
Na Kabuga Kanyegeri, Istanbul
MISRI imemtaka balozi wa Uturuki kuondoka nchini humo na
kuituhumu Ankara kuwa inaunga mkono makundi yanayoyumbisha uthabiti wa nchi,
tuhuma ambazo zinaonekana kuelekezwa Uturuki kuwa inakiunga mkono chama cha
rais aliyeondolewa madarakani, Muhammad Mursi.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imesema kuwa balozi wa
Uturuki nchini humo hatakiwi na kutaka aondoke kwa sababu ya kile
ilichokielezea kuwa Uturuki imeendelea “kuingilia” mambo ya ndani ya Misri.
CHANZO CHA MGOGORO
Uturuki imekuwa mkosoaji mkubwa dhidi ya hatua hiyo ya
kuondolewa kwa Mursi, na kukiita kitendo hicho kuwa ni “mapinduzi
yasiyokubalika”.
Mwezi Agosti Uturuki na Misri ziliwaita mabalozi wao kwa
muda baada ya Uturuki kushutumu vikali kitendo cha jeshi kumuondoa Mursi
madarakani na operesheni kali iliyoongozwa na jeshi hilo kuyadhibiti maandamano
ya kumuunga mkono Mursi. Baada ya hapo balozi wa Uturuki alirejea wiki mbili
baadaye, lakini Misri iligoma kumrejesha balozi wake Ankara.
Chama cha Mursi cha Udugu wa Kiislamu, ambacho kimekuwa
kikiitisha maandamano kikitaka Mursi arejeshwe madarakani, kinadaiwa kuwa na
uhusiano wa karibu na chama tawala cha Uturuki cha Haki na Maendeleo (AKP).
UTURUKI YAJIBU MAPIGO
Uturuki imejibu mapigo ya Cairo kwa kutangaza kuwa
balozi wa Misri ni mtu “asiyetakiwa” katika dalili mpya inayoashiria kukua kwa
mgogoro baina ya mataifa hayo mawili yenye nguvu katika eneo la mashariki ya
kati na ambao ni washirika wakubwa wa Marekani, mgogoro uliosababishwa na hatua
ya jeshi la Misri kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Muhammad
Mursi mnano Julai 3 mwaka huu.
Wizara ya mambo ya Nje ya Uturuki, katika taarifa yake,
imesema kuwa imesikitishwa na hali hiyo, lakini ikasema kuwa utawala wa mpito
wa Misri utahukumiwa na historia kwa sababu uliingia madarakani kwa mazingira
yasiyokuwa ya kawaida ya mapinduzi ya Julai 3.
Katika radiamali yake kwa msimamo wa Misri, Rais wa
Uturuki, Abdullah Gül alizungumza kwenye televisheni ya taifa, TRT, na kusema
kuwa: “Ninatumai uhusiano wetu utarejea katika hali yake ya kawaida.”
Rais Gül alielezea matarajio yake kuwa kipindi cha
mgogoro huo wa kidiplomasia ni cha mpito na kwamba Uturuki inatarajia kuwa muda
si mrefu Misri itarejea kuwa nchi ya kidemokrasia.
Mnamo Agosti 15, Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip
Erdogan, alitoa wito wa kufanyika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la
Umoja wa Mataifa kujadili operesheni kali ya jeshi la Misri dhidi ya waandamanaji
wanaomuunga mkono rais aliyepinduliwa, Muhammad Mursi.
Taifa hilo la Kiarabu liliangukia katika machafuko
makubwa mwezi Julai baada ya jeshi kumuondoa madarakani rais wa kwanza
kuchaguliwa kidemokrasia, bunge likavunjwa, matumizi ya katiba yakasitishwa, na
kumtangaza mkuu wa Mahakama Kuu ya Katiba, Adly Mahmoud Mansour, kuwa rais wa
mpito.
Serikali ya Mansour imeanzisha operesheni kali dhidi ya
wafuasi wa Mursi na imewakamata wanachama 2,000 wa vuguvugu la udugu wa
Kiislamu, akiwemo kiongozi mkuu wa vuguvugu hilo, Muhammad Badie.
Zaidi ya watu 1,000 waliaua ndani ya wiki moja katika
ghasia baina ya wafuasi wa Mursi na vikosi vya usalama baada ya polisi kuzivunja
kambi za waandamanaji katika operesheni kali ya Agosti 4.
Mauaji hayo yaliibua lawama ya kimataifa na kuzifanya
taasisi mbalimbali za kimataifa kutoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi huru
kuhusu ghasia hizo.
0 comments:
Post a Comment