Na Kabuga Kanyegeri
WAKATI Waturuki wakiadhimisha miaka 90 ya kuasisiwa kwa
Jamhuri ya Uturuki, leo taifa hilo limefungua reli ya kwanza duniani ianyopita
chini ya bahari na kuyaunganisha mabara mawili ya Asia na Ulaya. Mradi huo
unaojulikana kama Marmaray ni utekelezaji wa ndoto ya viongozi wa Kiuthmaniya
waliyokuwa nayo zaidi ya karne moja iliyopita.
Sherehe ya uzinduzi ilihudhuriwa na viongozi wa Uturuki
na wa kigeni ikiwa ni pamoja na Rais wa Uturuki, Abdullah Gül; Spika wa Bunge Cemil
Çiçek; Waziri Mkuu Recep Teyyip Erdoğan; huku wale wa kutoka nje wakiwa ni
pamoja na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, Waziri Mkuu wa Japan Shinzo
Abe, Rais wa Romania Victor Ponta na
wengine wengi.
Marmaray, ambayo ndio njia ya kwanza ya chini ya bahari
duniani kuyaunganisha mabara mawili, itakuwa na masafa ya kilometa 76.3 na itabeba
abiria 75,000 kwa saa na karibu wasafiri milioni 1 kwa siku.
Wakati wa uzinduzi huo, Rais wa Uturuki, Abdullah Gul
aliuelezea mradi huo kuwa ni mradi unaoziunganisha Beijing na London, na
kuongeza kuwa mazingira ya uthabiti na kujiamini yameifanya Uturuki kutekeleza
mradi huu wa aina yake.

Naye Waziri Mkuu, Recep Teyyep Erdoğan alisema kuwa Marmaray
sio tu mradi unaounganisha mabara, bali pia unawaunganisha watu.
“Ni utekelezaji wa ndoto ya miaka 150. Unatuunganisha na
wahenga wetu…sio tu unayaunganisha mabara, bali pia unawaunganisha watu na nchi
mbalimbali. Marmaray sio tu mradi wa İstanbul bali ni mradi wa binadamu wote,”
alisema Erdoğan.
Mipango ya njia ya reli inayopita chini ya bahari ni
mipango iliyoanza muda mrefu kuanzia mwaka 1891, pale kiongozi wa dola ya
Uthmaniya Sultan Abdülhamid, ambaye alikuwa mlezi wa huduma za ujenzi na ustawi
wa jamii anayehusudiwa na Erdoğan mwenyewe, alipowaita wahandisi wa Kifaransa
kuandaa mradi huo ambao hakuufanikisha.

0 comments:
Post a Comment