![]() |
Maofisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa ofisa mwenzao, Luteni Rajab Mlima ulipofikishwa nyumbani kwa marehemu Mbezi Beach, Dar es Salaam jana. |
SIKU chache baada ya kutokea kwa kifo cha mwanajeshi wa
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Rajabu Mlima, aliyekuwa katika
operesheni ya kulinda amani Mashariki mwa Kongo (DRC), serikali imesema
haitatetereka wala kurudi nyuma kwa kurudisha majeshi yake nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa kuaga
mwili wa marehemu Mlima katika viwanja vya jeshi Lugalo, Waziri wa Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, alisema serikali itaendelea kutoa
ushirikiano kwa wanajeshi waliobakia nchini humo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji
wa kulinda amani ya wananchi wa Kongo.
“Kama serikali tunasikitika kwa kifo cha mwanajeshi
wetu, lakini hili halitufanyi kushindwa kuendelea kulinda raia wa Kongo na bado
tunaendelea kutoa hamasa kubwa kwa wanajeshi waliobaki waendelee na majukumu
yao kama kawaida.
“Kikubwa tutaendelea kutoa ushirikiano kwa familia ya
marehemu kwa kuhakikisha shughuli zote za mazishi zinaenda sawa pamoja na kuwa
nao karibu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi,” alisema Nahodha.
Awali akisoma salamu za rambirambi kwa niaba ya Mkuu wa
Majeshi Nchini (CDF), Davis Mwamunyange, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi,
Luteni Jenerali, Samuel Ndomba, alisema marehemu Mlima alipigwa risasi Oktoba
27, saa 5:00 asubuhi, akiwa katika milima ya Cavana iliyoko mashariki mwa Kongo
na kufa papo hapo.
0 comments:
Post a Comment