MUASISI wa Chadema, Edwin Mtei ameelezea kusikitishwa na
yaliyomkuta Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, akisema kama kweli
amekutwa na hatia ya kusaliti chama chake, basi haikuwa akili yake, bali ‘alirubuniwa’.
Alisema anavyomfahamu yeye, Zitto ni kijana makini na
mwenye kujitambua.
Aidha, amesema kwa kuwa hakuhudhuria vikao vilivyobariki
kuvuliwa madaraka kwa Zitto, Dkt Kitila na Samson Mwigamba, kwa sasa hawezi
kuzungumza zaidi.
Alisema hayo jana kwa njia ya simu baada ya kutakiwa
kuzungumzia uamuzi wa chama alichokiasisi wa kuwavua madaraka viongozi hao
wenye nguvu na ushawishi kisiasa.
“Nasubiri nisikie wanazungumzaje kuhusu kuvuliwa kwao
madaraka, baada ya kutafakari nitakuwa na kitu cha kuzungumza, kama kutakuwa na
ulazima wa kufanya hivyo,” alisema.
BAREGU BADO YUPO
Kuhusu Uvumi wa mjumbe wa kamati Kuu ya Chadema, Profesa
Mwesiga Baregu kujiuzulu kama ilivyokuwa kwa Makamu Mwenyekiti, Said Arfi,
msomi huyo alisema hajafikiria kufanya hivyo.
Bali alikisihi chama hicho kuwaeleza kwa kina na
ukamilifu wanachama wake kwa nini kimefikia uamuzi wa kuwavua madaraka Zitto na
wenzake, badala ya kuwa na uamuzi mwingine.
Akizungumza kwa simu jana, Baregu alisema jambo muhimi
ni kwamba, Zitto na wenzake hawajafukuzwa uanachama, hivyo wana nafasi ya
kufanya mazungumzo ya maridhiano hususan katika mikutano mikubwa ya Baraza Kuu
au Mkutano Mkuu ambayo ina nafasi ya kukubali au kukataa uamuzi huo.
Aliwataka wanachama kuwa watulivu kwa sasa na kuelewa
sababu ya uamuzi huo na kutafakari ili wafanye uamuzi bila jazba au upendeleo.
Alisema kila chama kina katiba, taratibu na kanuni
katika utendaji kazi, hivyo Kamati Kuu ilikuwa na haki ya kufanya uamuzi huo,
lakini ni ushauri kwa vikao vya juu vilivyobaki.
0 comments:
Post a Comment