujauzito.
Wanawake
waliozalishwa kwa njia ya IVF ni wale
ambao walikuwa hawawezi kushika ujauzito kwa sababu kama vile mirija ya
kupitisha mayai kukatika, mayai kushindwa kupevushwa au kuwa na maradhi mengine
yanayozuia utungishwaji wa mimba.
IVF HUFANYIKAJE?
Profesa Kaisi anasema, yai la mama hupevushwa kwa kutumia dawa maalumu na hufuatiliwa kwa kutumia mashine ya uchunguzi wa ndani ya
mwili (ultrasound).
“Baada ya yai kukomaa, sindano maalum yenye wembamba
mithili ya unywele huingizwa ukeni hadi kwenye mirija na yai lililopevuka
huchukuliwa na kutolewa nje” anasema
Yai au mayai hayo
huwekwa kwenye chombo maalumu (test tube) kabla ya kuhamishwa kwenye beseni maalumu ambalo litalifanya
liendelee kuwa hai licha ya kutoka nje ya mwili wa binadamu.
“Beseni hilo halina budi kuwa na mazingira kama ya
mwilini, kwa mfano joto, mwanga na kusiwepo na sauti, kwani yai huweza
kuharibika kwa kasoro ndogo ndogo sana,” anasema
Anaongeza kuwa wakati huo mbegu za mwanaume hupimwa kama hazina
walakini na hutolewa kwa mwanaume
kujichua au kama hawezi kujichua basi hutakiwa kufanya tendo la ndoa na mke wake
na kisha mbegu kukingwa na kuwekwa kwenye chombo maalumu.
Mbegu za baba, hutakiwa kutolewa saa mbili mara baada
ya yai la mama kutolewa ili
visipishane. “Baada ya yai na mbegu
kutolewa, hatua inayofuata ni kuichoma
mbegu kwenye yai kwa kutumia sindano maalum. Mchakato huu unaitwa kwa
kitaalamu, Intra Cytoplasmic Sperm Injection au ICSI), ” anasema.
Anaeleza kuwa, baada ya mbegu na yai kuchanganywa,
huwekwa kwenye chombo maalum cha joto
kitaalamu ‘Incubator” kwa saa 40 kabla ya kuwekwa au kupandikizwa kwenye kizazi cha mama.
“Hali kadhalika,
‘incubator’ inatakiwa kuiga hali ya tumboni mwa mama wakati yai la mama na
mbegu za baba vinapowekwa kabla ya kuwekwa kwenye kizazi cha mama, kwa mfano
joto, mwanga na sauti” anasema Profesa Kaisi.
Hata hivyo,
Profesa Kaisi anasema IVF ina mafanikio makubwa kwa mtu yeyote isipokuwa
wanawake wenye umri wa miaka 40 na kuendelea .
Anaeleza zaidi kuwa, wanawake walio wengi hudhani kuwa
ni wagumba, lakini kumbe hawajafahamu matatizo yao.
UMUHIMU WA MADAKTARI
Profesa Kaisi anasema, bado madaktari nchini hawapewi
umuhimu unaolingana na kazi yao, bado hawathaminiwi kwa mchango wao.
Kwa mfano,
anasema, hakuna mtu anayejali kuwa madaktari hufanya kazi kwa saa 24 na wakati
mwingine kukosa wakati wa kupumzika hata na familia zao.
“Wakati mwingine mimi nilikuwa nakosa hata muda wa
kuonana na watoto wangu. Zinapita hata siku tano, sijawaona watoto” anasema
Anasema, viongozi wengi hawafahamu umuhimu wa madaktari
ndiyo maana wanakwenda kutibiwa nje.
HISTORIA YAKE
“Kabla ya kuingia chuo kikuu, nilibahatika kusoma Shule
ya Sekondari ya Wavulana Tabora, ambako nilisoma na Samwel Sitta (Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki), Joseph Mungai na Muhidin Ndolanga, ” anasema
Anasema alianza kazi Hospitali ya Muhimbili (sasa
Hospitali ya Taifa), mwezi Aprili mwaka 1969 baada ya kumaliza Shahada ya
Udaktari.
Profesa Kaisi, alishika nafasi hiyo hapo Muhimbili kwa
muda mfupi kabla ya kuhamishwa Hospitali ya Mawenzi iliyoko Moshi Mkoani
Kilimanjaro mwaka 1970. Mwaka 1971
alichaguliwa kuwa Daktari Mkuu wa Mkoa wa Mtwara (RMO).
Anasema alipata nafasi ya kujiendeleza kielimu ambapo
mwaka 1973 alikwenda Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba cha Muhimbili (Muhas) ambako
alibobea kwenye masuala ya tiba ya magonjwa ya wanawake hasa ugumba.
Kwa elimu hiyo, alikuwa ni daktari bingwa wa kwanza
nchini wa magonjwa ya wanawake.
Aliendelea na kazi hadi mwaka 1976 ambapo alitakiwa kuwa
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba (Muhas) kazi aliyoifanya hadi mkwaka
1998 alipostaafu.
Hata hivyo, kutokana na unyeti wa taaluma yake, Profesa
Kaisi hakustaafu moja kwa moja bali alipata mkataba wa kuendelea kufundisha
hadi serikali ilipotengua mikataba yao
Novemba mwaka jana.
Profesa Kaisi anasema, kutokana na kubobea kwenye
masuala ya uzazi kwa wanawake, aliamua kuanzisha huduma ya mama na mtoto ili kuwasaidia wanawake
vijijini.
“Niliomba fedha kwa wafadhili kwa ajili ya mafunzo kwa
wakunga ambao walikwenda mkoani Mtwara kuwasaidia wanawake walioathiriwa baada
ya vita iliyokuwa ikiendelea Msumbiji wakati huo” anasema
Anasema huduma hiyo ilisaidia sana wanawake wengi kupata
huduma ambayo ilipunguza vifo vya mama na mtoto maeneo ya vijijini.
Anamaliza kwa kusema: “Madaktari si mashetani wala
malaika, wanapogoma wasilaaniwe, bali
maslahi yao yaangaliwe upya kwani kazi yao ni ngumu.”
(Kwa hisani ya gazeti la Mwananchi)

0 comments:
Post a Comment