![]() |
| Waandamanaji wanaoipinga serikali wakipeperusha bendera za taifa mjini Bangkok, Novemba 25, 2013 |
WAANDAMANAJI wanaoipinga serikali nchini Thailand
wametishia kuwa watazikamata wizara zote baada ya kuingia kwa nguvu katika majengo
ya wizara ya fedha.
Waandamanaji hao waliokuwa na hasira waliingia kwa nguvu
katika majengo ya wizara ya fedha na kulizingira eneo hilo wakimlazimisha
Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Yingluck Shinawatra, ajiuzulu.
Waaandamanaji wanadai kuwa utawala wa Yingluck unadhibitiwa
na kaka mkubwa wa Waziri Mkuu huyo, Thaksin Shinawatra, aliyewahi kuwa Waziri
Mkuu wa nchi hiyo na kuondolewa na jeshi.
“Kesho tutazikamata wizara zote ili kuuonesha ukoo wa Thaksin
kwamba hawana hati miliki ya kuongoza nchi hii,” alisema kiongozi wa upinzani, Suthep
Thaugsuban, akiwahutubia waandamanaji mjini Bangkok.
Maandamano hayo yamechochewa na hatua ya serikali
kupeleka muswada bungeni ambao utatoa msamaha kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi
hiyo, Thaksin Shinawatra, ambaye anatuhumiwa kwa ufisadi na kutomheshimu mfalme
anayetambuliwa na katiba ya nchi hiyo, Mfalme Bhumibol Adulyadej.
Thaksin Shinawatra aliondolewa madarakani mwaka 2006 katika
mapinduzi ya jeshi kufuatia ugombaniaji wa madaraka baina ya wafuasi wake na
wapinzania wake.
Waziri Mkuu huyo wa zamani amekuwa akiishi uhamishoni
kwa miaka mitano sasa kwa hofu ya kushitakiwa na kutumikia kifungo gerezani kwa
makosa ya ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma.

0 comments:
Post a Comment