TAARIFA YA ZITTO ZUBERI KABWE (MB) KUHUSU KUVULIWA
NAFASI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA CHANGU CHA CHADEMA
1. Utangulizi
Katika kikao chake cha siku mbili kilichofanyika tarehe
20 - 22 Novemba 2013, Kamati Kuu ya CHADEMA, pamoja na mambo mengine, iliazimia
kunivua nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama. Kwa mujibu wa taarifa ya
chama iliyotolewa katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa tarehe
22 Novemba 2013, ilielezwa kwamba sababu za kuvuliwa uongozi mimi na Dk Kitila
Mkumbo ni uhaini na hujuma kwa chama kutokana na waraka unaojulikana kama
mkakati wa uchaguzi 2013. Ukweli ni kwamba waraka uliotajwa si sababu ya mimi
kuvuliwa nafasi zangu za uongozi kama ilivyojadiliwa katika Kikao cha Kamati
Kuu . Sababu za kufukuzwa kwangu kama zilizojadiliwa katika kikao cha Kamati
Kuu ni tuhuma lukuki ambazo si mara yangu ya kwanza kuzisikia zikijadiliwa
ndani na nje ya vikao vya chama. Hitimisho la tuhuma hizi ni kwamba mimi
nimekuwa nikikisaliti chama kwa kutumika na CCM na Usalama wa Taifa.
Nitazianisha tuhuma hizi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika
vikao mbalimbali vyama.
Ninatambua kwamba chama changu kinapita katika wakati
mgumu sana sasa hivi. Nataka nitamke mapema sana kwamba mimi Zitto Zuberi Kabwe
sitokuwa chanzo cha CHADEMA kuvunjika. Hiki ndicho chama kilichonilea na
kunifikisha hivi nilivyo. Ningependa chama hiki mtoto wangu atakapokuwa mtu
mzima na atakapoamua kujiunga na siasa aingie CHADEMA. Bado nina imani kubwa na
chama changu na ninaamini ndicho kinachostahili kuendesha nchi jana, leo na
kesho.
2. Kuhusu tuhuma mbalimbali zinazo elekezwa kwangu
Zipo tuhuma nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa
katika vikao vya chama na nje ya vikao na baadhi ya viongozi wenzangu. Tuhuma
hizi zinalenga kuonyesha kwamba mimi ni mbinafsi na kwamba ninapokea rushwa ili
kukihujumu chama changu. Nitazianisha tuhuma kwa kifupi na kuzijibu kama
ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vya chama.
i) Tuhuma kwamba sikushiriki kumpigia kampeni mgombea
wetu wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2010. Ningependa kueleza yafuatayo
kuhusu jambo hili:
Mimi nilikuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la
Kaskazini huko Kigoma.
Pamoja na kuwa mgombea wa ubunge, nilifanya kampeni
katika majimbo mengine 16 katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam,
Mtwara, Pwani, Shinyanga, Mara na Rukwa. Hakuna kiongozi yeyote wa juu
aliyefanya kampeni katika majimbo mengi kama mimi, ukiacha mgombea urais.
Kote nilipopita nilimpigia kampeni wagombea wetu wa
udiwani, ubunge na Rais.
Katika Mkoa wa Kigoma nilizunguka na mgombea urais
katika kata zote za Kigoma Kaskazini na majimbo yote manane ya Mkoa wa Kigoma.
ii) Tuhuma kwamba katika Mkoa wa Kigoma nilishindwa
kuwapigia kampeni wagombea wetu kiasi kwamba peke yangu ndiye niliyeshinda
katika uchaguzi huo. Ukweli ni kwamba niliwapigia sana kampeni wagombea wetu,
na hivyo ndivyo wapiga kura wa Kigoma walivyoamua.
iii) Tuhuma kwamba nilishiriki kuwashawishi wagombea
wetu katika baadhi ya majimbo kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili
kuwapisha wagombea wa CCM wapite bila kupingwa kwa njia ya rushwa. Majimbo
yanayotajwa ni pamoja na Sumbawanga, Musoma Vijijini na Singida Mjini. Kama
nilivyokwisha kueleza katika vikao mbalimbali vya chama jambo hili si la kweli
na hakuna popote ambapo watoa tuhuma hizi wamewahi kutoa ushahidi kwamba
nilifanya jambo hili. Nipo tayari kwa uchunguzi ndani ya chama na watoa tuhuma
waje na ushahidi bayana wa jambo hili. Si afya kwa chama kuendelea kurudiarudia
tuhuma hizi kila mara tangu mwaka 2010 bila uchunguzi wowote kufanyika na jambo
hili lifikie mwisho.
iv) Tuhuma kwamba nimekuwa sishiriki katika operesheni
mbalimbali za chama: Ukweli ni kwamba nimeshiriki sana katika operesheni
mbalimbali za chama ndani na nje ya nchi. Kwa mfano, mwaka 2011 tulikuwa na
operesheni kubwa katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na nilikwenda
katika mikoa yote tuliyotembelea. Mwaka 2012 baada ya hoja ya mkonge bungeni
nilifanya ziara Mkoa wa Tanga. Mwaka 2012 kulikuwa na operesheni kubwa moja
katika mikoa ya kusini ya Mtwara na Lindi. Operesheni hii sikushiriki kwa
sababu nilikuwa nchini Marekani kufungua matawi kwa mwaliko wa Watanzania
wanaoishi huko.
v) Tuhuma kwamba nimekidhalilisha chama kwa tamko la PAC
kwamba Hesabu za Vyama hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG): Katika jambo hili ninatuhumiwa kwamba mimi kama Naibu Katibu
nilipaswa kuwasiliana kwanza na viongozi wa chama 'kuwatonya' ili wajiandae.
Kwamba kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na kukiweka kundi moja na CCM na
nastahili kuadhibiwa vikali kwa kuwa katika taarifa yangu nilikuwa na nia mbaya
na chama chetu. Maelezo yangu niliyoyatoa na ambayo ningependa kuyakariri hapa
kuhusu jambo hili ni kama ifuatavyo:
Utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya
uenyekiti wa PAC kulinda chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni
kuendeleza tabia zile zile ambazo tunazipinga na ambazo tunapigania
kuzibadilisha
Napenda kusisitiza kwamba hakuna chama ambacho kimewahi
kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Natambua kwamba
mahesabu ya chama changu yamekuwa yakikaguliwa na wakaguzi wa nje kwa utaratibu
tuliojiwekea. Lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama vya siasa
hayajakaguliwa na CAG, na hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa hili ni la
nani.
vi) Tuhuma kwamba mimi ni mnafiki katika kukataa kwangu
kuchukua Posho za Vikao
Mtakumbuka kwamba mimi nilikataa kuchukua posho tangu
mwaka 2011 kama ishara ya kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chetu wa
kupinga posho za kukaa na matumizi mengine yasiyofaa katika fedha za umma kama
ilivyoanishwa kwenye Ilani yetu ya mwaka 2010-2015. Mtakumbuka kwamba hivi
karibuni Mheshimiwa Lema amenishutumu kwamba kukataa kwangu kuchukua posho ni
unafiki kwa sababu ninapokea posho kubwa zaidi katika mashirika ya umma ambapo
mimi ni mwenyekiti wa kamati husika. Ninapenda kueleza yafuatayo kuhusu jambo
hili:
Sipokei posho yeyote ya vikao (sitting allowance) ndani
na nje ya Bunge tangu mwaka 2011. Hii ni pamoja na vikao vyote katika Kamati za
Bunge ninavyohudhuria. Mtu yeyote mwenye ushahidi vinginevyo auweke hadharani.
Swala la kukataa posho (sitting allowance) ni swala la
kiilani katika chama chetu, na kwangu ni swala la kimisingi zaidi. Katika
Wilaya yangu vifo vya kina mama wajawazito ni 1900 kati ya wanawake 100,000
wenye ujauzito. Vifo hivi vinatokana na ukosefu wa huduma kwa sababu ya bajeti
finyu. Ndiyo maana nilifurahi sana kwa chama chetu kuliweka swala la kupunguza
matumizi ya Serikali katika Ilani, na kuondoa posho za wabunge, ambao tayari
wanapokea mishahara mikubwa, kungesaidia sana kupatikana fedha ambazo zingeokoa
vifo vingi vya kina mama.
Jambo hili si suala la ugomvi baina yangu na Mheshimiwa
Lema. Ni suala la msingi katika chama chetu.
3. Usambazaji wa Ripoti ya Siri kuhusu Zitto Kabwe
Hivi karibuni kulisambazwa waraka unaoitwa ripoti ya
siri kuhusu mimi ukibeba lundo la tuhuma kwamba nimehongwa fedha nyingi ili
kukihujumu chama changu. Waraka huu ulidaiwa kuwa umechomolewa kutoka makao
makuu ya CHADEMA. Jambo hili pia lilijadiliwa katika kikao cha juzi kwa kifupi,
na majibu ya viongozi wa chama ilikuwa ni kwamba waraka huu haukuandaliwa wala
kusambazwa na makao makuu. Katika mchango wangu nililalamikia mambo matatu
yafuatayo:
Kwamba baadhi ya waliokuwa wanasambaza waraka ule
walikuwa ni viongozi wa chama chetu. Bahati mbaya hadi leo hakuna hata mmoja
ambaye amekwishachukuliwa hatua za kinidhamu. Ninaamini kwamba kuna siku watu
hao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za chama chetu.
Kwa kuwa chama kimekana rasmi kuhusika na waraka huu,
nitaendelea na taratibu za kisheria ili kuhakikisha kwamba wote waliohusika
kutengeneza hekaya ile wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.
4. Hitimisho
Ninatambua kwamba kuna watu walitegemea leo ningejibu
mapigo na ningewazodoa watu kwa majina kama ilivyo kawaida katika siasa za
Tanzania. Natambua pia kwamba, kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro katika
vyama vya siasa hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo ningetangaza 'maamuzi
magumu'. Natambua kwamba wapo ambao wangependa kupata nafasi ya kuendelea
kutumia suala hili katika harakati zao za kudhoofisha mapambano ya demokrasia
na uthabiti wa siasa za ushindani nchini mwetu. Napenda wanachama wa CHADEMA na
wapenda demokrasia na siasa safi wote nchini watambue kwamba mimi bado ni
mwanachama mwaminifu wa chama hiki na nitakuwa wa mwisho kutoka kwenye chama
hiki kwa hiari yangu. Nitafuata taratibu zote ndani ya chama katika kuhitimisha
jambo hili.
Naomba wanachama waelewe kwamba mimi kama binadamu
ninaumia ninapopigwa. Tuhuma ninazorushiwa ni kubwa na zinanikwaza. Tuache
siasa za uzushi ili tujenge chama chetu na nchi yetu, ili hatimaye tuwakomboe
Watanzania wenye matarajio na imani kubwa kwa chama chetu.
Kama mwanasiasa kijana niliyekaa katika siasa kwa muda
sasa yapo mengi mazuri nimeyafanya. Lakini kuna maeneo nilipojikwaa na yapo
makosa niliyofanya kisiasa katika maisha yangu ya siasa.
Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya
kukuza demokrasia. Ni mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya
wahafidhina, waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa safi
dhidi ya watukuzao siasa majitaka. Hii ni changamoto kubwa ndani ya chama chetu
inayohitaji uongozi shupavu kuikabili. Nitasimama daima upande wa demokrasia.
Kama alivyopata kunena mmoja ya wanasiasa maarufu, 'kiwango cha juu kabisa cha
uzalendo katika nchi ni kukubali kutofautiana kimawazo', na ninatamani huu ndio
uwe utamaduni wa chama chetu.
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Dar es Salaam.
24 Novemba, 2013

0 comments:
Post a Comment