KIWANGO cha ufaulu katika matokeo ya darasa la saba
mwaka huu kimeongezeka, ambapo wanafunzi 427,606, sawa na ongezeko la asilimia
19.89 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari za
serikali.
Hata hivyo licha ya ufaulu kuongezeka, matokeo hayo
yanaonyesha kuwa wanafunzi wengi wamefeli somo la Hisabati na wamefanya vizuri
zaidi katika somo la Kiswahili.
Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam, Kaimu
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani, Dk. Charles Msonde, alisema somo la
Kiswahili liliongoza kwa asilimia 69.06 huku Hisabati likiambulia asilimia
28.62.
Alisema kwa upande wa somo la Kiingereza, lilifanya
vizuri kwa asilimia 35.52, Maarifa ya Jamii asilimia 53.00 na Sayansi asilimia 47.49.
Katika hatua nyingine, wavulana wameng’ara kwa kuongoza
kwa asilimia 55.1 na kuwapita wasichana waliopata asilimia 46.68.
Alisema wanafunzi 427,606 wamechaguliwa kujiunga na
kidato cha kwanza katika shule za sekondari za serikali.
Alisema kati ya wanafunzi hao, wasichana ni 208,227 na
wavulana ni 219,379, hivyo kufanya idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kuongezeka
kwa asilimia 19.89 tofauti na mwaka jana ambapo kiwango kilikuwa asilimia 8.8 .
Dk. Msonde alisema kuwa mtihani huo ulifanyika Septemba
11 na 12 ambapo watahiniwa walitumia karatasi maalumu za ‘optical mark reader’
na kusahihishwa kwa mfumo wa kompyuta.
“Matokeo haya yanaonyesha kuwa jumla ya watahiniwa 9,126
walipata daraja A, wakati wanafunzi 82,293
walipata daraja B.
“Jumla ya wanafunzi 336,187 walipata daraja C, 389,948
daraja D na waliobaki, yaani 27,367
walipata daraja E,” alisema Msonde.
Hata hivyo, Msonde, hakuweza kutaja mikoa iliyofanya
vema na ile iliyoshika nafasi ya mwisho, zikiwamo shule zilizoongoza na kueleza
kuwa baraza limewasilisha matokeo hayo kwenye mamlaka husika.
“Tumewasilisha matokeo kwa mamlaka husika ili zifanye
uchaguzi wa watahiniwa wa kujiunga na elimu ya sekondari na matokeo hayo
yatatangazwa na mamlaka husika mara baada ya kazi ya uchaguzi itakapokamilika,”
alisema.
Akizungumzia udanganyifu katika mtihani, alisema takwimu
zinaonyesha kuwa idadi ya watahiniwa waliofutiwa matokeo kutokana na
kujihusisha na vitendo vya udanganyifu katika mtihani huo imepungua.
Alisema waliofutiwa matokeo mwaka huu ni watahiniwa 13,
ikilinganishwa na watahiniwa 293 waliofutiwa matokeo kwa undanganyifu mwaka
jana.
Kuhusu tatizo la baadhi ya wanafunzi kutojua kusoma na
kuandika, Msonde alisema ni mapema mno kulijua hilo, kwani linahitaji muda.
Wanafunzi 844,983 wa shule za msingi walisajiliwa
kufanya mtihani huo wa kumaliza darasa la saba, wengine 23,045 sawa na asilimia
2.66 hawakufanya kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ya utoro, vifo, ugonjwa
na wasichana kupata mimba.
0 comments:
Post a Comment