
GENGE la wanaume watatu nchini India limembaka binti wa
miaka 13 na kisha kumuua kwa kumchoma moto katika muendelezo wa matukio ya
ubakaji na mauaji katika nchi hiyo ya Kusini mwa bara la Asia.
Jana Jumatano, vyombo vya habari nchini India viliripoti
kuwa tukio hilo lilitokea siku ya Jumanne katika Wilaya ya Sirsa Kalaar katika
mji wa Orai katika jimbo la kaskazini la
Uttar Pradesh.
Wanaume hao walimshambulia binti huyo wakati akienda shamba
pamoja na dada yake mkubwa.
Baba wa binti huyo anasema kuwa mabinti hao “walipowaambia
wabakaji kuwa wataripoti tukio hilo katika kituo cha polisi, walimchoma moto na
kukimbia.”
Kwa mujibu wa ripoti hizo, dada wa binti huyo alikimbia
kwenda kuomba msaada, lakini aliporejea alimkuta mdogo wake akiugulia maumivu
yaliyotokana na moto uliotishia kuyakatisha maisha yake.
Alipoteza maisha akiwa hospitali baada ya asilimia 80 ya
mwili wake kuungua vibaya sana, liliripoti gazeti la Times of India la nchini
humo.
Kwa sasa Polisi wanamtafuta mwanaume aliyetambuliwa kwa
jina la Ram Bahadur na washukiwa wengine wawili wa tukio hilo la kinyama.
Visa vya ubakaji na vifo vinavyotokana na matukio hayo
vinaonekana sio tu kuongezeka nchini India bali pia vimeongeza hasira na
ghadhabu ya umma.
Mwaka 2012, mwanafuzi wa masomo ya udaktari mwenye umri
wa miaka 23 alibakwa na kundi la wanaume sita ndani ya basi katika mji wa New
Delhi. Baadaye alifariki dunia kutokana na majeraha ya ndani akiwa hospitali.
Tukio hilo liliamsha maandamano ya umma yaliyotikisa nchi
nzima yakitaka kuwekwa kwa sheria kali dhidi ya wahalifu wa vitendo vya
ubakaji.
0 comments:
Post a Comment