![]() |
| Kambi ya wakimbizi wa ndani katika mji mkuu wa Jimbo la Darfur, Nyala |
Na Kabuga Kanyegeri
WATU wapatao mia moja, wakiwemo askari wa Chad, wameuawa
katika mapigano ya kikabila katika jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan.
Radio Omdurman ya nchini humo imeripoti kuwa vifo hivyo
vilitokana na mapigano baina ya makabila ya Misseriya na Salamat, ambayo
yamekuwa na uadui na uhasama kwa miaka mingi, na mwezi huu uhasama umeibua
mapigano makali baina yao.
Kwa mujibu wa kiongozi wa kabila la Misseriya, mapigano kati
ya makundi hayo uliendelea jana karibu na eneo la Umm Dukhun, karibu na mpaka
wa nchi hiyo na nchi ya Chad na kugharimu maisha ya watu 50 kutoka pande mbili.
Aidha, siku hiyo hiyo, chanzo kimoja kilieleza kuwa
askari kadhaa wa Chad waliuawa katika mapigano na kabila la Salamat karibu na
eneo la Umm Dukhun yaliyotokea siku ya Alhamisi.
Ripoti zinasema kuwa tangu Aprili mwaka huu watu wapatao
200 wameshapoteza maisha yao katika mapigano baina ya makabila hayo mawili.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya
kibinadamu (OCHA) inasema kuwa mwaka huu migogoro ya kikabila na uasi
vimesababisha watu wapatao 460,000 kuyahama makazi yao katika jimbo la Darfur.
Mnamo Novemba 13, Waziri wa Ulinzi wa Sudan, Abdulrahim
Mohammed Hussein alisema kuwa ghasia za kikabila katika jimbo la Darfur zimekuwa
hatari kwa usalama wa eneo hilo kuliko hata mapigano ya waasi.
Tarehe 12 Novemba, misheni ya Umoja wa Mataifa katika
jimbo la Darfur, UNAMID, ilielezea “wasiwasi mkubwa” kutokana na ripoti za
ghasia za hivi karibuni baina ya makabila ya Misseriya, Taisha, na Salamat katika
eneo la katikati mwa jimbo la Darfur.
Sudan inaituhumu Sudan Kusini, ilijitoa kutoka Jamhuri
ya Sudan Julai 2011, kuwa inayasaidia makundi yanayoipinga serikali
yanayopatikana Darfur na katika majimbo ya Blue Nile na Kordofan Kusini.
Sudan Kusini ilipata uhuru wake Julai 9, 2011, baada ya
miongo kadhaa ya mapigano baina yake na Sudan Kaskazini.

0 comments:
Post a Comment