AFISA mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Pakistan
amesema kuwa nchi hiyo imemuachia huru kiongozi mwandamizi wa Taliban la
Afghanistan, Abdul Ghani Baradar.
Baradar, ambaye alielezwa kuwa kiongozi namba mbili wa
wapiganaji wa Taleban ameachiwa huru leo Jumamosi.
“Ndiyo, Baradar ameachiwa huru,” msemaji wa wizara ya
mambo ya ndani, Omar Hamid, alisema bila
kutoa taarifa zaidi kuhusu mazingira ya kuachiwa kwa mfungwa huyo.
Mapema Ijumaa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan
ilisema kuwa kuachiwa huru kwa Baradar mwenye umri wa miaka 45, anayejulikana
pia kama Mullah Baradar, kungesaidia mchakato wa amani nchini Afghanistan.
“Ili kuweka mazingira mazuri ya mchakato wa maridhiano
nchini Afghanistan, kiongozi huyo wa Taliban, Mullah Abdul Ghani Baradar,
angeachiwa kesho (leo),” ilisema taarifa ya wizara hiyo.
Serikali ya Afghanistan imekuwa ikiitolea wito Pakistan
kumuachia huru Baradar, ambaye alitiwa nguvuni katika mji wa Karachi Julai
2010.
Rais wa Afghanistan, Hamid Karzai, anafanya juhudi za
kuanzisha mazungumzo ya moja kwa moja baina ya serikali yake na wapiganaji wa
Taliban ili kurejesha amani iliyozorota nchini mwake.
Tangu mwaka jana, Pakistan imewaachia huru wafungwa
wapatao 33 wa Kitaliban baada ya kuombwa na Afghanistan ili kusukuma mbele
juhudi za mazungumzo ya amani.
Kwa upande wa serikali ya Afghanistan iliupokea kwa
furaha uamuzi huo. “Tunaikaribisha na kuipokea hatua hii iliyochukuliwa. Tunaamini
kuwa hili litasaidia kwenye mchakato wa amani ya Afghanistan,” alisema msemaji
wa Rais Karzai, Aimal Faizi.
Marekani na waitifaki wake waliingia vitani nchini
Afghanistan Oktoba mwaka 2001 katika kile kilichoitwa kuwa ni vita dhidi ya
ugaidi.
Hatua hiyo iliwaondoa Taliban madarakani, lakini baada
ya zaidi ya miaka 11, vikosi hivyo vya kigeni havijaweza kuleta usalama nchini
humo.

0 comments:
Post a Comment