WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amesema kuwa ujenzi
wa daraja katika Mto Malagarasi, mkoani Kigoma umekamilika.
Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo baada ya kufanya ziara
katika eneo hilo wiki iliyopita ambapo alisema kuwa ameridhishwa na hatua ya
ujenzi huo ulipofikia kwa kiwango cha juu.
“Nimeridhishwa na utendaji wa mkandarasi huyu, hasa kwa
jinsi alivyoweza kumaliza sehemu hii ya kwanza kwa muda mzuri na viwango vya
hali ya juu,” alibainisha Magufuli.
Alisema Kampuni ya M/S Hanil Engineering and
Construction Company Limited za nchini Korea Kusini ziliingia mkataba na kuanza
ujenzi wa daraja hilo Desemba 2010 huku wakitakiwa kukamilisha kazi hiyo
ifikapo Desemba 2013.
Alisema kuwa mradi huo unajumuisha ujenzi wa madaraja
matatu yenye jumla ya urefu wa meta 275
pamoja na barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 48 kwa gharama ya sh
bilioni 90 zilizotolewa na Benki ya Exim ya Korea Kusini kwa asilimia 90 huku
kiasi kilichobaki kikiwa ni fedha za ndani.
Alisema kuwa hivi sasa kuna ongezeko kubwa la magari
kati ya Manyoni – Itingi – Tabora hadi Kigoma kupitia katika Daraja hilo la
Kikwete, hali ambayo awali ililazimu kupitia barabara ya Manyoni – Singida -
Nzega – Kahama – Nyakanazi – Kibondo – Kasulu hadi Kigoma.
Naye Mhandisi wa mradi huo, Yu Sing, wa Kampuni ya Hanil
Engineering alisema kuwa mradi huo umegawanywa katika sehemu mbili.
“Sehemu ya kwanza ambayo ndiyo iliyokamilika ni ujenzi
wa madaraja matatu yenye urefu wa meta 25, meta 200 na meta 50 pamoja na
kilometa 11 za lami na sehemu ya pili ni ujenzi wa kilometa 37 za lami ambazo zinaendelea
kukamilishwa kwa sasa,” alisema.

0 comments:
Post a Comment