Na Kabuga Kanyegeri, Istanbul
WAZIRI Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan, ameendelea
kushikilia msimamo wake wa kutoutambua utawala wa mpito wa Misri akisema kuwa
haukuchaguliwa na wananchi.
Akizungumza katika jimbo la Trabzon kwenye pwani ya
Bahari Nyeusi, Erdoğan alisisitiza msimamo wake kuwa kamwe hatawaheshimu wale
wanaongia madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi.
"Tuko upande wa wananchi wa Misri wanaodhulumiwa. Tuko
upande wa wale waliokuwa katika medani ya Rabaa al-Adawiya," alisema, akiwakusudia
wale walioandamana katika uwanja wa Rabia mjini Cairo kupinga hatua ya jeshi la
nchi hiyo kumuondoa madarakani rais Muhammad Mursi.
Katika kuonesha msimamo wake ambao amekuwa nao tangu
mapinduzi hayo, alinyosha juu mkono wake akiwa amevikunjua vidole vinne ambavyo
hutumika kama ishara ya wale wanaopinga mapinduzi hayo nchi Misri.
“Hatukuwahi kuwaheshimu wale waliofanya mapinduzi na
kamwe hatutafanya hivyo. Tutaendelea kuheshimu matakwa ya wananchi, hapa kwetu
na popote pale duniani. Ndio maana msimamo wetu upo wazi na tupo makini sana na
suala hili.”
Aidha, Erdoğan amekosoa vikali hatua ya jeshi kuingilia
siasa akielezea kuwa jeshi linapaswa kukaa nje ya siasa na kuangalia majukumu
yake.
Uhusiano wa kidiplomasia umeingia katika sura mpya baada
ya hapo jana Misri kumfukuza balozi wa Uturuki nchini humo kwa kile ilichoeleza
kuwa Ankara imeendelea kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo kwa kuyaunga mkono
makundi iliyoyaelezea kuwa yanayumbisha uthabiti wa nchi, yaani vuguvugu la
Udugu wa Kiislamu. Uturuki ilijibu mapigo kwa kumfukuza balozi wa Misri nchini
humo.
Uturuki imekuwa mkosoaji mkubwa wa watawala wa Misri na
msimamo wa Erdoğan umekubwa mwiba kwa utawala wa Cairo, ambao unajaribu
kutuliza hali ya mambo iliyofuatia kuondolewa madarakani kwa rais
aliyechaguliwa na wananchi, Muhammad Mursi, ambapo jeshi lilimchagua mkuu wa
mahakama ya katiba, Adly Mahmoud Mansour kuwa rais wa mpito, likavunja bunge na
kusimamisha matumizi ya katiba.

0 comments:
Post a Comment