
Na Kabuga Kanyegeri, Istanbul
IRAN na mataifa sita yenye nguvu zimefikia makubaliano
kuhusu programu yake ya nishati ya nyuklia.
Akizungumza baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa siku
kadhaa mjini Geneva, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif,
amethibitisha kuwa hatimaye Iran na mataifa hayo wamefikia
makubaliano.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Laurent Fabius
na msemaji wa mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton, Michael
Mann, wametangaza kufikiwa kwa makubaliano hayo.
Makubaliano hayo yametangazwa leo baada ya mazungumzo
mazito baina ya Iran na mataifa ya Uingereza, China, Ufaransa, Urusi Marekani
na Ujerumani, ambayo yalikuwa yamepangwa kumalizika Ijumaa lakini yakaingia
siku ya tano.
Makubaliano hayo ya muda yanairuhusu Iran kuendelea na
shughuli zake kwenye vinu vya Arak, Fordo, na Natanz.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran,
makubaliano hayo pia yanabainisha kuwa hakuna vikwazo zaidi vitakavyowekwa
dhidi ya Iran kwa sababu ya programu yake ya nishati ya nyuklia.
Aidha, katika makubaliano hayo, Iran itaweza kupokea
dola bilioni 4.2 kama sehemu ya makubaliano hayo.
Mwakilishi mkuu wa Iran kwenye mazungumzo hayo, Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje Seyyed Abbas Araqchi, amesema kuwa kwa mujibu wa makubaliano
hayo, Iran itaendelea na programu yake ya urutubishaji wa madini ya urani.
Awali Araqchi alikuwa amesisitiza kuwa Tehran isingekubali
mpango wowote usiotambua haki ya nchi yake ya urutubishaji wa urani.
Makubaliano hayo ya aina yake yamefikiwa katika awamu ya
tatu ya mazungumzo baina ya Tehran na Mataifa makubwa tangu kuingia madaraki
kwa uongozi mpya wa taifa hilo chini ya Rais Hassan Rouhani aliyeingia
madarakani Agosti mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment