WAZIRI Mkuu wa Australia, Kevin Rudd, amekiri kushindwa katika uchaguzi wa shirikisho na hivyo kumtengenezea njia kiongozi mwenye mrengo wa kihafidhina, Tony Abbott, kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo.
Akizungunza mbele ya wafuasi wake mjini Brisbane, Rudd alikubali na kutangaza kuwa hatagombea tena uongozi wa chama chake cha Labor.
"Ninaweza kuwataarifu kuwa serikali ya Australia imebadilika," Rudd aliwaambia wafuasi wake.
Hata hivyo, Rudd aliongeza kuwa anajivunia kukisaidia chama chake kuendelea kuwa mshindani katika siasa za nchi hiyo.
Kauli yake inakuja baada ya wapiga kura kuiadhibu serikali ya chama cha Labor kwa kuupa kura mgombea wa muungano wa vyama vya kihafidhina katika uchaguzi wa bunge.
Wananchi wengi wa Australia wanaituhumu serikali ya chama cha Labor, ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka 2007, kwamba kimeshindwa kutatua kero zao na utawala wake wa miaka 6 ulijaa misukosuko.
Katika uchaguzi huo, masuala ya uchumi, nakisi ya bajeti na suala la wanaotafuta hifadhi ya ukimbizi, ndiyo yaliyoziteka kampeni za uchaguzi huo.

0 comments:
Post a Comment