KILA mwaka, madini aina ya Tanzanite huiingizia Tanzania
kiasi cha dola milioni 20 (zaidi ya Sh bilioni 30). Duniani kote, madini hayo
hayo huingiza wastani wa dola milioni
500 (zaidi ya Sh bilioni 800).
Wakati mabilioni yote hayo yakiingia mfukoni mwa
serikali na wafanyabiashara, mgunduzi wa madini hayo, Jumanne Mhero Ngoma (74),
anaishi kwa kutegemea ruzuku za watoto. Mapato yake kwa mwaka ni shilingi za
Tanzania sifuri!
Nilikutana na Mzee Ngoma siku chache zilizopita jijini
Dar es Salaam katika ofisi ya mmoja wa wanawe. Pamoja na masahibu na mikasa
mbalimbali iliyomkumba katika maisha yake, bado aliweza kunipokea kwa bashasha
na tabasamu.
Amefanya mahojiano na vyombo mbalimbali vya habari na
pengine ameanza kuchoka sasa. Mvi kichwani kwake na kwenye eneo la ndevu ni
ishara kwamba umri unaanza kumtupa Mzee Ngoma.
Nimekaa namtazama. Huyu ndiye mtu aliyegundua madini ya
Tanzanite. Alipaswa kuwa utambulisho wa Watanzania. Katika nchi nyingine
zinazothamini watu wake, huyu alitakiwa kufahamika na watu wote waliomaliza
elimu ya msingi.
Kama ambavyo watoto wote wa Kimarekani wanavyomfahamu
Thomas Edison (mbunifu mashuhuri na mfanyabiashara wa karne kadhaa zilizopita)
. Lakini mbele ya macho yangu, alikaa mzee mmoja ambaye kama ningekutana naye
kwenye daladala (na ndiyo usafiri wake mkuu), nisingemtazama mara mbili.
Namuuliza swali moja la msingi kwamba ilikuwaje yeye
aliyagundua madini ambayo wakoloni (wazungu) walishindwa kuyabaini kwa muda
wote waliokaa hapa nchini.
“Nakumbuka kila kitu kuhusu mara yangu ya kwanza kuona
madini hayo. Mara ya kwanza kuyagundua madini haya nilikuwa mdogo sana.
Nilikuwa na umri wa chini ya miaka 20 na nilikuwa porini nikichunga mifugo.
“Nilikuwa kwenye msitu ambao Wamasai walikuwa wameupa
jina la Lalouo. Eneo ambako niliyaona lilikuwa linafahamika kwa jina la
Naisunyai ambako kwa kawaida Wamasai
walikuwa wakilitumia kunywesha mifugo yao.
“Siku hiyo niliona vitu vinavyowaka. Nikawa nashangaa
vitakuwa ni vitu gani. Awali nilidhani pengine ni nyoka au wanyama wa hatari.
Nikasogea nikiwa na upinde na mshale wangu tayari kwa lolote.
“Nilipogusa na mti niliokuwa nimeushika, nikashangaa
mawe yanayong’aa yakitoka ardhini. Vipande vidogo vidogo vyenye rangi ya bluu.
Kwa kweli nilivipenda sana.
“Nilishangaa sana lakini ghafla nikakumbuka kuwa
nilikuwa nachunga mifugo. Kumbe ng’ombe na mbuzi niliokuwa nawachunga walikuwa
wamekimbia tayari. Nikaacha shughuli hiyo na kwenda kuwafuata.
“Kwa bahati nzuri, nilifuatilia njia walizopita hadi nikawapata
wote. Lakini ilikuwa kazi ngumu maana ule ulikuwa msitu mkubwa. Nikarudi
nyumbani nikiwa na mifugo ile na nikawa nimesahau kabisa habari za madini yale
kwa muda ule,” anasema.
Mtoto wa Ngoma aitwaye Asha aliyekuwa mwenyeji wetu
kwenye ofisi ile ananiuliza kama naweza kutumia kinywaji chochote. Namwomba
samahani kwa kuwatia hasara maana nikaagiza vinywaji viwili badala ya kimoja.
Maji na soda. Kwenye dunia hii ya kisukari, kunywa soda pekee bila kuchanganya
na maji kunaleta hatari ya kuongeza sukari mwilini.
Mzee Ngoma yeye anaomba maji tu. Tunasubiri kidogo.
Tunapiga mafunda mawili matatu na kisha tunaendelea na mazungumzo yetu.
Hata hivyo, mwaka 1966 ilitokea bahati iliyobadilisha
maisha yangu. Mwanzoni mwa mwaka huo, serikali ilitangaza kuwepo kwa mafunzo
kuhusu utafiti wa madini yaliyopangwa kufanyika mkoani Morogoro.
“Mimi wakati huo nilikuwa nafanya biashara zangu tu
lakini nilikuwa mpenzi sana wa masuala ya madini na ndiyo nilipoyaona madini
yale ya Tanzanite kwa mara ya kwanza nilishikwa na hamu ya kutaka kuyajua.
“Ulitakiwa kujilipia mwenyewe nauli na gharama nyingine
halafu serikali inakulipia mafunzo hayo kwa muda wa wiki tatu. Nikazungumza na
mke wangu kuhusu hilo na akaniruhusu niende kwenye mafunzo.
“Nilikwenda Morogoro na hatimaye nikafaulu kwenye
mafunzo hayo. Ilipofika tarehe sita, mwezi wa sita mwaka 1966, nikapewa cheti
cha utafiti ambacho ninacho hadi leo. Pamoja na mambo mengine, cheti hicho
kilikuwa kinakuwezesha kufahamu madini na sifa zake mbalimbali,” anasema.
Ni mafunzo hayo ambayo baada ya kuyamaliza yalimfanya
Ngoma aweze kugundua madini hayo ya Tanzanite.
Lakini kabla ya madini hayo, mzee huyu kwanza aligundua
madini aina ya Gypsum ambayo sasa yanatumika katika nyumba nyingi za Watanzania
wenye kipato kuanzia cha kati hadi cha juu.
Aliyagundua madini hayo katika eneo la Chankoko, Makanya
mkoani Kilimanjaro.
“Wakati nikigundua madini hayo, hayakuwa na kazi sana.
Watu wengi hawakujua kazi yake. Kwa bahati nzuri, katika wakati huohuo, kukawa
na kiwanda cha saruji cha WAZO ambacho kilitaka kuanza kufanya shughuli zake na
gypsum ilikuwa ni malighafi nzuri sana.
“Kuna bwana mmoja aitwaye Petro Gerson Kizigha
akanikutanisha na wazungu waliokuwa wakitaka kuanzisha kampuni hiyo na tayari
wakiwa na taarifa za gypsum niliyoigundua.
“Nakumbuka majina ya wazungu hao yalikuwa ni Florench,
Carter na Habel. Walikuja hadi Makanya kwa ndege binafsi na walishukia katika
shamba la katani la bwana mmoja aliyekuwa akiitwa Hassan.
“Walipoona gypsum ile wakaipenda sana. Wakaagiza mara
moja mzigo wa tani 36 ambao tuliupakia kwenye mabehewa. Kuna barabara kutoka
Chankoko hadi stesheni ya reli ya Makanya yenye urefu wa kilomita 10 ilijengwa
ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa hiyo.
“Mimi ndiye niliyepewa jukumu la ujenzi wa barabara
hiyo. Nilipewa na wazungu wale kiasi cha Sh 8,000 kwa ajili hiyo. Kwa wakati huo, hiyo ni hela nyingi sana.
Wajenzi walikuwa wakilipwa shilingi nne kwa siku na
zilikuwa nyingi kiasi kwamba watu walikuja kuomba kazi kwa wingi hadi wengine
nikawakataa, anasema.
Pamoja na mafanikio hayo katika biashara ya gypsum, kuna
kitu kimoja kilikuwa kinamsumbua Ngoma kichwani kwake. Yale madini aliyoyaacha
kule Umasaini, Marerani yalikuwa ni madini gani?
“Ndipo siku moja nikawachukua ndugu zangu na kuwaomba
wanisindikize kwenda kwenye ule msitu wa Lalouo ili nikayachunguze tena yale
madini. Niliomba kusindikizwa kwa sababu ule msitu ni mkubwa na nilitaka pia
nipate watu wa kunisaidia kubeba.
“Nakumbuka tulichimba karibu kilo sita za madini hayo.
Kuna jiwe moja lilikuwa na ukubwa wa takribani gramu 55 hivi. Jiwe kubwa tu.
Ndilo lililokuwa kubwa zaidi.
“Nikalipeleka Moshi kwenye Ofisi ya Mkaguzi wa Madini
aliyekuwa akiitwa Bills wakati huo. Mzungu huyo. Akayatazama na akasema
hajawahi kuona kitu kama kile. Akahisi yanaweza kuwa Blue Tomaline, lakini
tukakubaliana kuwa si yenyewe.
“Mimi nikamuuliza sasa mwenzangu unadhani haya ni madini
gani? Unajua wazungu ni watu wakweli kidogo. Wana matatizo yao lakini hawapendi
kusema uongo. Akasema kwa kweli siyajui. Inabidi tuyapeleke kwenye maabara ya
serikali iliyokuwa iko Dodoma.
“Nikampa sampo yote niliyokuwa nayo lakini lile jiwe
kubwa zaidi nikabaki nalo. Alipoliona, mke wa bwana Bills akawa amelipenda
sana. Akaniomba abaki nalo.
“Nikakataa. Nikamwambia kama nikikupa, nitakuwa nakupa
nini? Maana mumeo ambaye ndiye mtaalamu
wa mambo haya ameshindwa kuyajua. Siwezi kukupa na nitabaki na hili kama
kumbukumbu yangu.
“Ilipofika Septemba 23 mwaka 1967, ndipo nikapokea barua
rasmi kutoka maabara ya Dodoma. Vipimo vikaonyesha madini yale yanafahamika kwa
jina la Zoisite. Ndiyo maana tunasema madini hayo yaligunduliwa rasmi mwaka huo
wa 1967 kwa sababu ndipo cheti kile cha maabara kilipotoka,” anasema.
Katika simulizi kuhusu gunduzi mbalimbali za madini hapa
nchini, zipo zinazoeleza namna wananchi wa Shinyanga walivyokuwa wakicheza bao
kwa kutumia almasi kwa sababu hawakujua thamani yake.
Hali iko hivyo kwa Mzee Ngoma ambaye alikuwa akilitumia
jiwe hilo la gramu 55 kwa ajili ya kuzuia karatasi zake zisipepee kutoka mezani
kwake. Lilikuwa jiwe la kawaida kabisa ndani ya nyumba yake.
Nimeangalia bei ya sasa ya Tanzanite ili upate picha ya
nini mzee huyu alikuwa nacho ndani kwake. Kwa sasa, bei ya madini hayo katika
soko la dunia inacheza kati ya dola 500 hadi 700 kwa karati moja.
Zipo taarifa kwamba zipo sehemu duniani ambako watu
wanauziwa hadi dola 1000 kwa karati moja. Tuseme wastani ni dola 600 (sh
800,000) kwa karati moja.
Karati moja ni sawa na gramu 0.2. Gramu 55 maana yake ni
karati 275. Kama bei ya karati moja ni Sh 800,000, bei ya karati 275 ni sawa na
takribani Sh milioni 220.
Mzee Ngoma alikuwa anatumia Sh milioni 220 kuzuia
karatasi na magazeti yasipeperuke kutoka mezani kwake ! Mzee huyu hakujua kitu
wakati huo.
Jiwe hilo kipenzi la mgunduzi huyu likaja kumpotea
katika mazingira ya kutatanisha. Simulizi yake, ilinifanya niombe mahojiano
haya yapumzike kidogo ili niweze kuvuta pumzi.
“Nilikuwa na marafiki wawili wenye asili ya kihindi
waliokuwa wakiishi Handeni mkoani Tanga. Mmoja akiitwa Habib Esack Ismail na
mwingine akijulikana kwa jina la Nuru Skanda. Walikuja siku moja nyumbani
kwangu na wakaliona lile jiwe.
“Wakaniomba waende nalo kwao (Handeni) ili wakawaonyeshe
wazazi wao wajue la kufanya. Wakati huo, Zoisite ama Tanzanite kama
inavyofahamika sasa, haikuwa maarufu sana na matumizi yake hayakuwa
yakijulikana.
“Walisema watalirudisha baada ya siku tatu. Nikawapa na
wakaondoka nalo. Hawakurudi baada ya siku tatu na sijawaona tena tangu wakati
huo. Siku moja nilikutana na aliyekuja kuwa Kamishina wa Madini hapa nchini
aliyejulikana kwa jina la Luwena na akaniambia lile jiwe liko Ujerumani na
waliuziwa kwa Sh 6000 kwenye miaka hiyo.
“Hizo ni hela nyingi sana. Ina maana akina Habib
waliliuza na wakaondoka zao. Lile jiwe linaniuma sana maana kama ningebaki nalo
pengine lingeweza kunipa fedha nyingi,” anasema Ngoma.
Machungu ya Mzee huyu hayakuishia hapo. Kuna unyama
mwingine mkubwa zaidi ambao alifanyiwa.
Baada ya kuibiwa jiwe lake hilo, akili ya Ngoma ilifanya
kazi haraka na akaamua kwenda kupata leseni ya umiliki wa eneo ambako aliyapata
madini yale.
Akapewa viwanja nane kwenye eneo lile la Lalouo ambako
alilipia kiasi cha Sh 15 kwa kila kimoja. Akaweka alama zote muhimu na kuamini
kwamba lile ni eneo lake halali kisheria na mara wakati utakapofika, ataanza
kuchimba madini hayo.
“Siku moja mwezi Februari mwaka 1968, nikaenda
kutembelea kwenye eneo lile. Nikamkuta kijana mmoja anaitwa Daudi Mayaya akiwa
anachimba madini hayo kwenye eneo langu. Alikuwa ameyajaza kwenye ndoo.
“Nikamwambia kwanini amechimba madini hayo kwenye eneo
langu? Akanijibu kwamba lile si eneo langu bali ni la mtu mmoja aiwaye De Souza
(Huyu nitamweleza zaidi baadaye). Nikamwonyesha alama zangu zote nilizoweka
pamoja na nyaraka nilizokuwa nazo.
“Nilipoenda kushitaki Polisi kuhusu huyu mtu anayeitwa
De Souza, nikaambiwa ataitwa na atafika Jumatatu. Bila ya taarifa, kumbe huyo
bwana akaja Jumamosi na akazungumza na polisi mapema.
“Mkuu wa Polisi kwenye eneo letu alikuwa akifahamika kwa
jina la Herbert Kitenge. Huyu bwana akaniita Polisi na akaniambia ameamua kumpa
De Souza vitalu (viwanja) vinne kati ya nane nilivyokuwa navimiliki.
“Sasa mimi nikabaki nimeshangaa, inakuaje mtu anapewa
vitalu vyangu. Lakini afande Kitenge akasema ama nikubali hiyo dili au
nitanyang’anywa vyote. Nikakasirika sana na nikasusa kabisa. Sikurudi tena kule
kwenye machimbo. Nikaenda kufanya biashara zangu,” anasema kwa huzuni.
Mzee Ngoma anamtaja De Souza mara nyingi katika maelezo
yake. Manuel De Souza, mzaliwa wa Goa nchini India alikuja nchini Tanganyika
mnamo mwaka 1933 akiwa na umri wa miaka 20 tu na tayari akiwa fundi cherehani
mzuri.
Taarifa katika mitandao mbalimbali duniani inamtaja yeye
kama mvumbuzi wa Tanzanite. Mtandao wa Ilios Jewellers unadai kwamba Julai
mwaka 1967, kundi la Wamasai, lilimpeleka Mhindi huyo kwenye eneo ambako
aligundua madini hayo.
Kwenye mtandao unaoheshimika zaidi duniani wa Wikipedia
unamtaja fundi cherehani, Emmanuel Merishiek Mollel kama mgunduzi wa madini
hayo. Katika maelezo yake, mtandao huo unadai kwamba ni Mollel ndiye aliyempa
De Souza madini hayo na yeye akayapeleka kwa wataalamu ambao waliyabaini kwamba
ni Tanzanite.
Hata historia inapindishwa ili Mzee Ngoma akose hadhi na
heshima anayostahili !
Kabla ya kuitwa Tanzanite, madini haya yalikuwa
yakifahamika kwa jina la Zoisite. Jina hilo, kwa mujibu wa maelezo ya nyaraka
mbalimbali, lilitokana na raia wa Austria, Siegmund Zois, ambaye alikuwa
akifadhili safari mbalimbali za watu waliokuwa wakitafuta madini mbalimbali.
Kwa Kijerumani, neno Zoisite linafanana kimatamshi na
neno la Kiingereza Suicide. Kampuni iliyokuwa ikifanya biashara ya Tanzanite ya
Tiffany& Co. ndiyo ikaamua kubadili jina hilo na kuyaita madini hayo
Tanzanite ili liwe na mvuto.
Hakukuwa hata na mmoja aliyeona yanafaa kuitwa Ngomanite
au Ngomasite !
Mwaka 1984, serikali iliamka kutoka usingizini na
kumtaja Mzee Ngoma kama mvumbuzi wa madini hayo. Kama zawadi yake kwa uvumbuzi
huo wa kihistoria, serikali ilimpa mzee huyo Ngao, cheti cha kumtangaza kama
mvumbuzi na fedha taslim Sh elfu 50,000.
Kwa mujibu wa Wikipedia, katika kipindi cha kati ya
mwaka 1967 hadi mwaka 1972 wakati serikali ilipoamua kutaifisha shughuli za
uchimbaji wa Tanzanite, kiasi cha karati milioni mbili zilikuwa tayari
zimechimbwa kutoka Mirerani.
Kwa bei ya sasa ya karati moja, maana yake ni kwamba kwa
miaka hiyo mitano pekee, De Souza, washirika wake kama vile Ally Juyawandu na
askari jeshi mmoja aliyekuwa na asili ya Ugiriki aliyefahamika kwa jina moja tu
la Papanichalou, walifanikisha biashara yenye thamani ya takribani Sh trilioni
1.6 kwa thamani ya sasa !
Watoto wa De Souza aliyefariki dunia mwaka 1969 akiwa na
umri wa miaka 56 kwa ajali ya gari, wametapakaa katika nchi mbalimbali kama
vile Denmark, Malta na Uingereza, pengine wakila faida ya ‘ugunduzi’ wa baba
yao.
Kwa upande mwingine, Mzee Ngoma amejibanza katika ofisi
ndogo ya mwanaye Asha katikati ya jiji. Fedha pekee ambayo ameitengeneza
kutokana na kuipa Tanzania sifa na utajiri huu wa kipekee ni Sh elfu 50,000
zile alizopewa na Hayati Rashid Mfaume Kawawa !
Namuuliza shujaa huyu wa taifa anataka nini kutoka kwa
serikali; “Sihitaji mambo makubwa sana. Ninachohitaji ni kuishi maisha
yanayofanana na Tanzanite. Nataka mtu akiniona mimi aone Tanzanite,” anasema.
Ni ombi ambalo linanisisimua. Watanzania wanapaswa
kuwafahamu watu kama akina Ngoma. Serikali inapaswa kuwaenzi watu kama akina
Mzee Ngoma.
Hawa watachochea watu wawe wagunduzi zaidi. Simulizi zao
zitafanya watu wajenge akili ya kuhoji kila wanachokiona. Nani ajuaye, pengine
kuna ‘Tanzanite’ nyingine katika maeneo mbalimbali hapa nchini lakini
hazijulikani kwa vile hakuna akina Ngoma?
Nani atataka kuwa mgunduzi wa vitu vya thamani iwapo
wagunduzi waliopo tunapanda nao daladala, tunashinda nao njaa na hawathaminiki?
Serikali imfanye Mzee Ngoma afanane na faida ambayo
Tanzanite imeiletea nchi yetu.
CHANZO: Raia Mwema

0 comments:
Post a Comment