NA EDO KUMWEMBE
NCHI inaliwa usiku na mchana. Unajua kwanini? Achilia
mbali tamaa binafsi zilizojaa katika mioyo yetu, lakini asilimia kubwa ya
Watanzania hatuitazami nchi yetu katika jicho la uzalendo.
Huyu anashirikiana na mzungu kuingia mkataba duni wa
Madini, yule anashirikiana na mgeni kuingia porini kuua Tembo na kutoweka na
meno yao. Matokeo yake barabara nzuri za Lami zinajengwa Ulaya, vijijini kwetu
tunaachiwa mashimo.
Kwetu sisi, mtu akipata kazi TRA tunamwambia ‘Kazi
kwako, ushindwe mwenyewe kujenga sasa’. Hii ndio Tanzania kadri niijuavyo. Mtu
hana habari kwamba huyo mtu anayemshawishi kujenga ndiye mwenye mamlaka ya
kusimamia kodi zetu.
Uzalendo ni neno gumu kwa Mtanzania. Hata katika michezo
ni hivyo hivyo. Mwaka 2006, mgeni mmoja alisafiri kilomita 8945 kutoka Rio de
Janiero mpaka Dar es salaam kwa ajili ya kuwafundisha Watanzania jinsi ya
kuipenda timu yao ya taifa.
Ni Marcio Maximo. Mbrazil huyu alisafiri kutoka kwao
kuja kutuelekeza jinsi ya kuvaa jezi za Taifa Stars, jinsi ya kuvaa skafu,
jinsi ya kushangilia wachezaji wetu uwanjani. Aibu iliyoje! Mpaka leo
Watanzania wanakiri hili hadharani. Kwanini tulishindwa kulitambua hili kabla
hajafika?
Wakenya wana matatizo yao. Lakini nje ya matatizo yao,
Mkenya akimuona mwenzake, basi anajihisi kama anajitazama mwenyewe. Ni kama
ilivyo kwa Waingereza, Wacongo, Wamarekani, Wanigeria na wengineo.
Wanamuziki wa DR Congo kazi yao kubwa ni kusifia watu
wao. Nyakati Fulani nilikuwa nasikiliza nyimbo zao na muda mwingi walipenda
kumtaja Dikembe Mutombo. Staa wa zamani wa Kikapu wa NBA aliyezaliwa Kinshasa.
Umewahi kumsikia Mwanamuziki wa Tanzania ameimba wimbo
na kumtaja Hasheem Thabeet? Katika ubora wake wa sasa hivi, umewahi kufikiria
Diamond Platinum anamtaja Hasheem katika wimbo wake walau mmoja?
Lakini pia umewahi kufikiria katika mahojiano yoyote
ambayo Hasheem anaweza kufanya na CNN au kituo chochote cha Televisheni duniani
anaweza kusema anavutiwa na nyimbo za Diamond au Juma Nature ambaye alikuwa
akimpenda sana wakati yupo shuleni Makongo? Hapana.
Sehemu ya ndani ya mioyo yetu haitutumi kujipenda. Inatutuma
kuwapenda zaidi wengine. Kama Hasheem Thabeet angekuwa Mkenya, Watanzania
tungemfuatilia kwa umakini zaidi.
Na ndio maana kwa kufuta ujinga huu, nilianza kwenda
Lubumbashi kwanza kueleza jinsi Mbwana Samatta anavyoishi kifahari nchini humo,
kabla ya kwenda Italia kueleza jinsi McDonald Mariga anavyoishi. Tanzania
kwanza, Afrika Mashariki na dunia baadae!
Mara kadhaa katika mahojiano yake na vyombo vya habari,
Obi Mikel huwa anasema anavutiwa na wanamuziki ndugu wa kundi la P Square. Na
wanamuziki hawa wakihojiwa kuhusu wanasoka wanaowapenda huwa wanaanza na Obi
Mikel. Wote ni Wanigeria hawa. Kwao, maisha yanaanzia nyumbani!
Carlos Tevez akifunga bao huwa anaonyesha fulana yake ya
ndani iliyoandikwa jina la Fuerte Apache. Hiki ndio kitongoji alichotoka pale
Buenos Aires, Argentina. Lakini umewahi kufikiria kwamba siku moja Samatta
atavua jezi yake na kutuonyesha fulana iliyoandikwa Mbagala, eneo alillokulia?
Hawezi kufanya hivi. Hajafundishwa uzalendo. Na wakati
mwingine unajiuliza, kwanini umlaumu wakati hata nyumbani kwake pale Lubumbashi
sebuleni hakuna bendera ya Tanzania? Watu wanaochota pesa Serikalini kwa madai
ya kuitangaza Tanzania wamewahi kuwasiliana naye?
Majuzi kulikuwa na picha imeenea katika mitando
mbalimbali ya kijamii ikimuonyesha Robin van Persie na Hasheem Thabeet wakiwa
wamepiga picha jijini London. Ni Van Persie mwenyewe ndiye aliyekuwa ameituma
picha hiyo katika mitandao.
Cha ajabu, kuna baadhi ya Watanzania walianza kuhisi
kwamba picha hiyo ilikuwa imetengenezwa tu kiubunifu na watu wa mitandaoni.
Aibu iliyoje! Kuna ajabu gani mwanasoka nyota wa Ligi Kuu ya England akapiga
picha na mchezaji kikapu wa NBA. Au kwa sababu mcheza kikapu huyo ni Mtanzania?
Kujidharau kulikopitiliza.
Wakati Francis Cheka alipompiga bondia wa Marekani, Phill
Williams Agosti mwaka huu, mashabiki wakaanza kukejeli kwamba Cheka alikuwa
amempiga Kinyozi tu kutoka Marekani. Ni kweli kwamba Williams anamiliki Saluni
nchini Marekani. Lakini si hata Cheka anaokota chupa za maji pale Morogoro?
Wote ni mabondia wa kulipwa lakini wana shughuli zao nje ya ulingo wa ngumi.
Hata hivyo kwa sababu Cheka alishinda, tukatafuta sababu
kuwa Williams ni kinyozi. Lakini Cheka angedundwa tungemkejeli tu kuwa hajui
ngumi. Ndivyo tulivyo Watanzania. Mgeni kwanza, mwenyeji baadae.
Pambano la Flyod Mayweather na Canelo Alvarez wa Mexico
lilijaza marafiki kibao wa Mayweather ambao ni mastaa kama vile Puff Daddy, Lil
Wayne, Denzel Washington na wengineo. Hapo ilikuwa Marekani kwanza. Sisi hapa
Cheka akishinda tunanuna.
Matokeo yake nchi inaliwa taratibu na sasa ni kama vile
tumechelewa. Kila mtu anaishia kujitazama yeye. Hakuna anayeitazama nchi kama
nchi. Uzalendo wetu uko chini sana wakati kwa wenzetu uzalendo ni sawa na ngozi
na mfupa.
Karibu kila kitu kilichokwama hapa nchini, tatizo lake
kubwa la msingi ni uzalendo. Mengine yote yanakuja baadae. Hatuipendi nchi
yetu. Hatuna ufahari nayo. Hatujikubali. Hatujielewi. Hatuna uzalendo. Nani
anabisha?

0 comments:
Post a Comment