![]() |
Rosweeter Kasikila (60) |
![]() |
Michael Christian (26) |
Hatimaye Mbunge Rosweeter Kasikila (60), aliyefunga
ndoa na kijana mwenye umri wa miaka 26, amefunguka kwa kusema aliyeng'ang'ania
kufunga ndoa hiyo ni kijana mwenyewe licha ya kumtahadharisha tofauti ya umri
wao.
Kasikila alitoa kauli hiyo jana, baada ya kutakiwa
kujibu shutuma zilizotolewa na mumewe huyo, Michael Christian (26) ya
kung'ang’ania vyeti vyake vya elimu kwa lengo la kumtaka arudi nyumbani.
Jana Christian alionesha nakala ya barua aliyoituma
kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuomba atumie uwezo
wake wa kisheria ili mbunge huyo amrudishie vyeti vyake alinavyovishikilia.
Kufuatia maelezo hayo, alimtafutwa Dk. Nchimbi kwa
njia ya simu ili athibitishe kupokea nakala ya barua hiyo lakini simu yake
ilikuwa imezimwa.
Nakala nyingine za barua hiyo zilitumwa kwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na Haki za Binadamu kwa jamii-Madhehebu ya dini
nchini, Askofu William Mwamalanga, Mchungaji wa Kanisa la Assembilies of God,
Mikocheni B, Mchungaji Getrude Rwakatare na vyombo vya habari.
Akijibu shutuma hizo, mbunge huyo alisema hajawahi
kung'ang'ania vyeti vya kijana huyo wala kulazimisha ndoa kama anavyodai
Christian.
"Nahisi kuna watu wanamtumia ili wanichafue,
siwezi kung'ang'ania vyeti, kwanza vya kazi gani kwangu, ukweli ni kwamba
Michael, shida yake anataka nichafuliwe, kwangu aliondoka wakati sipo, sasa
hivyo vyeti nimeving'ang'ania saa ngapi," alisema na kuongeza:
"Mwaka jana nikiwa Dodoma nilipata taarifa
ameondoka nyumbani, kweli nilivyorudi nilikuta amechukua vitu vyake vyote
kasoro tu vile nilivyomnunulia, hivyo vyeti anavyosema nimeving'ang'ania mbona
hajawahi kutamka mbele yangu zaidi nimeona kwenye magazeti," alihoji.
Alisema baada ya kufika nyumbani alipata taarifa
kuwa, mume wake huyo amepanga chumba na anaishi na mwanamke mwingine (askari)
ambaye ni mjamzito.
Alisema utaratibu alioutumia kijana huyo wa
kumchafua kwenye magazeti siyo sahihi na kumshauri angeenda mahakamani au
kanisani kama aliona haitaki ndoa tena.
Aliongeza kuwa yeye na Christian walifahamiana mwaka
2009 baada ya kufiwa na mume wake aliyemtaja kwa jina moja la Mushi.
"Sikumtongoza kama anavyosema, alikuja katika
hospitali ya Bagamoyo akitokea chuo cha Red Cross wakati huo nilikuwa Muuguzi
Mkuu, aliponiona alinipenda alianza kunitongoza, nilimkatalia na kumwambia mimi
ni mtu mzima sana kwake, " alisema na kuongeza:
"Alikuwa ananitumia email (barua pepe) za
kunitaka, nilimwambia umri wangu ni mkubwa, lakini yeye alikuwa ananiambia
kwenye vitabu vya dini kuna sehemu gani kumeandikwa umri," alisema.
Alisema alijikuta ametumbukia kwenye penzi la kijana
huyo na kuanza mahusiano naye.
"Nina nakala zote za vidhibitisho ambavyo
alikuwa akinitumia kunitongoza nimevichapisha kama vielelezo vyangu, tena
wakati tumeanza uhusiano Taasisi ya Safina ambayo ilikuwa ikimsaidia katika
masomo yake, ilinipigia simu," alisema na kuongeza:
"Safina walitaka kujua kama nina mahusiano na
huyu kijana niliwajibu ni kweli, waliniambia kama ndiyo hivyo wanafuta
kumsaidia kwa sababu wao huwasaidia wale ambao hawana uwezo, yatima, "
alisema.
Alisema wakati taasisi hiyo ikimfuta, ilikuwa
imemlipia Christian sehemu ya ada ya masomo aliyokuwa akiyachukua."
"Nililazimika kumlipia ada ya mwaka wa pili na
watatu wa masomo yake pamoja na mambo mengine na ilifika kipindi aliniambia
anataka kunioa, ndipo tulipofanya mchakato ambapo nilitolewa mahari na ndoa
ilifuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na kutangazwa mara tatu," alisema.
Alisema Christian alifuata taratibu zote ikiwa ni
pamoja na kutoa mahari ya Sh. 200,000 na baada ya harusi alipelekwa Kondoa kwa
ndugu wa kijana huyo.
"Huko tulienda kati ya mwezi Julai au Agosti,
mwaka jana, tulifanyiwa sherehe za kimila na ndugu za mume wangu ambao ni baba
mdogo, bibi mzaa baba yake na shangazi, pia ndugu zake wa Kimara na Dodoma
wananijua, " alisema.
Hata hivyo, mbunge huyo alipoulizwa kama ndoa hiyo
ipo sasa hasa kufuatia shutuma hizo, alisema hawezi kujua kwa sababu mume wake
aliondoka bila kumuaga na kwa sasa anaishi na mwanamke mwingine toka Novemba
mwaka jana.
Alisema wakati wa mahusiano yao wafanyakazi wenzake
Christian walikuwa wakimhoji kwa nini ameamua kuwa na mtu mzima kama (mbunge),
lakini yeye aliwajibu hakuna umri kwenye biblia.
Alipoulizwa kama ana mpango wa kuchukua hatua dhidi
ya kijana huyo, mbunge huyo alisema hana mpango.
Mbunge huyo alijitetea kuwa, hakumlazimisha kufunga
ndoa na kwamba wakati kijana huyo akimtongoza, alimweleza kuwa hawezi kuzaa kwa
sababu umri wake umeshapita.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment