![]() |
| Zitto Kabwe |
JESHI la Polisi limempa ulinzi wa siri Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA) kama njia ya kumkinga asidhuriwe na maadui wake
katika siasa.
Hatua hiyo ya polisi imechukuliwa siku chache baada ya
mwanasiasa huyo kijana na mama yake mzazi, Shida Salum, kwa nyakati tofauti,
kudai kuwa Zitto amekuwa akiwindwa na watu ambao wamekuwa wakitishia uhai wa
wake kutokana na siasa zinazoendelea ndani ya Chadema.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi,
kiliiambia RAI kuwa uamuzi huo ulifikiwa katika kikao wiki iliyopita, baada ya
jeshi hilo kupata taarifa za tishio la kudhuriwa kwa kiongozi huyo kwa kile
kilichoelezwa kuwa tofauti baina yake na viongozi wenzake wa Chadema.
Kikao hicho ambacho kiliwahusisha makamishna kutoka
makao makuu ya jeshi hilo, kilipitia kwa kina taarifa ya kutaka kudhuriwa kwa
Zitto kwa kutofautiana msimamo na viongozi wenzake ndani ya chama hicho.
“Kikao kilifanyika Novemba 11 mwaka huu ambako pamoja na
mambo mengine kimeweza kujadili kwa kina kutaka kudhuriwa Zitto … hivyo
walitumwa makachero wa jeshi la polisi waweze kubaini anapoishi.
“Wamefanya kazi hii na sasa kiongozi huyo analindwa
kuanzia nyumbani kwake Tabata. Askari maalumu wamepewa kazi ya kuimarisha
ulinzi nyumbani kwake hadi katika nyendo zake,” kilisema chanzo hicho ndani ya
jeshi la polisi.
Zitto, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, kwa
muda mrefu amekuwa akitofautiana na viongozi wenzake hasa katika masuala ya
taifa hali inayofanya atafsiriwe kuwa anatumika kutaka kuivuruga Chadema.
RAI ilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania,
Advera Senso kupata uthibitisho wa uamuzi huo lakini alisema suala hilo liko
mikononi mwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
“Kwa jambo hili nakuomba mtafute Kamanda wa Mkoa husika,
yeye anaweza kukupa maelezo ya kina ya jambo hilo ndugu yangu au Kamanda wa
Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,” alisema Senso.
KOVA
Alipotafutwa jana, Kova alisema hawezi kukubali au
kukata kwa sababu suala hilo liko katika mamlaka ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Ilala, Marietha Minangi.
“Siwezi kusema ndiyo au hapana, nakuomba umtafute
kamanda wa mkoa husika atakupatia maelezo ya kina,”alisema Kamanda Kova.
KAMANDA WA ILALA
Kamanda Minangi alipoulizwa jana kuhusiana na suala
hilo, naye alimrushia mpira Kova akisema ndiye pekee anayeweza kutoa ufafanuzi
wa suala hilo.
“Jamani nawaomba suala hili mmtafute Kamanda Kova ndiye
anayeweza kulitolea ufafanuzi,”alisema Kamanda Minangi.
Kwa muda mrefu sasa, Zitto amekuwa akishutumiwa na
viongozi wenzake wa ngazi za juu katika Chadema akidaiwa kutengeneza ufa baina
yake na wazito ndani ya chama hicho tangu mwaka 2009.
Zitto amekwisha kuwahi kutangaza uamuzi wa kutaka
kuwania uenyekiti wa chama hicho aweze kupambana na mwenyekiti wake, Freeman
Mbowe.
Hata hivyo baadaye alijiondoa kuwania nafasi hiyo baada
ya wazee wa chama hicho kuingilia kati na kumsihi atumie busara kutogombea.
Katika siku za hivi karibuni, Zitto amejikuta akihusishwa
na kile kinachotajwa kuwa nyuma ya `usaliti’ unaodaiwa kufanywa na Mwenyekiti
wa Chadema Mkoa wa Arusha aliyesimamishwa, Samson Mwigamba.
Hata hivyo, Zitto alikanusha tuhuma hizo na kuwataka
viongozi wenzake kuelekeza nguvu kwa wanachama akisema malumbano hayatakijenga
chama.
Mbali na hilo, kwa muda mrefu Zitto amekuwa na msuguano
wa ndani na nje ya chama, hasa kutokana na misimamo yake.
Hivi karibuni, Mbunge Arusha Godbless Lema (Chadema)
aliibuka na kumtuhumu Zitto kwa uamuzi wake wa kutochukua posho za vikao
bungeni tofauti na msimamo alioutoa mwaka 2011.
Msuguano mwingine ni baina yake na vyama vya siasa kwa
msimamo wake wa kutaka vyama vyenye wabunge ambavyo vinapata ruzuku ya
serikali, viwasilishe ripoti ya ukaguzi wa hesabu zake kwa Msajili wa Vyama vya
Siasa.
Zitto ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu
za Serikali (PAC) pia aliwaonya viongozi wenzake kuacha propaganda kwa
kulichukulia suala hilo kuwa ni la siasa au lake binafsi.
Alisema anachokifanya ni kusimamia sheria kutokana na
nafasi yake kama mwenyekiti wa PAC.
Vyama vya siasa vinatajwa kuchukua ruzuku ya Sh bilioni
67.7, lakini havijaanika mchanganuo wa matumizi yake.
ATUA POLISI
Katika hatua nyingine, jana Zitto alisambaza ujumbe
kwenye mtandao wake wa jamii akisema amelazimka kwenda makao makuu ya jeshi la
polisi kutoa maelezo kwa kutishiwa kifo.
Katika ujumbe huo alindika: “Nimetoka makao makuu ya
upelelezi kuandika maelezo kuhusu vitisho dhidi yangu, kufuatia hekaya
inayoitwa ripoti ya siri ya Zitto Kabwe.
“Chanzo cha hekaya ya sasa kinabadilishwa kutoka makao
makuu ya Chadema na kuwa ni Usalama wa Taifa au Chama Cha Mapinduzi (CCM)”.
Taarifa hiyo ilisema wahusika wanaendelea kuhamisha
chanzo, lakini wanaopaswa kujua watasakwa, kukamatwa na kuburuzwa mahakamani.
“Nimewashtaki kwa kunitishia maisha, ninawashtaki kwa
kunichafua kwa tuhuma za uongo, nafanya haya kwa lengo la kuhakikisha siasa za
kuzushiana na kusambaza uongo zinakuwa na gharama kubwa,”ilisema taarifa hiyo.
MSIMAMO WAKE
Mwanasiasa huyo kijana ambaye amejipambanua kuwa mtetezi
wa misingi ya utaifa, raslimali za nchi, uchumi na masuala ya utawala bora
ndani na nje ya chama chake, alitoa msimamo wake kwa mara ya kwanza wiki
iliyopita alipohutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika uwanja wa Kolimba
wilayani Kaliua, Mkoa wa Tabora.
“Katika umri huu mdogo, nimepigwa mishale mingi ya
siasa, mimi ni binadamu nina damu, nikipigwa hii mishale damu inatoka,
ninaumia, sasa nimechoka kupigwa mishale, lazima sasa tuambiane ukweli,”
alisema Zitto.
Saa kadhaa baada ya hotuba yake hiyo, alisambaza tamko
la maandishi ambalo lilibeba ujumbe unaofanana na ule alioutoa Kaliua.
Awali katika mkutano wa Kaliua, Zitto alisema alikuwa hayuko
tayari kuendelea kukaa kimya pasipo kuchukua hatua zikiwamo za sheria wakati
akichafuliwa.
Alisema alikuwa ameshamwandikia barua Katibu Mkuu wake,
Dk. Willbrod Slaa akihoji iwapo taarifa ya kumchafua iliyosambazwa katika
mitandao ya intaneti chini ya kichwa cha habari kisemacho, “Taarifa ya Siri ya
Chadema” ni ya chama hicho au la.
Zitto aliyekuwa akizungumzia matokeo ya ziara yake ya
kufuatilia fedha zilizofichwa na baadhi ya Watanzania katika benki za Uswisi na
kwingineko Ulaya, alieleza kusikitishwa na kile alichodai kuwa ni kikundi cha
watu ndani ya Chadema ambacho kimekuwa mstari wa mbele kumpaka matope.
“Wakati nafanya kazi hii ya hatari ya kufuatilia hizo
fedha zilizofichwa nje ya nchi, navunjwa nguvu na watu ambao tuko chama kimoja
kwani imekuwa ni kawaida unapofanya siasa, lazima upate mashambulio na sasa
nashambuliwa na chama changu.
“Katika hali ya kawaida, wenzagu tulionao katika chama
ndiyo waliopaswa kunipa nguvu kwa vile tuna kazi kubwa ya kupambana na ‘lidude
likubwa linaloitwa CCM,” alisema Zitto.
Bila kutaja jina la mtu, alisema kuna watu wachache
ambao hawana kazi ndani ya chama hicho ambao shughuli yao imekuwa ni
kugonganisha viongozi wagombane.
Akirejea historia ya kuchafuliwa kwake, Zitto alisema
hali hiyo ilianza mwaka 2009 baada ya kujitokeza kutaka kugombea uenyekiti wa
Chadema akichuana na Freeman Mbowe.
CHANZO: Mtanzania

0 comments:
Post a Comment