
TAARIFA KWA WATANZANIA JUU YA UAMUZI WA KAMATI KUU YA
CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) KUHUSU KUWAVUA NYADHIFA ZA UONGOZI
NAIBU KATIBU MKUU, MH. ZITTO ZUBERI KABWE NA WENZAKE
Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Kamati Kuu
ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliyokutana Ubungo Plaza, Dar es
Salaam kuanzia asubuhi ya siku ya Jumatano ya tarehe 20 Novemba, 2013 hadi
alfajiri ya leo Ijumaa tarehe 22 Novemba, 2013 imetafakari na kujadili kwa kina
taarifa mbali mbali juu ya hali ya kisiasa ndani na nje ya Chama chetu ambayo
kwa muda mrefu imegubikwa na tuhuma kubwa na nzito dhidi ya Chama chetu na
viongozi wake wakuu, yaani Mwenyekiti wa Taifa, Mheshimiwa Freeman Aikaeli
Mbowe (MB), na Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Peter Slaa. Tuhuma hizi zilikuwa na
malengo na athari ya kuwapaka matope na kuwachafua viongozi wakuu wa Chama na
Chama chenyewe, kutengeneza mtandao wa siri ndani na nje ya Chama ambao
hatimaye ungefanikisha sio tu lengo la kufanya mapinduzi nje ya utaratibu wa
kikatiba wa Chama, bali pia ungekipasua Chama vipande vipande na hivyo kuua
matumaini ya Watanzania juu ya uwezekano wa kufanya mabadiliko ya kisiasa na
kiuchumi na kijamii katika nchi yetu kwa kukiondoa madarakani Chama cha
Mapinduzi (CCM).
Ndugu
Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA, Uchunguzi wa Kamati Kuu umebaini
kuwepo kwa mkakati mkubwa wa kutimiza malengo hayo ambao umeandikwa katika
waraka unaoitwa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013.’ Mkakati huu uliandaliwa na
kikundi kinachojiita ‘Mtandao wa Ushindi’ ambacho vinara wake wakuu ni wanne,
yaani Naibu Katibu Mkuu na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe ambaye kwenye waraka huo anajulikana pia kama
‘MM’ au ‘Mhusika Mkuu’; mjumbe wa Kamati Kuu na mwanazuoni kutoka Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Dk. Kitilla Mkumbo ambaye kwenye waraka anajulikana pia kama
M1; Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha ambaye kwa sasa amesimamishwa uongozi,
Bwana Samson Mwigamba na ambaye kwenye waraka anaitwa M3; na mtu mwingine
ambaye hadi sasa jina lake halijajulikana lakini kwenye waraka anajulikana kama
M2 na anatajwa kuwa yuko ‘ukingoni kupigwa nje’ katika mageuzi ya kiutendaji
yanayoendelea katika Sekretariat ya Chama hapa Makao Makuu.
Kwa mujibu
wa waraka wenyewe, “Mkakati huu umeandaliwa kwa pamoja na M2 na M3 na kupitiwa
na kurekebishwa na M1 ili upelekwe kwa MM kwa maoni ya mwisho na kuanza
utekelezaji.” Mbele ya Kamati Kuu, Dk. Mkumbo alikiri kwamba MM au Mhusika Mkuu
ni Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe; M1 ni yeye mwenyewe Dk. Mkumbo na M3 ni Bwana
Mwigamba. Dk. Mkumbo alikataa kata kata kumfahamu M2. Aidha, Dk. Mkumbo alikiri
mbele ya Kamati Kuu kwamba yote yaliyoandikwa katika ‘Mkakati wa Mabadiliko
2013’ yametoka kwenye ‘Mtandao wa Ushindi’ na hayajabadilishwa.
Ndugu
Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA, Mkakati wa Mabadiliko 2013 ni
mpango wa kuipasua pasua CHADEMA na kuiangamiza kabisa kwenye uso wa siasa za
Tanzania. Huu sio mkakati wa kufanya mabadiliko ya kiuongozi ndani ya Chama kwa
njia za kidemokrasia na za kikatiba. Ni mpango wa kukiteka nyara Chama na
kukiua. Ndio maana watunzi wa waraka huu wamesema kwenye waraka wao:
“Tunahitaji kutekeleza mkakati huu kwa siri kubwa ili mkuu aliyepo aendelee
kubweteka na ndio maana hata lugha iliyotumika ndani hapa ni ya pekee.” Kamati
Kuu inaamini mkakati wenye malengo halali ya kufanya mabadiliko ndani ya Chama
kwa njia halali za kikatiba usingependekeza kwamba:
“Vikao vyetu na yeye (MM aka Mhusika Mkuu aka Naibu
Katibu Mkuu Zitto Kabwe) vitafanyika mara chache sana na mahali pa faragha
kupita kiasi ikiwezekana hata nchi jirani.” Aidha, Kamati Kuu inaamini kwamba
kama mkakati huu ungekuwa na malengo mazuri ya kukijenga Chama na sio kukiteka
nyara na kukiua, wanamtandao hawa wasingependekeza utaratibu ufuatao wa
utekelezaji wa mpango: “M1 (Dk. Mkumbo) ndiye atakayekuwa anawasiliana na
tunayemtaka ambaye ataitwa MM (Mhusika Mkuu).
Tumepanga kwamba kusiwe na mawasiliano mengi kati ya
kamati na mhusika mkuu kuepuka tracking ya wapinzani wetu. M1 ni mtu wa karibu
na MM kwa hiyo mawasiliano yao hayataweza kutiliwa shaka na mtu yeyote hata
wangewasiliana mara nyingi kiasi gani. Hata hivyo, linapokuja suala la mkakati
huu tunasihi mawasiliano yawe kwa kuonana uso kwa uso ama kwa simu na si sms.
M1 ndiye atakayewasilisha mambo yote yanayotoka kwenye kamati ya kitaifa na
endapo kuna haja ya MM kukutana na kamati ya kitaifa, mipango yote ya kikao
itafanywa na M1 kwa usiri mkubwa.”
Ndugu
Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA, Mkakati wa Mabadiliko 2013 ni
mpango haramu na ambao unaichana chana Katiba ya Chama chetu. Ni mkakati wa
vita dhidi ya Chama chetu na utaratibu wetu wa kikatiba. Wakati ibara ya
10.1(iv) ya Kanuni za Uendeshaji Kazi za Chama ambazo ni sehemu ya Katiba ya
Chama chetu ya mwaka 2006 inamkataza kiongozi wa CHADEMA asijihusishe na
vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini, au ukanda ambavyo vina makusudi ya
kubaguana ndani ya Chama na miongoni mwa jamii kisiasa au kijamii”, wanaMtandao
wa Ushindi wameonyesha wazi kuwa wanaendekeza siasa za udini kwa kusema
yafuatayo juu ya waliemwita ‘mtu tunayemtaka’, yaani Naibu Katibu Mkuu Zitto
Kabwe: “Kwa kuwa ni Mwislamu, hii ni fursa katika kupata kuungwa mkono na
wanachama waislamu ambao wamekuwa na kigugumizi wakidhani waislamu hawatakiwi
katika uongozi wa taasisi yetu.”
Wakati
ibara ya 10.1(viii) ya Kanuni za Uendeshaji inamtaka kila kiongozi wa CHADEMA
“... kuwa mkweli na muwazi wakati wote ... na aachane na vikundi vya majungu na
wadanganyifu (rumour mongers) ...”, wanaMtandao wa Ushindi wameeleza kwenye
waraka wao kwamba mipango yao ya utekelezaji wa Mkakati wa Mabadiliko 2013
‘itafanyika kwa usiri mkubwa.’ Wakati ibara ya 10.1(ix) ya Kanuni za Uendeshaji
Kazi za Chama inamtaka “kiongozi asijihusishe na vikundi na vitendo vya
kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa chama au wanachama wake”,
wanaMtandao wa Ushindi wamesambaza tuhuma za uongo dhidi ya Mwenyekiti wa Chama
Taifa (ambaye wanamwita kwenye waraka wao kuwa ni ‘Mpinzani wetu’) kuwa “...
hana mahusiano mema na mazuri na viongozi wa ngazi za chini kutokana na dharau
nyingi anazozionyesha pale anapokutana na viongozi wa ngazi za chini akiwa
katika kuijenga taasisi hii.... Hii imemfanya kutopendwa na viongozi wengi wa
ngazi za chini hivi sasa na kutoa fursa ya pekee kwa tunayemtaka.”
Wakati
ibara ya 10.1(x) ya Kanuni za Uendeshaji inamtaka “kiongozi asitoe tuhuma
zozote juu ya viongozi wenzake pasipo kupitia vikao halali na kuzingatia
taratibu na ngazi zilizowekwa kwenye Kanuni”, tuhuma zote zilizotolewa na
wanaMtandao hawa dhidi ya viongozi wakuu wa Chama chetu hazijawahi kutolewa na
yeyote kati ya wanaMtandao hawa katika kikao chochote halali cha Chama cha
ngazi yoyote.
Wakati
ibara ya 10.1(xii) ya Kanuni za Uendeshaji inaeleza kwamba “itakuwa marufuku
kwa kiongozi wa CHADEMA kukashifu Chama, kiongozi au mwanachama yeyote wa Chama
...”, Mkakati wa Mabadiliko 2013 umejaa kashfa kubwa, matusi mengi na
udhalilishaji mkubwa wa Chama, viongozi wake wakuu na wanachama kwa ujumla.
Hivyo, kwa mfano, Mwenyekiti wa Chama Taifa ametuhumiwa na wanaMtandao hawa
kuwa ni mtu mwenye ‘uzalendo unaotia shaka’, mwenye ‘elimu ya magumashi’,
‘mzito kujieleza’, ‘mtu mwenye akili ndogo’, n.k.
Ndugu
wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA, Hakuna chama au taasisi yoyote
duniani inayoweza kunyamazia mkakati wa aina hii dhidi yake na viongozi wake
wakuu na ikadumu au kubaki salama. Chama au taasisi yoyote inayoendekeza
vitendo vya aina hii miongoni mwa viongozi wake wa ngazi yoyote au miongoni mwa
wanachama wake wa kawaida inakaribisha kifo na mauti. Chama chetu na viongozi
wake wa juu wamekaa kimya kwa muda mrefu sana; wamevumilia mashambulizi na
kashfa nyingi sana dhidi yao binafsi na dhidi ya Chama; wamestahimili matusi
makubwa sana dhidi yao. Chama chetu kimevumilia yote haya na viongozi wake
wamevumilia yote haya sio kwa sababu walitaka Chama chetu kiuwawe na
wanaMtandao hawa. Uvumilivu wote huu ulitokana na haja ya kuwapa wanaMtandao wa
Ushindi fursa ya kugundua hatari ya siasa zao na kuwapa muda wa kujirekebisha
na kujirudi.
Kama
ilivyo kwa binadamu au taasisi yoyote ile, uvumilivu wa Chama chetu na viongozi
wake wakuu una kikomo. Na hiki ndio kikomo cha uvumilivu wa Chama chetu,
viongozi wake na wanachama wake kama wanavyowakilishwa na Kamati Kuu ya Chama
chetu. Hivyo basi, katika kikao chake tajwa, Kamati Kuu ya Chama chetu, kwa
kutumia mamlaka yake ya kikatiba ya dharura chini ya ibara ya 6.5.2(d) ya
Katiba ya Chama, imeazimia yafuatayo kuhusu Mkakati wa Mabadiliko 2013 na hao
wanaojiita wanaMtandao wa Ushindi:
Kwamba, kuanzia sasa, viongozi wote
waliohusika ama kuhusishwa na mkakati huu, yaani Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe,
Mjumbe wa Kamati Kuu Dk. Kitilla Mkumbo na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha Samson
Mwigamba wavuliwe nyadhifa zao zote za uongozi ndani ya Chama; Kwamba timu
ndogo ya pamoja ya watendaji wa Sekretariat ya Makao Makuu ya Chama na wajumbe
wa Kamati Kuu ifanye uchunguzi wa haraka ili kumtambua mtu anayeitwa M2 na
ambaye anadaiwa kuwa mtumishi wa Makao Makuu ya Chama ili hatua stahiki na za
haraka zichukuliwe dhidi yake, pamoja na watu wengine wote watakaobainika
kuhusika na mpango huu wa uhaini dhidi ya Chama chetu; Kwamba Kamati ya Chama
ya Wabunge inaelekezwa kuchukua hatua za haraka za kuhakikisha Naibu Katibu
Mkuu Zitto Kabwe anavuliwa madaraka yake yote kama Naibu Kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, with immediate effect;
Kwamba
viongozi waliotajwa katika aya ya (a) waandikiwe hati zenye tuhuma dhidi yao
haraka iwezekanavyo na watakiwe kujieleza kwa nini wasifukuzwe kwenye Chama kwa
vitendo vyao na wapatiwe fursa kamili ya kujitetea kama inavyotakiwa na ibara
ya 6.5.2(a), (b) na (c) ya Katiba ya Chama; Kwamba mara baada ya utekelezaji wa
azimio (d), Kamati Kuu ikutane kwa dharura kwa ajili ya kufanya uamuzi juu ya
hatma ya watuhumiwa na hatua nyingine zitakazofuata; Kwamba waraka wa
wanaojiita wanaMtandao wa Ushindi uwekwe hadharani na usambazwe kwa vyombo vya
habari vya aina zote ili wananchi wa Tanzania, wanachama na viongozi wa Chama
chetu na dunia nzima kwa ujumla iweze kupima uzito wa Mkakati wa Mabadiliko
2013 na uhalali wa maamuzi haya ya Kamati Kuu.
Ndugu
wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA, Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe na
Mjumbe wa Kamati Kuu Dk. Kitilla Mkumbo waliiomba Kamati Kuu iwaruhusu
kujiuzulu nyadhifa zao baada ya Mkakati wao wa kukiteka nyara Chama na
kukiangamiza kujulikana mbele ya Kamati Kuu. Kwa kuzingatia uzito wa makosa
waliyokifanyia Chama, viongozi wake wakuu na wanachama wake kwa ujumla; na kwa
kuzingatia uzito na umuhimu wa nyadhifa kubwa walizo nazo ndani ya Chama; na
kwa kuzingatia uelewa wao wa Katiba, Kanuni na taratibu za Chama na uzoefu wao
katika safu za juu za uongozi wa Chama, Kamati Kuu ilikataa kwa kauli moja
kuridhia maombi hayo ya kujiuzulu. Kufanya hivyo ingekuwa ni sawa na kuwaruhusu
wajiondoe kwenye uongozi wa Chama wakiwa na heshima wasizostahili hata kidogo.
Chama
chetu ni tumaini pekee la Watanzania wote wanaotaka mabadiliko ya kweli na ya
kimsingi katika mfumo wa kiutawala, kiuchumi na kijamii wa nchi yetu. Hii ndiyo
sababu kubwa na ya pekee iliyosababisha vita kubwa na chafu inayopigwa dhidi ya
Chama chetu na viongozi wetu wakuu. Lengo kuu ni kuwachafua viongozi wakuu,
kuleta mgogoro na mgawanyiko ndani ya wanachama, viongozi wake na hivyo
kukichafua Chama mbele ya macho ya Watanzania. Chama chetu kikishachafuka kwa
mtindo huu, matumaini ya Watanzania wanaotaka mabadiliko yatakufa. Vita hii
kubwa haijaanza jana, na haitaisha kesho. Kama ambavyo tumekabiliana nayo na
kuishinda siku za nyuma, vivyo hivyo tutakabiliana nayo mara hii na kuishinda.
Kama Chama chetu kilivyoibuka na nguvu na heshima kubwa zaidi katika mapambano
ya siku za nyuma, vivyo hivyo Chama chetu kitaibuka na nguvu na heshima kubwa
zaidi katika awamu hii ya mapambano.
Tunawaomba Watanzania, wanachama na viongozi wetu wasife moyo, bali
waendelee kukiunga mkono chama chao cha ukombozi. Tunawaomba Watanzania,
wanachama na viongozi wetu waendelee kulilinda tumaini lao pekee la mabadiliko
ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Badala ya kukatishwa tama,
kila mmoja wetu aongeze bidii maradufu ili kuwashinda wale wanaotaka kuleta
majanga katika Chama chetu na kwa Taifa letu.
------------------------------------------
FREEMAN AIKAELI MBOWE (MB) - MWENYEKITI, TAIFA
------------------------------------------
WILBROD PETER SLAA - KATIBU MKUU
0 comments:
Post a Comment