TAARIFA KWA UMMA
KUKOMA KUWA KIONGOZI KWA MWENYEKITI WA WILAYA
YA MONDULI MCHUNGAJI AMANI SILANGA MOLLEL
Kwa niaba ya baraza la uongozi la mkoa wa Arusha, napenda
kuujulisha umma wote kwa ujumla kuwa mwenyekiti wa wilaya ya monduli Mchungaji
Amani Silanga Mollel amekoma/amesimamishwa kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya
monduli kuanzia tarehe 29 Novemba 2013 kufuatia tuhuma nzito za uvunjifu wa
kanuni za maadili ya chama.
Hatua hii imefikiwa baada ya kuthibitika na yeyé mwenyewe
kukiri mbele ya kikao cha kamati tendaji ya wilaya ya monduli kilichoketi
tarehe 29 Novemba 2913 saa NNE asubuhi kuwa alitoa tamko batili akitumia
wadhifa wa mwenyekiti wa wilaya bila ridhaa ya kamati tendaji na huku
akidanganya kuwa ni tamko kwa niaba ya wilaya ya Monduli.
Katika tamko lake ametoa tuhuma dhidi ya wajumbe wa kamati
kuu na viongozi wakuu wa kitaifa kwa maamuzi halali ya kikao cha kamati kuu
huku akijua kuwa anavunja kanuni za chama kwa mujibu wa katiba ya chama toleo
la mwaka 2006 ya Kanuni za uendeshaji kazi za chama, sura ya KUMI, ibara ya 10
(X) “Kiongozi asitoe tuhuma zozote juu ya viongozi wenzake pasipo
kupitia vikao halali na kuzingatia taratibu na ngazi zilizoelezwa kwenye kanuni
za chama”.
Sambamba na hilo, Mchungaji Amani Silanga ametoa tuhuma za
uzushi, uongo na upotoshaji na kutaka kuaminisha jamii kuwa chadema ina makundi
ya CHADEMA Asili na CHADEMA Family kitu ambacho ni upotoshaji mkubwa na wa
hatari kwa ustawi na umoja wa chama na kinyume na kanuni za uendeshaji kazi za
chama, sura ya KUMI, ibara ya 10 (VII), “Kiongozi anatakiwa kuwa mkweli
na muwazi wakati wote hususani katika vikao halali na aachane na vikundi vya
majungu, wadanganyifu (Rumour Mongers). Ni mwiko kwa kiongozi kujihusisha na
upotoshaji wa maamuzi wa vikao halali”.
Kamati tendaji ya wilaya ilipomtaka aonyeshe CHADEMA asili
ni kina nani na CHADEMA family ni kina nani alishindwa kutoa maelezo yoyote ya
maana na kufikia hatua ya kutaka kuvuruga kikao kwa kuleta vijana wahuni
wapatao 17 ndani ya kikao ambao wengi walijulikana kuwa sio WANACHADEMA. Katika
utambulisho wake wa majigambo Mchungaji Amani SIlanga kwa kiburi na kejeli
amejitambulisha na kukiri kuwa yeye yupo kambi ya Zito Kabwe na hakuna wa
kumfanya kitu maana ni mjumbe wa baraza kuu la chama. Maneno yake
yalidhihirisha kuwa Mchungaji Amani Silanga anashiriki mpango wa kuunda makundi
yasiyo na tija ndani ya chama na hivyo kuwa kinyume na sura hiyo hiyo ya kumi
ya kanuni za uendeshaji kazi za chama ibara ya 10 (IX), “Kiongozi
asijihusishe au kushiriki na vikundi au vitendo vya kuchonganisha au kuzua
migogoro ndani ya uongozi wa chama au wanachama wake”.
AZIMIO LA BARAZA LA UONGOZI LA MKOA WA
ARUSHA:
Baraza la uongozi la mkoa lililoketi tarehe 29 Novemba
2013, limepokea mapendekezo ya kamati tendaji ya wilaya na kuzingatia hofu
kubwa iliyoainishwa na kamati tendaji kufuatia matendo mengi yanayotia shaka ya
uadilifu na uwezo wa kiuongozi wa Mchungaji Amani Silanga na hivyo baraza la
uongozi la mkoa limeridhia kuwa amevunja kanuni za maadili ya chama sura ya
KUMI ibara ya (VII) hadi (XII) na hivyo kupelekea ukomo wa yeye kuwa Mwenyekiti
wa wilaya kuanzia tarehe 29 Novemba 2013. Baraza la mkoa likiwa mamlaka ya
nidhamu kwa mujibu wa katiba ibara ya 6.3.6 (a) (iv) limemjulisha tuhuma zake
na hatua hii stahiki iliyochukuliwa. Kwa vile Mchungaji Amani Silanga alikiri
kosa hili mbele ya kamati tendaji ya wilaya bila kulijutia au kuomba msamaha,
baraza la mkoa limechukua hatua hii stahiki kwa maslahi ya chama na kuwa
uchunguzi zaidi utafanyika ili kufikia maamuzi makubwa zaidi ya tuhuma nyingi
kwa mujibu wa kanuni za hatua za kinidhamu.
Baraza la uongozi la mkoa wa Arusha, linatoa onyo kwa wote
ambao wapo katika mtandao huu mchafu, ama watoke wenyewe mapema maana
hawatavumiliwa kamwe. Baraza la uongozi wa mkoa liliona kuwa Mchungaji Silanga
amepotoka na hivyo yeyé kuendelea kuwepo ndani ya chama wakati wa uchunguzi wa
tuhuma hizi nzito dhidi yake ni hatari zaidi kwa ustawi wa chama na hivyo
baraza likaridhia kwa kuzingatia tafsiri ya katiba ya chama ibara ya 6.3.4 (c)
wa yeyé kukoma uongozi na hivyo akae nje kwa muda na waliopotoka wenzake.
Amani Golugwa
Katibu wa CHADEMA – Mkoa wa Arusha.
(Kwa niaba ya Baraza la Uongozi la Mkoa wa Arusha)
Tarehe 30 Novemba 2013
Amani Golugwa
Katibu wa CHADEMA – Mkoa wa Arusha.
(Kwa niaba ya Baraza la Uongozi la Mkoa wa Arusha)
Tarehe 30 Novemba 2013

0 comments:
Post a Comment