MANDELA ATOKA HOSPITALI

Picture taken on July 16, 2013 shows a wall of tributes for former South African President Nelson Mandela outside the Medi Clinic Heart Hospital in Pretoria. 

Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela amerudi nyumbani baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini mjini Pretoria.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na serikali ya nchi hiyo, hali ya Mandela imeelezwa kuimarika ingawa bado ni tete. Atapatiwa huduma na uangalizi maalumu akiwa nyumbani kwake.

"Hali ya Madiba bado ni tete na wakati mwingine hudorora. Lakini, timu ya madaktari wake wameshawishika kuwa ataweza kupokea matibabu yale yale akiwa nyumbani kwake,” ilisema taarifa ya ikulu ya nchi hiyo.

Shujaa huyo wa Afrika alipelekwa hospitali tarehe 8 Juni kutokana na maambukizi katika mapafu. Tatizo hilo alilipata alipokaa gerezani kwa kipindi cha miaka 27 katika zama za utawala wa makaburu.

Mnamo Julai 18, watu wa Afrika Kusini walisherehekea siku ya kuzaliwa kwa Mandela kwa kufanya kazi za hisani, huku watu wengi wakijitolea dakika 67  za kutoa huduma za kijamii kwa heshima ya miaka 67 ya mapambano ya Mandela katika kutetea haki za binadamu na uadilifu wa kijamii.

Mandela, aliyeiongoza nchi yake kwenye demokrasia mwaka 1994, aliondoka madarakani mwaka 1999 baada ya kutumikia kipindi cha muhula mmoja kama rais wa Afrika Kusini.  Kiongozi huyo alistaafu kabisa kazi za umma mwaka 2004, lakini akaendelea kuonekana katika baadhi ya matukio ya kijamii.



Mandela amepata zaidi ya tuzo 250 kwa kipindi cha miongo minne, ikiwa ni pamoja na Tuzo ya Amani ya Nobel aliyoipata mwaka 1993.
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment