
Na Kabuga Kanyegeri
WATU thelathini na nne wamepoteza maisha na wengine
kadhaa kupotea baada ya jimbo la kati nchini Vietnam kukumbwa na mafuriko
makubwa kuwahi kutokea kwa zaidi ya muongo mmoja.
Mvua kubwa iliyotokana na mgandamizo wa kimbunga Haiyan
kilichopiga katika Bahari ya Kusini mwa China kimesababisha mafuriko ambayo
hayajawahi kutokea tangu mwaka 1999.
Mafuriko yaliyodumu kwa siku kadhaa yamezigharikisha
nyumba na barabara katika mji wa Hoi An na jiji la Hue, na kuwalazimisha watu wapatao
80,000 kuuhama mkoa huo.
Zaidi ya nyumba 100,000 zimegharikishwa huku usafiri wa
barabara, anga na reli ukiathiriwa vibaya sana katika jimbo hilo na mvua imeendelea
kunyesha katika wilaya za pwani za Quang Ngai na Binh Dinh – ambapo watu
wapatao 20 (kati ya 34) wamepoteza maisha.
Hasara iliyotokana na mafuriko hayo inakadiriwa kufikia
dola za kimarekani milioni 65.
Maelfu ya watu walihamishwa kabla ya kufika kwa Kimbunga
Haiyan, ambacho kiliiathiri vibaya sana nchi ya Ufilipino, kabla ya kuelekea
Katika Bahari ya Kusini mwa China.
Mamlaka nchini Ufilipino na Umoja wa Mataifa zimetoa
idadi ya vifo inayotofautiana, vinavyokadiriwa kufukia zaidi ya watu 3,600. Idadi
ya makadirio ya majeruhi ni 12,487, huku watu 1,187 wakiripotiwa rasmi kuwa
wamepotea.
Matukio hayo mapya yanakuja baada ya mvua za msimu
zilizosababishwa na Kimbunga Usagi kuyapiga maeneo kadhaa ya nchi za Vietnam na
Cambodia mapema mwezi jana na kugharimu maisha ya watu 40.
0 comments:
Post a Comment