![]() |
| Essam el-Erian |
Na Kabuga Kanyegeri
VIKOSI vya usalama nchini Misri vimemkamata kiongozi
mwandamizi wa vuguvugu la Udugu wa Kiislamu, Essam el-Erian, katika muendelezo
wa kulidhibiti vuguvugu hilo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi hiyo,
Erian ambaye ni naibu kiongozi wa chama cha Uhuru na Uadilifu kilicho chini ya
vuguvugu hilo, amekamatwa leo baada ya Kikosi Maalumu kuivamia nyumba yake.
Amekamatwa kufuatia amri iliyotolewa na mwendesha
mashitaka wa serikali, ambaye alimtuhumu kwa “kuchochea ghasia” na “kusaidia
vitendo vya kihalifu.”
Erian ndiye kiongozi pekee wa ngazi ya juu wa vuguvugu
hilo ambaye alikuwa hajakamatwa baada ya viongozi wengine wote wa kundi hilo
kutiwa nguvuni.
Idadi kubwa ya maafisa wa vuguvugu la Udugu wa Kiislamu
wamewekwa korokoroni na vikosi vya jeshi na polisi tangu kuondolewa madarakani
kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Muhammad Mursi mapema mwezi Julai.
Mnamo Julai 3, mkuu wa jeshi la Misri, Jenerali
Abdulfattah al-Sisi alitangaza kuwa Mursi alikuwa ameondolewa madarakani baada
ya “jeshi kumpiindua.” Vilevile al-Sisi alisitisha matumizi ya katiba na kulivunja
bunge.
Mwezi Septemba, mahakama moja nchini humo ililipiga
marufuku vuguvugu la Udugu wa Kiislamu kufanya kazi kama taasisi isiyokuwa ya
kiserikali (N.G.O) na kuamuru mali zake zote zitaifishwe.
Katika wimbi jingine la kulibana vuguvugu hilo, mwezi
Agosti, kwa uchache watu 1,000, wengi wao wakiwa wafuasi wa Mursi, waliuawa na
wanachama wengine wa vuguvugu hilo wapatao 2,000 wakakamatwa, baada ya serikali
ya mpito iliyoteuliwa na jeshi kuamuru kuyasambaratisha maandamano ya kumuunga
mkono Mursi.
Vuguvugu hilo kongwe liliunda chama cha kisiasa mwaka
2011, miezi kadhaa baada ya kuanguka kwa rais wa zamani, Husni Mubarak.

0 comments:
Post a Comment