1. Katika kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kilichofanyika
tarehe 20-22 Novemba 2013, pamoja na mambo mengine, kulijadiliwa waraka wa siri
unaojulikana kama Mkakati wa Mabadiliko 2013. Waraka huu ulilenga kujenga hoja
ya kufanya mabadiliko ya uongozi na kuanisha mikakati ya ushindi kwa mgombea
mlengwa katika uchaguzi mkuu ndani ya CHADEMA. Nilikiri kuwa nilikuwa naufahamu
waraka huu, na kwamba nilishiriki kuuandaa na kuuhariri, na kwamba mimi ni
mmoja wa wanachama wanaoamini kwamba kuna haja ya kubadilisha uongozi wa juu wa
chama katika uchaguzi ujao ndani ya chama.
2. Katika mjadala, maudhui ya waraka huu yalionekana kwa
wajumbe kwamba yalikuwa na mapungufu na yalikiuka misingi na kanuni
zilizoanishwa katika Katiba ya Chama. Kwa kuwa katika chama cha siasa hoja za
watu wengi ndizo hupewa uzito, na kwa kuwa dhamira na nia yangu ndani ya chama
hiki imekuwa ni kusukuma mabadiliko ambayo watanzania wanayatazamia nje ya
mfumo wa sasa wa utawala, nilikiri makosa yangu na kuwaomba msamaha wajumbe wa
Kamati Kuu na viongozi wakuu wa chama, na kueleza kwamba nilikuwa tayari
kujiuzulu na kubaki kuwa mwanachama wa kawaida. Wajumbe walikataa kukubali ombi
langu la kujizulu bali walipitisha azimio la kunivua mimi na Mhe. Zitto Zuberi
Kabwe nafasi zetu za uongozi. Nilipokea kwa unyenyekevu adhabu ya kuvuliwa
nafasi zote za mamlaka nilizokuwa nazo ndani ya chama hiki na kueleza kuwa
nitaendelea kutoa mchango wangu kama mwanachama wa kawaida hadi hapo chama
kitakapoona ninafaa kukitumikia katika nafasi yeyote.
3. Kufuatia mkutano wa waandishi wa habari siku ya
Ijumaa tarehe 22 Novemba 2013 ambapo, pamoja na mambo mengine, ilielezwa na
viongozi wa CHADEMA kwamba mimi na wenzangu (Samson Mwigamba na Zitto Kabwe)
tumehujumu chama na tumefanya uhaini kwa kuandaa mkakati wa ushindi kwa mgombea
tunayemtaka, ningependa nieleza mambo yafuatayo:
a. Siamini hata kidogo kwamba kugombea nafasi yeyote
iliyo wazi ndani ya chama cha siasa ni uhaini na hujuma. Msingi namba moja wa
CHADEMA ni demokrasia na hakuna namna ya kudhihirisha mapenzi kwa demokrasia
zaidi ya kuruhusu ushindani katika nafasi za uongozi na hasa uongozi wa juu
kabisa. Hiki kinachoitwa uhaini ni wasiwasi wa siasa za ushindani katika chama
chetu.
b. Sijawahi na sitarajii kushiriki vitendo vyovyote vya
kuhujumu chama changu cha CHADEMA na harakati za mabadiliko hapa nchini. Chama
hiki kiliniamini katika nafasi nyingi nyeti sana na kama mie ningekuwa mhujumu nilikuwa
na fursa nzuri za kufanya uhujumu huo. Nimeshiriki kuandaa ilani ya chama ya
2010-2015, kuratibu kampeni za mwaka 2010 nikiwa makamu mwenyekiti wa kampeni
chini ya Profesa Baregu na nilishiriki kutengeneza na kusimamia utaratibu mzuri
wa kupata wabunge wa viti maalumu katika chama chetu. Zote hizi ni nafasi nyeti
mno ambazo kamwe huwezi kumkabidhi mtu ambaye ni ‘mhaini’ na ‘mhujumu’.
Nilishiriki katika shughuli za chama kwa kiwango ambacho nilijisababishia
matatizo makubwa katika familia yangu na kazini, lakini sijawahi kutetereka na
sijaterereka. Nilifanya yote haya kwa mapenzi yangu ya dhati na imani yangu kwa
CHADEMA kwamba ndicho chama kinachostahili kuongoza harakati za mabadiliko hapa
nchini kwa sasa.
c. Nasikitika kwamba nimesababisha usumbufu kwa viongozi
wangu wa CHADEMA kutokana na dhamira yangu ya kutaka mabadiliko ya uongozi
ndani ya chama chetu kwa njia halali za kidemokrasia. Nilifanya hivi kwa imani
niliyo nayo kwa misingi ambayo CHADEMA inasimamia, ikiwemo demokrasia, na imani
yangu kwamba chama hiki kinahitaji kufanya mabadiliko makubwa katika uongozi wa
juu wa chama, ikiwa ni maandalizi muhimu kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Nasisitiza tena kwamba siamini hata kidogo kwamba matamanio ya mabadiliko ya
uongozi ndani ya chama, na kuandaa mikakati ya kufikia matamanio hayo kwa njia
za kidemokrasia ni uhaini.
d. Tunaweza kujifunza kutokana na historia. Siasa za
ushindani ndani ya vyama katika nchi hii sio kitu kigeni. Enzi za TAA na kabla
TANU haijazaliwa wanachama walikuwa wanagawana nafasi za uongozi mezani. Lakini
mwaka TANU ilipozaliwa (mwaka 1954) kulikuwa na uchaguzi mkali sana kwa nafasi
ya uenyekiti. Mwalimu Nyerere alimshinda Mzee Skyes kwa kura chache sana. Rais
Obama wa Marekani alianza mkakati wa kushinda uteuzi wa kugombea nafasi ya
urais kupitia chama chake cha Democrat mapema kabisa mwaka 2006 kupitia waraka
maalumu wa siri ulioainisha mikakati yake. Waraka huu uliandaliwa na watu wanne
tu bila yeye mwenyewe kujua. Waandaji wa mkakati huu walikuja kumshirikisha
baadaye mwaka 2007 na kumshawishi yeye ajitokeze kugombea dhidi ya Hillary
Clinton aliyekuwa anachukuliwa kama mrithi halali wa kiti cha urais. Yaliyobaki
ni historia. Hivi ndivyo ambavyo siasa za ushindani ndani ya vyama hatimaye
huzaa wagombea na viongozi imara katika nchi.
e. Zitto Zuberi Kabwe hajafukuzwa kwa sababu ya waraka
huu kwa sababu yeye hakuhusika kwa namna yoyote kuuandaa, ingawa alikuwa ni
mlengwa mkuu. Yeye amefukuzwa kwa sababu ambazo yeye atazieleza na ambazo
viongozi wa CHADEMA hawakuzieleza katika mkutano na waandishi wa habari.
f. Napenda ijulikane kwamba sikuomba kujiuzulu kwa
sababu ya kuogopa aibu ya kufukuzwa. Niliomba kujiuzulu kwa sababu nilitambua
kwamba wenzangu katika Kamati Kuu walikuwa hawana imani nami tena, na ni
uungwana kujiuzulu mkifika mahala hamuaminiani. Nilitambua vilevile kwamba, kwa
mujibu wa Katiba yetu, Kamati Kuu ilikuwa haina uwezo wa kunivua nafasi yangu
moja kwa moja.
Kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA, Sura ya Sita, Ibara ya
6.3.6 (b), inasomeka hivi “Kiongozi aliyeteuliwa na vikao vya uongozi ataweza
kusimamishwa au kuachishwa uongozi na kikao kilichomteua”. Mimi nilichaguliwa
na Baraza Kuu na ni kikao hiki pekee chenye uwezo wa kunivua nafasi niliyokuwa
nayo. Ninaamini wajumbe wa Kamati Kuu walipitiwa katika hili kwa sababu siamini
kwamba hawajui takwa hili la kikatiba ukizingatia kwamba ndani yake kuna
wajumbe waliobobea kabisa katika tasnia ya sheria.
4. Hiki kilichotokea ndani ya chama sio kitu kibaya.
Vyama vingi imara hupitia katika migogoro na misukosuko kama hii na zaidi.
Naamini tutavuka na tutakuwa imara zaidi. Muhimu ni kwamba ni lazima
tuaminiane. Katika kuaminiana sio lazima tufanane kimawazo na kimtazamo kwa
sababu hili ni jambo lisilowezekana kibinadamu na zaidi katika siasa.
5. Ninapohitimisha, ninawasihi wanachama wa CHADEMA na
wapenzi wa mabadiliko popote walipo wapiganie kwa dhati MISINGI mama ya CHADEMA
ikiwemo demokrasia ndani ya chama. Hakuna namna ambavyo chama chochote kinaweza
kushawishi umma kwamba kitapigania demokrasia katika nchi wakati kinayahainisha
mapambano ya kidemokrasia ndani ya chama chenyewe.
Kukataa siasa za ushindani ndani ya chama ni kuhujumu
demokrasia na ni usaliti kwa misingi mama ya chama ambayo ni uhuru wa kweli na
mabadiliko ya kweli. Hisia za usaliti na umamluki zilitumika enzi za ukomunisti
katika kunyamazisha wapinzani ndani ya vyama vya siasa na katika nchi. Zilikuwa
ni njia haramu zilizozoeleka ambazo hatimaye zilizaa udikteta wa kutisha katika
mataifa ya kikomunisti. Tusikubali utamaduni wa kuhisiana usaliti na umamluki
ukaota mizizi katika chama chetu na katika nchi kwa sababu utaua demokrasia na
mfumo wa vyama vingi utakuwa hauna maana tena.
6. Nitafuata taratibu zote za chama kama zilivyoelekezwa
na Kamati Kuu na kwa mujibu wa katiba yetu, na nitashiriki kikamilifu katika
kutuliza hali ya kisiasa ndani ya chama ili kuhakikisha kwamba tunabaki imara,
na CHADEMA inaendelea kuwa tumaini la watanzania.
Mungu ibariki Tanzania.
Dkt. Kitila Mkumbo
Dar es Salaam
Jumapili, 24 Novemba 2013.

0 comments:
Post a Comment