Na Seif Abalhassan
Wiki hii rabsha na vita vimezuka tena huko Msumbiji kati
ya Renamo na Frelimo, vita hivyo pamoja na mambo mengine vimenikumbusha juu ya
Kanali Ali Mahfoudh.
Kanali Ally Mahfoudh, Mkurugenzi wa zamani wa Operesheni
wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Mwanajeshi mshika mbele katika harakati za
Ukombozi wa Nchi za Afrika, Shujaa wa Mapinduzi ya Zanzibar, Mjamaa na Komredi
wa kweli ni mtu muhimu sana maishani mwangu.
Kwetu Bomboka Tanga kuna Kijiwe Maarufu kiitwacho
Jamaika, kijiwe nchi kiko mita kama 100 kutoka ilipo nyumba yetu, makutano ya
Barabara ya 16 na mtaa wa Majimaji, Kata ya Majengo, Maarufu zaidi kama
nyumbani kwa Mzee Mwaruwa, Muungwana wa Umwamwande aliyekuwa 'Mwanazuoni wa
Umma' akijitolea kurithisha elimu ya Utu, Maadili, Haki, Utamaduni na Uzalendo
kwa vijana wadogo wa mitaa ile, miaka ile ya utoto wangu ndipo nilimjua Kanali
Mahfoudh kupitia kijiwe chetu kile.
Kanali Ali Mahfoudh ni Mmoja wa Wanajeshi wa Jeshi la
Wananchi wa Tanzania, JWTZ waliotajika sana kwa Miaka hii 50 ya Jeshi letu
hili, visa vya Ushupavu, Ushujaa na Umahiri wake Vitani zikielezewa kwa Vijana
na kuwashajiisha wengi kutamani kuingia Jeshini kufuata njia yake njema ya
Utumishi wa Kutukuka, Kujituma, Weledi, Ushupavu na Ushujaa.
Akifanya kazi njema ya Ukombozi tokea Mapinduzi ya
Zanzibar ambapo vipawa vyake na Umahiri wake Jeshini vilionekana mwanzoni tu,
akitajwa kama Komandoo aliyeogopwa kutoka Chama cha Makomredi, Umma Party
aliyepata Mafunzo yake ya Kijeshi Nchini Cuba mwanzoni tu mwa miaka ya 60.
Mahusiano haya ya Makomredi na Cuba yakitajwa na kuhusishwa zaidi na Komredi
Ali Sultan Issa.
Mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuundwa kwa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kanali Ali Mahfoudh na wengi wa Makomredi
wenziwe waliingizwa kwenye Serikali ya Muungano na kuondolewa kabisa Zanzibar
kwa sababu ya hofu ya Rais Abeid Amani Karume juu ya Ujemedari wao, Usomi wao
na "Utata" wao.
Zaidi walionekana ni vijana wasomi na wajamaa waliokuja
na lengo la kusimika uongozi mpya wenye kusimamia misingi ya Utu, Haki, Usawa
na Ukombozi wa Kweli wa Wanyonge, jambo ambalo halikuwa lengo hasa la
Wahafidhina wengi wa ASP kama Karume mwenyewe, Kanali Seif Bakari Mussa,
Brigedia Ramadhani Haji Faki, Abdallah Said Natepe na wengineo wa aina hiyo.
Kanali Mahfoudh alipata Umaarufu zaidi kati ya Mwaka
1964 - 1972 kwa nafasi yake ndani ya JWTZ katika kuvisaidia Vyama vya Ukombozi
vya Afrika kama FRELIMO, ZANU, ZAPU na MPLA katika vita vya Msituni vya
Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika, na pia akitajwa kuwa ndiye aliyeongoza
Kikosi cha JWTZ katika RABSHA moja Maarufu na 'Nyeti' dhidi ya Uchokozi wa Rais
Kamuzu Banda wa Malawi juu ya Utata wa Mipaka ya Ziwa Nyasa.
Wakati wa Mapambano ya Frelimo kudai Uhuru kutoka kwa
Waremo Kanali Mahfoudh alijichimbia Nachingwea akiwasapoti Majemedari wa
Msumbiji, Kina Samora Machel, Joachim Chisano, Albarto Sipande, Raymundu
Pasinuwapa na wengineo katika ukombozi wa nchi hiyo kutoka Mikononi mwa
Wakoloni hao waonevu. Nchi ambayo pia alizikwa kama Shujaa wa Taifa hilo na
Afrika kwa ujumla.
Kati ya Mwaka 1972 mpaka mwaka 1978 aliwekwa kizuizini
Jijini Dar es salaam kwa Tuhuma za kuhusika na Mauaji ya Rais wa Kwanza wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Makamo wa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Sheikh Abedi Amani Karume, na akahukumiwa Kifo katika
Kesi ambayo iliendeshwa Zanzibar na Jaji Wolfango Dourado bila yeye kuwepo.
Wengine waliotiwa Kizuizini pamoja naye ni Profesa
Abdulrahman Mohammed Babu, Tahir Ali Salim, Hashil Seif Hashil, Salim Saleh
Salim, Ali Yusuf Baalawi, Hemed Hilal Mohammed, Suleiman Mohammed Abdullah,
Amour Mohammed Durgheish, Ahmed Mohammed Habib, Haji Omari Haji, Saleh
Abdallah, Abdallah Juma Khamis, Ali Salim Hafidh, Shaaban Salim Mbarak, Badru
Said, Ali Mohammed Ali na Abdulaziz Abdulkadir Ahmed, Makomredi wengine kama
Ali Sultan Issa, Sharifu Ahmad Badawy Qullatein na wenziwao walishikiliwa
Zanzibar.
Baada ya Mbinyo mkali kutoka Shirika la Haki za Binaadam
la Amnesty International na Mataifa ya Kigeni juu ya kushikiliwa kwao, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu Julius Kambarage Nyerere alitoa amri ya
kuachiwa kwa Kanali Ali Mahfoudh na Makomredi wenzie Aprili 26, Mwaka 1972.
Mara baada ya kutolewa Gerezani Kanali Ali Mahfoudh alichukuliwa na Serikali ya
Msumbiji kwa Ombi Maalum la Rais Samora Machel kwa kuthamini mchango ambao
Nguli huyu alitoa kwa Nchi hiyo, japo ikidaiwa pia kuwa kulikuwa na Makubaliano
Maalum ya Kuhakikisha Kanali Ali Mahfoudh hakanyagi tena Ardhi ya Tanzania.
Nchini Msumbiji Kanali Mahfoudh alikuwa Mshauri Mkuu wa
Mambo ya Kijeshi wa Rais Samora Machel na baadaye Rais Chisano na kwa kiasi
kikubwa ndiye anayetajwa kulisaidia Jeshi la Msumbiji kimbinu katika kupambana
na Waasi wa Renamo waliokuwa wakipewa Msaada wa Mbinu za Kijeshi, Silaha na
Fedha kwa Dhahiri na Makaburu wa Afrika ya Kusini pamoja na Mataifa mengi
makubwa ya Magharibi na Marekani. Kwa kutambua Ushujaa na Ujuzi wa Mbinu
mbalimbali za Vita wa Kanali Ali Mahfoudh, Makaburu walijaribu Mara tatu kutaka
kumuua lakini mara zote walishindwa katika Majaribio yao hayo.
Kanali Ali Mahfoudh aliendelea kuishi Msumbiji hata mara
baada ya kustaafu kazi yake ya Ushauri wa Mambo ya Kijeshi kwa Serikali ya
Msumbiji, Baadaye alijiingiza kwenye Biashara, mara nyingi alikuwa Akipatikana
katika Klabu ya Watanzania iliyokuwa katika Jengo la Ubalozi wa Tanzania Nchini
Msumbiji ambalo tulipewa zawadi na Serikali ya Msumbiji kwa msaada wetu kwao.
Hata alipofariki Dunia Nchini humo bado Kanali Ali Mahfoudh hakurudishwa
Tanzania na alizikwa Katika Makaburi ya Mashujaa (Heroes Cemetary) Jijini
Maputo huko huko Msumbiji.
Mengi ya hayo juu ya Kanali Mahfoudh niliyajulia kwa
Mzee Mwaruwa. Miezi miwili iliyopita nilikuwa Zanzibar kikazi, nikivitembelea
Visiwa vya Karafuu vya Unguja na Pemba kwa muda wa zaidi ya juma moja.
Nikitumia wasaa huo kutekeleza wajibu ulionipeleka Visiwani humo lakini pia
nikitumia vema fursa na muda mchache nilioupata kujaribu kujifunza mema ya
Wanzanzibari. Naomba nikiri kuwa mimi si Mpenzi sana wa siasa za vilivyokuwa
vyama vya Ukombozi vya Zanzibar vya ASP na ZNP, kwa machache niliyojifunza na
kuyasoma juu ya historia ya vyama mbalimbali vya siasa Zanzibar nimejikuta
nikiwa na imani sana na Umma Party, Chama cha Kijamaa kilichokuwa kikiongozwa
na Profesa Abdulrahman Mohammed Babu. Hivyo kwa kiasi kikubwa nilipanga
kujifunza machache juu ya Chama hiki.
Nakumbuka kuhudhuria Tamasha la 'Kamati ya Maridhiano ya
Zanzibar' katika Ukumbi wa Salama, pale Bwawani, siku ambayo Mansour Yussuf
Himid alitoa ya moyoni baada ya kufukuzwa Uanachama ndani ya CCM, tukio
lililonipa wasaa wa kukutana na Mzee wangu Hassan Nassoro Moyo pamoja na
Waungwana Ismail Jussa, Eddy Al Mugheiry na Salim Bimani. Jioni ya siku hiyo
nikakutanishwa na Mama Naila Jidawi, Mwanamke Jasiri wa Tanzania, Mwanasiasa
Nguli wa Maridhiano, Mfanyabiashara aliyekumbana na Vikwazo vingi na aliyekuwa
Mke wa Kanali Ali Mahfoudh.
Mama Mkarimu, Mzungumzaji na Mcheshi ambaye nikiri kuwa
kwake nilijifunza mengi juu ya Mumewe na Tanzania ambayo sikuwahi kuyajua,
nilijisikia faraja sana aliponionyesha Picha yake akivalishwa Medali ya Heshima
na Ushujaa ya Uganda na Rais Yoweri Kaguta Museveni, kwaajili ya kutambua mchango
wa Kanali Ali Mahfoudh kwa jeshi la nchi hiyo wakati wa mapambano ya msituni
yaliyomuingiza Madarakani Museveni.
Mama Naila alivutiwa na udadisi wangu juu ya Mumewe na
kwa hilo alifanya mipango nikaonane na Mwanaye wa mwisho 'Che Guevara' Mahfoudh
huko Bwejuu, Nje Kidogo ya Mji wa Unguja.
Pamoja na Rafiki yangu Hamed Mazrui tunapelekwa Bwejuu
na kupokelewa naye 'Che Guevara' katika hoteli yao ya Palm Beach hapo Bwejuu,
kitu kimoja cha kuvutia zaidi ni mmoja wa watoa huduma Hotelini hapo, Kijana
Hashim kutoka Bomboka aliyeajiriwa Hotelini hapo ambaye alifurahi na zaidi
kushangazwa juu ya kukutana kwetu hapo.
Kama alivyo mamiye Che Guevara naye ni mtu Mkarimu,
Mchangamfu na Muongeaji mno, tulizungumza kwa kirefu juu ya babiye, siasa za
Zanzibar, hali ya Ubaguzi, Sekta ya Utalii Zanzibar, Heshima ya Kanali Mahfoudh
nchini Msumbiji na hata juu ya kipawa chake cha uimbaji na kupiga gitaa
alichokirithi kutoka kwa baba yake.
Sikujua jambo moja kuhusu Kanali Ali Mahfoudh, Mwaka
1961 alikuwa CUBA katika Afisi Maalum juu ya Ukombozi wa Afrika Nchini humo,
safari ambayo ilibadili mtazamo wake juu ya Ujamaa na hata msimamo wake juu ya
maisha.
Athari kubwa zaidi juu ya safari yake hiyo ni majina ya
watoto wake ambayo ni kumbukumbu njema ya mafungamano yake na Mashujaa ya
Visiwa hivyo vya Kijamaa vya Amerika.
Kanali Ali Mahfoudh na Mkewe Mama Naila Jidawi
wamefanikiwa kupata watatu katika Ndoa yao, Kijana Kamilo 'Cienfuegos'
Mahfoudh, Binti Celia 'Sánchez' Mahfoudh na 'mziwanda' Che Guevara Mahfoudh.
Majina hayo ni kumbukumbu ya Mashujaa wa Mapinduzi wa
CUBA Kamilo Cienfuegos Gorriarán (Februari 6, 1932 – Oktoba 28, 1959), Celia
Sánchez Manduley (Mei 9, 1920 – Januari 11, 1980) na Erneto Che Guevara (Juni
14, 1928 – Oktoba 9, 1967)
Kumuenzi baba yake, Che Guevara Mahfoudh ameyafanya
majina ya vyumba vya Hoteli yao ya Palm Beach hapo Bwejuu yabebe kumbukumbu hii
njema ya maisha na nyakati za Kanali Ali Mahfoudh.
Mola amlaze pema Kanali Ali Mahfoudh na aiepushie mbali
vita mpya inayonukia Nchini Msumbiji. Mungu ibariki Afrika.

0 comments:
Post a Comment