
Hali ya wasiwasi iligubika eneo kinapofanyika kikao cha Kamati Kuu ya Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilichoanza Dar es Salaam jana.
Ulinzi mkali wa walinzi wa Chadema (Blue Guard),
uliimarishwa katika ukumbi wa Ubungo Plaza kinapofanyika kikao hicho ambacho
kinatarajiwa kumalizika leo, huku kukiwa na maagizo yaliyoashiria kuwapo kwa
mambo mazito.
Maazimio ya kikao hicho yanasubiriwa kwa hamu na
wafuatiliaji wa mambo ya siasa nchini kwani kinafanyika katika kipindi ambacho
chama hicho kikuu cha upinzani nchini kinapita katika misukosuko na hasa ya
malumbano baina ya makamanda wake wa juu.
MAELEKEZO YA ULINZI
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwasili ukumbini
hapo saa 5.20 asubuhi na baada ya kuingia, wapiga picha waliruhusiwa kuingia
kuchukua kumbukumbu ya tukio hilo kwa dakika moja tu.
Waandishi wa habari hawakutakiwa kuingia na badala yake
walielezwa kuwa wangepewa taarifa baadaye.
Wakati wapiga picha wakiwa ndani, mmoja wa wajumbe wa
mkutano huo alitoka na kutoa maelekezo kwa walinzi wa Chadema akiwataka kuwa
makini kutekeleza kazi yao watakapopewa amri ya kumwondoa mjumbe yeyote
mkutanoni.
“Kama mkipewa amri ya kuondoa mtu ingieni na mtekeleze
amri hiyo mara moja,” alisisitiza mjumbe huyo na kuingia ndani haraka. Walinzi
hao zaidi ya 10, walipokea maelekezo hayo kwa kutikisa kichwa kuashiria
kukubaliana na amri hiyo.
KIKAO KUFUNGULIWA
Kikao hicho ambacho kilifunguliwa dakika nane baada ya
Mbowe kuwasili, kilipangwa kujadili mambo matatu jana.
Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo ambaye hakutaka kutajwa
jina lake alisema kingepitia taarifa za vikao viwili vya Kamati Kuu
vilivyopita.
Suala jingine ambalo lilipangwa kujadiliwa jana ni
ushiriki wa Chadema katika uchaguzi mdogo wa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi
Jimbo la Kiembesamaki, Zanzibar na kupitia taarifa ya fedha.
LEO MOTO
Ajenda zinazotarajiwa kujadiliwa leo ni pamoja na ripoti
ya utekelezaji wa Kampeni ya ‘Movement For Change’ (M4C) na hali ya siasa.
Ajenda hiyo inatazamiwa kugusa matukio ya hivi karibuni
ndani ya chama hicho. Hayo ni pamoja na malumbano kati ya Naibu Katibu Mkuu,
Zitto Kabwe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuhusiana na masuala ya
posho, kusimamishwa kwa Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Arusha, Samson
Mwigamba, kuvunjwa kwa uongozi wa Mkoa wa Mara na pia kuondolewa kikaoni kwa
Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda.
Zitto na Lema waliingia katika vita ya maneno mwanzoni
mwa Novemba kuhusiana na masuala ya posho ya vikao.
Vita hiyo ilianzishwa na Lema katika kikao cha wabunge
wiki iliyopita aliposema kuwa Zitto anafanya unafiki kukataa posho.
Lema alimtuhumu Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kwamba
anakataa posho za vikao bungeni, lakini anapokea posho nyingi kutoka mashirika
mbalimbali ya kijamii nchini.
Lema aliweka tuhuma hizo kwenye Mtandao wa Jamii Forum
huku akisema suala hilo halihitaji vikao vya chama kulijadili isipokuwa vyombo
vya habari na hususan, mitandao ya kijamii kwani hata Zitto hutumia mitandao
hiyo.
Akijibu hoja hizo, Zitto alisema tangu siku nyingi
alikwishapiga marufuku kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
kupokea posho kutoka taasisi au mashirika yanayosimamiwa na kamati hiyo.
Alisema tangu alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), alipiga marufuku posho na pia aliwahi
kuwashtaki Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) wabunge wanaochukua
posho kutoka taasisi za Serikali.
Zitto pia alipata msukosuko mwingine baada ya kusambazwa
ripoti inayoitwa ‘Taarifa ya Siri ya Chadema’ iliyomtuhumu kuwa alikuwa
anashirikiana na CCM na viongozi wa Idara ya Usalama wa Taifa kuhujumu chama
hicho.
Ripoti hiyo inayodaiwa kuwa iliandaliwa na Idara ya
Upelelezi ya Chadema, ilieleza kuwa Zitto alikuwa akipokea fedha kutoka kwa
maofisa wa usalama na kuzisambaza kwa makada wengine wa chama hicho ili wafanye
kazi ya kukihujumu. Hata hivyo, Chadema kupitia kwa Mnyika ilitoa taarifa
kupinga vikali suala hilo.
CAG KUKAGUA RUZUKU
Pia, Zitto aliingia katika malumbano na chama chake
baada ya kutuhumu vyama vya siasa kuwa hesabu zake hazikaguliwi na CAG. Chadema
ilipinga vikali madai hayo na kueleza kuwa imekuwa inatumia taasisi binafsi
kufanya kazi hiyo.
Suala jingine linalotazamiwa kujadiliwa katika kikao
hicho ni kusimamishwa kwa Mwigamba na Baraza la Uongozi Kanda ya Kaskazini
ambako kulizuka vurugu kiasi cha kunyang’anywa kompyuta mpakato (laptop) baada
ya kudaiwa alikuwa anasambaza taarifa za kuhujumu chama hicho.
Suala lake linasubiri uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu
kama lile la kuvunjwa kwa uongozi wa Chadema wa Mara.
Pia kitendo cha Baraza la Kanda ya Ziwa Mashariki
kumtimua Shibuda kwa madai kwamba halina imani naye nacho kina uwezekano mkubwa
wa kujadiliwa.
ZITTO NA MNYIKA WAKOSEKANA
Zitto na Mkurugenzi wa Uenezi wa chama hicho, John Mnyika walikuwa miongoni mwa wajumbe
walioshindwa kuhudhuria jana.
Zitto yuko na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC) huko Sudan Kusini na Mnyika pia yuko katika ziara ya kibunge
Uturuki.
Kikao cha jana kilihudhuriwa na wajumbe 23 kati ya 32.
CHANZO: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment