Kama nilivyosema jana kuwa leo kabla ya saa nane
mchana nitaweka wazi unafiki wa Zitto katika suala la posho , suala ambalo
halihitaji vikao vya Chama kulijadili isipokuwa vyombo vya habari na hususani
mitandao ya kijamii kama yeye anavyofanya na kujaribu kupotosha ukweli na
kutafuta sifa ambazo kimsingi hana.
CHADEMA wakati inaamua kulijadili suala hili la
posho , msingi wake mkuu ulikuwa kama ifuatavyo :
1) CHADEMA iliona na kutambua ubadhirifu unaofanyika
kupitia kivuli cha posho katika Taasisi za Umma na Serikali na sio Bunge pekee
, hivyo CHADEMA ikapendekeza mishahara ipandishwe na posho zisizo za lazima
ziondolewe ili kuondoa mwanya wa ubadhirifu wa fedha za Umma .Huu ndio uliokuwa
msimamo wetu .
Kulikuwa na msingi mkuu ambao ungekuwa na faida
kubwa kwa Nchi na Watu wake lakini kabla msimamo huu haujawekwa hadharani na
kutafsiriwa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni , Zitto Kabwe tayari alishatoka
katika vyombo vya habari ni kujipambanua kuwa yeye hataki posho na wala
hatachukua posho , na hapa vyombo vya habari vilichukua jambo hili kama hoja
yake binafsi na huku mantiki ya hoja kamili ikipotea . ( Mantiki ilikuwa ni
kuondoa posho zisizo za msingi kwa Watumishi wote wa Umma na kuboresha masilahi
yao kwa maana ya mishahara )
Lengo kubwa la Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa
na CHADEMA ni kupigania masilahi bora ya Watumishi wa Umma na Sekta binafsi
katika Nchi hii . Msingi wa CHADEMA ulikuwa na maana pevu kwani tulijua kama
mishahara ikiongezwa itampa fursa Mtumishi kuwa na Maisha bora leo na hata
baadaye kwa mafao bora baada ya utumishi wake kazini . Lakini ingekuwa rahisi
pia kwa Mtumishi kuwa na uwezo mkubwa wa kutafuta mikopo kwa ajili ya maendeleo
kwani Mabenki yanatoa mikopo kupitia mishahara ya Watumishi . Ikumbukwe kwamba
, mtumishi mwenye mshahara mzuri anakuwa na fursa ya kupata mkopo mkubwa ambao
utatatua matatizo yake mengi . Kwa hiyo msingi wa kutaka posho zisizo na msingi
ziondolewe ilikuwa ni mkakati wa CHADEMA kuboresha masilahi ya Umma kupitia
mishahara .
Niliposema Mh Zitto ni mnafiki kuhusu suala hili ,
nilikuwa na maana ifuatavyo :
Kwamba , sio kweli kuwa kukataa posho ni uzalendo na
hata ingekuwa ni uzalendo Zitto sio mzalendo katika suala hili la fedha na
maisha yake . Aliposema hatachukua posho Wananchi wengi walimuona ni shujaa ,
ushujaa ambao hana katika jambo hili . Nasema hivi kwa sababu , Wakati Zitto
anakataa posho ya kikao ya shilingi sabini elfu ( 70,000 /=) kwa siku ambayo ni
sawa na shilingi takribani milioni kumi na mbili kwa vikao vyote vya Bunge kwa
Mwaka , Zitto huyo huyo , anapokea posho ya kikao kati ya shilingi laki saba
hadi milioni moja kwa kikao kimoja katika vikao vinvyofanywa na mashirika mbali
mbali hususani Mashirika ya hifadhi za Jamii . Maana yake ni kwamba kama
anapokea laki saba kwa siku na mashirika haya kwa ujumla wake yakafanya vikao
ishirini tu kwa mwaka na mara nyingi Zitto kama Mwenyekiti wa PAC huwa anapata
mwaliko wa kuhudhuria vikao hivi , basi atakuwa akipata posho ya kikao
takribani ya shilingi milioni kumi na nne mpaka milioni ishirini kwa vikao
visivyozidi ishirini , wakati kule juu amekataa posho ya shilingi milioni
takribani kumi na mbili kwa vikao vya siku takribani mia moja na themanini
ambayo ni miezi sita .
Ikiwa vikao hivyo vya mashirika anayohudhuria Zitto
kama Mwenyekiti wa PAC ni vya siku mia moja themanini kama ilivyo kwa vikao vya
Bunge basi Zitto atakuwa anapokea posho kati ya ya shilingi milioni mia moja na
ishirini na sita elfu na laki sita ( 126,600,000) na milioni mia moja na
themanini ( 180,000,000) . Na hapa naomba kutaja masilahi yangu katika hili
kwani Wabunge wa kawaida ikiwa wakialikwa katika vikao hivyo huwa wanalipwa
shilingi laki tano kwa kikao kwa siku . Mimi nimewahi kuhudhuria vikao hivyo
mara mbili na nikalipwa hivyo pamoja na chai na chakula cha mchana . Tofauti na
Mwenyekiti wa Kamati ya PAC yeye pamoja na posho anayochukua ( 700,000 -
1,000,000) hupewa mafuta ya gari au tiketi ya ndege yamkutoa alipo na
kumrudisha na kukodiwa Hoteli yenye hadhi ya nyota nne mpaka tano ambayo kwa
siku . Hotel hiyo hulipiwa kati ya dola za Marekani mia moja mpaka dola mia
sita kwa siku .
Ø JE MTU HUYU ANAYEPINGA POSHO YA ELFU SABINI YA
KIKAO CHA BUNGE AMBACHO MSINGI WAKE NI UWAKILISHI WA WANANCHI NA KUKUMBATIA
POSHO YA YA SHILINGI LAKI SABA HADI MILIONI MOJA YA MASHIRIKA AMBAYO MSINGI
WAKE PENGINE NI KUWAZIBA MIDOMO WENYEVITI WA KAMATI ZA BUNGE KATIKA MASHIRIKA
HAYO NDIYO UZALENDO ? HUU NI UNAFIKI WAKUTAKA SIFA AMBAZO HAZINA MSINGI.
Lakini huyu Zitto anatoka Jimbo lenye Umasikini
mkubwa ambapo naamini kuwa kuna wahitaji wengi kama yatima , wajane , wazee ,
na wasiojiweza kwa namna mbali mbali , kama yeye ni mzalendo kwa nini
asingetumia malipo yake hayo halali kuwasaidia hao ndugu na Jamaa na Wapiga
kura wake ?
Ø NI NA WASI WASI NA UZALENDO ANAOUHUBIRI ZITTO , NA
AMEPOTEZA MWELEKEO WA HOJA YA MSINGI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI INAYOONGOZWA NA
CHADEMA JUU YA FIKRA SAHIHI YA KUBADILISHA MFUMO WA KIBADHIRIFU ULIOJIFICHA
KWENYE POSHO ZISIZO ZA MSINGI NA KUBORESHA MASILAHI YA WATUMISHI WA UMMA
KUPITIA MISHAHARA YAO.
MSIMAO WANGU
Kwanza najua na ninamini kuwa “ UMASIKINI SIO
UZALENDO “ sipendi umasikini , nachukia umasikini lakini pia sipendi kuona
mafanikio yangu yanabaki kwangu tu huku wengine wakiteseka , lakini siwezi pia
kukumbatia umasikini kwa lengo lakuthibitisha uzalendo wangu .
Najua watu wa Jimbo langu wanataka maji , umeme na
huduma bora za Afya na mambo mengi yenye sura hii lakini sitang’oa bomba la
maji nyumbani kwangu kwa sababu jirani yangu hana maji ila nimtasaidia kwa
kadri nitakavyoweza na yeye aepukane na adha hiyo ya ukosefu wa maji .
Najua shule za Kata hazina ufaulu mzuri na mazingira
yake ni magumu , lakini sitampleka mtoto wangu kwenye shule zisizo na waalimu
ili kuonyesha uzalendo bali nitapigania ubora wa shule hizo kuongezeka ili
Wananchi wote wapate Elimu bora .
Zitto Julai 2012 stahili za Mbunge ziliongezwa kwa
takribani shilingi milioni tatu ambazo ni sawa na milioni thelasini na sita kwa
mwaka , je kwani Zitto hakugoma kupokea pesa hizo ili kuonyesha uzalendo wake ?
Zitto kuna wakati uliumwa ukapelekwa India kutibiwa
, sasa kwani hukuwa mzalendo na kufanya mgomo ili utibiwe hapa Nchini ili
kuonyesha Uzalendo wako ? na kuokoa pesa ya serikali kama ambavyo unaionea
huruma kwenye posho ?
Zitto ningekuelewa , kama maisha unayoishi
yangeendana na kauli zako za Kikomunisti lakini maisha yako na matendo yako na
mienendo yako yanashindwa kutafsiri kauli zako .
MWISHO – MIMI SIAMINI KAMA MSINGI WA UZALENDO NI UMASIKINI
. LAITI INGEKUWA HIVYO MAKUSUDI YA KUANZISHA MFUMO WA VYAMA VINGI ILI
KUWAKOMBOA WATANZANI NA LINDI LA UMASIKINI ULIOSABABISHWA NA CCM YASINGEKUWA NA
HAJA , NAJUA ASILIMIA 80 YA WATANZANIA NI MASIKINI SANA , JE WATANZANIA NI
WAZALENDO KWA TAIFA LAO KULIKO WAMAREKANI ?
Namalizia kwa maneno ya Charles Darwin “ If the
misery of the poor be caused not by the laws of nature, but by our
institutions, great is our sin.”
Godbless J Lema
2/11/2013
0 comments:
Post a Comment