MFANYABIASHARA maarufu mjini Tabora, Hakimu Hamdun,
mkazi wa Kata ya Kanyenye anashikiliwa na Polisi akituhumiwa kujaribu kujiua
kwa kujipiga risasi kutokana na wivu wa mapenzi.
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Kamishna Msaidizi Peter
Ouma, alisema jana kuwa Hamdun alijaribu kujiua kwa risasi wiki iliyopita saa
kumi na mbili jioni nyumbani kwake eneo la Kanyenye mjini Tabora.
Alisema kuwa Hamdun ambaye kwa sasa amelazwa katika
Hospitali ya Mkoa Kitete kwa matibabu, alijipiga risasi baada ya mkewe aliyempa
talaka mbili, kumtaka afuate utaratibu wa ndoa ili warudiane.
Inadaiwa Hamdun alimpa talaka mbili mtalaka huyo, Joha
Binti Sudi, lakini baadaye alibadilisha mawazo na kumtaka warudiane huku
akimtishia kumuua kama asipokubali.
Kwa mujibu wa madai ya Kamanda Ouma, wanandoa hao
waliotalikiana walikuwa wakiishi nyumba tofauti na Hamdun aliamua kumfuata
mwanamke alipokuwa akiishi akiwa na gari lake na kumtaka warudiane.
Hata hivyo, alidai mwanamke huyo alikataa kurudiana
kiholela na kumtaka Hamdun kama kweli anampenda, afuate utaratibu wa Dini ya
Kiislamu ndipo watimize azma yao hiyo ya kurudiana.
KUJIUA
Badala ya kufuata utaratibu, inadaiawa hamdun alienda
kwenye gari lake na kuchukua bunduki aina ya Shot gun na kwenda nyumbani kwake
ambapo alifunga milango, akajipiga risasi katika ubavu wa kushoto.
Kwa mujibu wa Kamanda Ouma, mtuhumiwa huyo hali yake
inaendelea vizuri lakini amepoteza sifa ya kumiliki bunduki na hivyo hatapewa
tena.
Aidha, Hamdun atakapomaliza matibabu atafikishwa
mahakamani kujibu mashitaka yake ikiwemo ya kutishia kuua na jaribio la kutaka
kujiua.
CHANZO: Habari Leo

0 comments:
Post a Comment