![]() |
Ghislaine Dupont (kushoto) na Claude Verlon |
WAANDISHI wawili raia wa Ufaransa wameuawa baada ya
kutekwa na watu wenye silaha katika mji mmoja kaskazini mashariki mwa nchi ya
Mali.
Taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje
ya Ufaransa ilisema kuwa waandishi hao ambao walikuwa wakifanya kazi idhaa ya Radio
France International (RFI), walikutwa na mauti katika nchi hiyo ya Afrika
Magharibi.
"Waandishi wa habari wa RFI, Claude Verlon na
Ghislaine Dupont walipatikana wakiwa wamekufa nchini Mali,” ilisema taarifa
hiyo na kuongeza kuwa walitekwa na kundi lenye silaha katika mji wa Kidal.
"Serikali ya Ufaransa, kwa ushirikiano na
mamlaka za Mali, itafanya kila juhudi kubaini mazingira ya vifo vyao mapema
iwezekanavyo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Mapema jana, duru kutoka kundi la waasi la National
Movement for the Liberation of Azawad (MNLA), na vikosi vya usalama vya
serikali ya Mali zilisema kuwa waandishi hao waliuawa katika viunga vya mji wa
Kidal.
"Dakika kadhaa baada ya kuwafuatiliaji
watekaji, tulitaarifiwa kuwa miili yao imepatikana ikiwa imepigwa risasi nje ya
mji,” alisema kiongozi wa mji wa jirani wa Tinzawaten, Paul-Marie Sidibe.
Chanzo kimoja kutoka ndani ya safu ya usalama wa
serikali ya Mali kilisema kuwa wawili hao waliuawa karibu kilometa 12 (maili 8)
nje ya mji, huku afisa mmoja mwandamizi wa waasi wa MNLA akisema pia kuwa miili
hiyo ilikutwa nje ya mji wa Kidal.
Wawili hao walitekwa nyara baada ya kufanya
mahojiano na mkazi mmoja wa Kidal, Ambeiry Ag Rhissa, aambaye ni afisa wa kundi
la MNLA katika eneo hilo.
Aidha, shirika la RFI lilithibitisha habari hizo na
kusema kuwa waandishi hao walipakiwa katika gari kabla ya kuwaua.
Idhaa hiyo imesema kuwa Verlon na Dupont walikuwa
wamekwenda Kidal kwa mara ya pili, huku mara ya kwanza ikiwa ni mwezi Julai
walipokwenda kuripoti kuhusu uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.
Mara hii walikuwa wamekwenda kutengeneza ripoti ya
matangazo maalumu yaliyokuwa yamepangwa kutangazwa Novemba 7, lakini sasa
programu hiyo imefutwa.
Kufuatia tukio hilo, Rais wa Ufaransa, Francois
Hollande alilaani mauaji hayo na kuyaita kuwa ni ya kinyama.
Ufaransa ilipeleka majeshi yake nchini Mali mnamo
Januari 11, 2013 katika kile ilichokiita kuwa ni kuwazuia waasi wa nchi hiyo
waliokuwa wakisonga mbele katika mapambano yao na kuhatarisha usalama wa Mali.
0 comments:
Post a Comment