SHEIKH PONDA: SIJUTII





SHEIKH Ponda Issa Ponda, Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, amesema hawezi kujutia harakati zake za kudai haki za Waislamu nchini licha ya misukosuko anayoipata kwa sasa. Anasema ikibidi yupo tayari kupoteza uhai wake.

Anasema, katika harakati zake kamwe hatachonganisha wananchi wa taifa moja isipokuwa hayupo tayari kusimamia dhulma kwa kundi moja dhidi ya jingine kama inavyofanyika sasa.

Mwandishi wa habari hizi alifanikiwa kuzungumza na Sheikh Ponda kwa muda mfupi akiwa kitandani kwenye Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MOI) baada ya kupenza kama mmoja wa wanandugu wa karibu wa kiongozi huyo.

“Natambua kwamba wapo wanaokerwa na harakati hizi, natambua wapo wanaojali harakati hizi bila kujali imani zao iwe ndani ya serikali ama nje ya serikali.

“Lakini kukwepa kusema ukweli ni kuahirisha vurugu nchini, nisiposema mimi wapo watakaosema kwa sauti kali kuliko yangu na wanaweza kuwa hatari (kama wanavyoniita) zaidi yangu tofauti na serikali inavyonitazama mimi, na hapo wajukuu zangu wataishi kwa wasiwasi zaidi,” Sheikh Ponda alimweleza mwandishi.

Mwandishi alimhakikishia taarifa za polisi zinaeleza kwamba Jeshi hilo halihusiki na kumpiga risasi huku wakikiri kufyatua risasi “lakini mdomo wa bunduki ulielekezwa juu ili kutawanya watu na si kwa mtu yeyote aliyekuwa eneo la tukio.”

“Mimi nilikuwa na akili timamu, nilikuwa na fahamu timamu. Nilipigwa risasi na polisi na itabaki kuwa hivyo. Unaweza kutumia akili ndogo kukubaliana na hilo la polisi kwani inawezekanaje risasi ipigwe hewani iingilie mbele ya bega langu?” alihoji.

Jeshi la Polisi juzi kupitia kwa msemaji wake, Avera Senso, lilieleza kuwa, “baada ya askari kutaka kumkamata, wafuasi wake walizuia ukamataji huo kwa kuwarushia mawe askari polisi, kufuatia purukushani hizo askari walipiga risasi hewani kama onyo la kuwatawanya.”

Aisha Issa Ponda ni mtoto wa Sheikh Ponda aliyeliambia FAHAMU kwamba mazingira ya baba yake pale alipo bado yanatia shaka kw akuwa “kuna sura mbalimbali zinajitokea kwenda kumtazama.”

“Nilikwenda jana na sasa hivi mume wangu (Mwinyikombo Ayubu) ndio yupo pale kwa kuwa watu wengi wamekuwa wanakwenda na mazingira kwa sasa hayaonekani kuwa rafiki,” alisema Aisha akionesha kuhofia usalama wa baba yake.

Sley Issa Ponda, kaka wa Sheikh Ponda, anayeishi Kigoma alisema mazingira ya Sheikh Ponda kusakamwa yanatokana na serikali kutotaka kuutambua ukweli.

“Haya yote yanatokana na msingi wa dhulma nchini. Haya yanatokana na dhulma iliyokomaa nchini na ndio maana Chadema, CUF, TLP, NCCR-Mageuzi na vyama vingine ambapo vinaposema ukweli, serikali inawafuatafuata na kuwatisha.

“Mfumo huu si kwa Sheikh Ponda pekee, mtu yeyote atakayeiambia serikali hili sio sawasawa, kuanzia hapo anakuwa adui mkubwa. Mara ngapi viongozi wa siasa wanatiwa ndani na kisha wanaachwa. Huu ni mfumo wa CCM na hauwezi kukoma,” alisema.

Sley alieleza matukio hatari yaliyomkumba mdogo wake ikiwa ni pamoja na sakata la Mwembechai wakati wa utawala wa Benjamin Mkapa na kusababisha kuondoka Dar es Salaam kutokana na serikali kumsaka.

Tukio la pili ni la kupigwa risasi akiwa kwenye meli. “Ponda baada ya sakata la Mwembechai alikuja hapa (Kigoma), akaenda alikozaliwa mama yake Wilaya ya Nkasi na kisha akaenda Burundi.

“Alipokuwa akitoka Burundi, meli aliyopanda ilivamiwa na waasi na ndipo alipopigwa risasi na kuumizwa mguu wake. Alipofika bandarini tu na kuangaliwa pasipoti yake.
“Walipobaini ni yeye, polisi walimfuata na kumchukua kisha wakampeleka Maweni (Hospitali ya Mkoa wa Kigoma) na hapo niliitwa kwenda kuthibitisha kama ndio Ponda kweli.

“Baada ya kumpa matibabu polisi walimvisha kitambaa usoni na kumtowesha mkoa wa Kigoma kumpeleka Mwanza na kumsafirisha mpaka Dar es Salaam,” alisema Sley.

Sley alitaja tukio la tatu alilosema lilitikisa familia yao kuwa la kukamatwa na kuwekwa korokoroni kwa miezo saba huku akinyimwa haki yake ya dhamana.

“Tukio la mwisho ni hili la kupigwa risasi Morogoro. Sisi tunaamini kwamba hakuna kisichokuwa na mwisho. Ponda nchi hii inamhusu na hapa ndio kwao na atazikwa hapa. Tunasubiri mwisho ufike tumzike,” alisema.



Amiri wa Shura ya Maimamu nchini, Alhaji Mussa Kundecha jana aliliambia FAHAMU kwamba, busara kwa serikali imekwisha, sasa taifa linaelekea kusikojulikana.

“Kukaa kimya hakuna maana kwamba tumedhibitiwa, kama wapiga risasi watakuwa wanaamini hivyo watakuwa wanajidanganya. Tunachunga ndimi zetu kwa kuwa madhara ni makubwa, nyoyo za watu zina madonda na tukiyatonesha risasi hazitatosha,” alisema.

Wakati hayo yakiendelea, Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba ambaye alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufika Muhimbili kuwangalia Sheikh Ponda mara tu alipofikishwa na kulazwa, alisema kutunza amani ya nchi kunahitaji umakini wa hali ya juu.

Prof. Lipumba alisema, Serikali kudharau ama kuamini kwamba kundi fulani lina haki na jingine halina, mwisho wake ni kutengeneza mgogoro ambao athari zake zinashuka kwa makundi yote.

“Serikali kama imesema tumechoka, basi wananchi ndio waliochoka zaidi, sasa serikali imechoka, inatandika risasi hovyo. Je wananchi wakianza kutekeleza uchovu wao kwa serikali inakuwaje?” alihoji.

Alishangaa serikali inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete kwa kushindwa kukemea uovu huku Waziri wa Mambo ya ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi na IGP Said Mwema wakitaka kujisafisha mbele ya jamii.

Kutokana na sakata hilo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro, ameiambia fahamu kwamba, Watanzania hawapaswi kuchekelea hatua za mabavu za Jeshi la Polisi kwa raia wake.

“Ikiwa viongozi tutachekelea unyama huu na kuacha fulani atambuliwa kama ‘mtu hatari sana’ eti kwa sababu tu yeye ni wa dini fulani, ni kweli mhusika atashughulikiwa ipasavyo, atateswa tutachekelea, ataumizwa tutachekelea na atauawa tutapiga nderemo na vifijo,” alindika Mtatiro kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Godbless Lema, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema) aliliambia FAHAMU kwamba tukio hilo la kupigwa risasi Sheikh Ponda ni matokeo ya kauli ya Waziri Mkuu Pinda ndani ya Bunge pale aliposema ‘wapigeni tu, tumechoka.”

Lema alisema, hata jambazi hatakiwi kukamatwa kwa kupigwa risasi ndio akamatwe labda akiwa na silaha za moto, ambazo anaweza kuanza kuzitumia kupambana na wanaomkamata.

“Siku za hivi karibuni alipokuwa Zanzibar na ndipo walipoamuru akamatwe. Je, tujiulize kutoka Zanzibar hadi Morogoro alitumia usafiri gani hata wakashindwa kumkamata kwa utaratibu unaoeleweka?

“Nakumbuka Mchungaji mmoja Israel alipata kusema kuwa ukiona mtu anafanyiwa dhulma na wewe ukakaa kimya, iko siku utafanyiwa wewe. Leo ni kwa Ponda, kesho ni kwa Lema, Mbowe, Lipumba na hata wewe mwandishi,” alisema.

Alisema kelele nyingi zinapigwa na Chadema zikiashiria kutaka haki za kibinadamu na si uchochezi, na hata nachokifanya Sheikh Ponda ni kutafuta haki na usawa kwa jamii ya wale anaowaongoza na siyo kuchochea vurugu kama inavyodaiwa na serikali ya CCM.
“Nasema Ponda akiuliwa, Lema akiuawa, Mbowe akiuliwa, Lipumba akiuliwa, sio mwisho wa harakati, “ alisema.

Kutokana na tukio la Sheikh Ponda, Mashirika ya Uteteziw a Haki za Binadamu – THIRD-Coalition, LHRC, SIKIKA, TGNP, CPW na TAMWA yametoa taarifa ya pamoja kwa kusikitishwa na hali ya uvunjaji wa haki za binadamu inayotokana na yabia ya vyombo vya dola kutumia nguvu inayokiuka haki za msingi za wananchi.

“Tunalaani kabisa utaratibu ambao Jeshi la Polisi lilitumia ili kumkamata Sheikh Ponda, utaratibu huu wa kumkamata mtuhumiwa mbele ya halaiki ya wafuasi wake ulikuwa hatarishi kwa maisha ya askari wenyewe pamoja na maisha ya raia na pia ilikuwa inaibua hamasa ya hamaki ya umma. Ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kaimu Mufti wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Alhadi Mussa Salum ameunga mkono kauli ya Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania kuitaka serikali kuchunguza kwa kina tukio lililopelekea kupigwa risasi kwa Sheikh Ponda.
“Serikali ilikuwa na nafasi ya kumkamata Sheikh Ponda kwa kufuata mkondo wa sheria, tofauti na hali ambao imejitokeza sasa,” alisema.



HALI ILIVYOKUWA

Agosti 10 mwaka huu, Sheikh Ponda alialikwa na Waislamu wa Morogoro kuhudhuria sherehe za Sikukuu Ya Eid ya Pili. Sheikh Ponda, Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu alialikwa na viongozi wa Jumuiya ya Wahadhiri wa Kiislamu Mkoa wa Morogoro kuhudhuria kongamano walilloliandaa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro (RPC) aliruhusu kongamano hilo ambapo Sheikh Ponda aliingia uwanjani saa 11:30 na kupanda jukwaani.

Alizungumza kwa muda mfupi na baadae kushuka na kuingia kwenye gari dogo huku akiwa anasindikizwa na Waislamu wakitembea kwa miguu kuelekea Msikiti wa Dini Moja Mungu Mmmoja kwa ajili ya swala ya Magharibi.

Kiwanjani palikuwa na Landrover nne za jeshi la polisi ambazo zilianza kuwafuata na baadaye askari walipiga mabomu ya machozi kuwatawanya waumini hao.
Baada ya hapo, Waislamu walisambaratika na kumuacha Sheikh Ponda akiwa na watu watano tu, ndipo ilipotokea Landrover nyingine ya polisi mbele ya gari aliyokuwa amependa Sheikh Ponda.

Baada ya kuona hivyo, Sheikh Ponda akashuka kwenye gari akiwa na watu wachache waliosimama ubavuni mwa gari yake. Alipoteremka tu kwenye gari, akajikuta amezungukwa na askari kwa umbali wa mita chache na kufyatuliwa risasi iliyompiga bega la kulia na kutokea upande wa pili.

Sheikh Ponda alipelekwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ambako hakupata huduma kwa sababu hakuwa na PF3 na polisi walikuwa wanamtafuta kwa nia ya kumkamata na kumaliza kazi yao na siyo kumtibu.

Baadaye alipelekwa Hospitali ya Kiislamu iliyopo Msamvu ambako alipata huduma ya kwanza na baadaye kusafirishwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako anaendelea kutibiwa akiwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi.




Wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Eliezer Feleshi alitangaza kwenye vyombo vya habari kuwa polisi wamkamate Sheikh Ponda kwa kufanya kosa linalohusu hukumu aliyopewa na Mahakama ya kifungo cha nje.
DPP Feleshi alisema atapelekwa mahakamani kwa kuvunja sheria.
Tamko lake lilikuja siku mbili tu baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia kwa Makamu wa Pili wa Rais, balozi Seif Ali Iddi, kutangaza kuwa Sheikh Ponda alifanya uchochezi wa vurugu alipokuwa ziarani Zanzibar ambako alihutubia kwenye misikiti mitatu.
Balozi Seif alisema, Sheikh Ponda katika hotuba zake alijiegemeza katika siasa, vurugu na chuki za kisiasa na kutaka wananchi wasisikilize kanda zake.

Lakini akiwa kwenye Msikiti wa Mtambani, Kinondoni jijini Dar es Salaam, wiki mbili zilizopita, Sheikh Ponda aliwaambia waumini wa Kiislamu kwamba aliisema serikali ya Zanzibar pamoja na viongozi wake wakuu kwamba wamevunja sheria kuendele kuwashikilia masheikh kadhaa wa Kiislamu bila ya kuwahukumu mahakamani.

Alisema viongozi hao wanathubutu kufunga dhamana ya masheikh hao japokuwa sheria waliyoshitakiwa inaruhusu dhamana kutolewa na mahakama. Dhamana ya watuhumiwa hao imefungwa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka wa Zanzibar, Ibrahim Mzee.

Masheikh tisa, akiwemo kiongozi wao, Amiri Farid Hadi Ahmed, walikamatwa Oktoba 16 mwaka jana na kupelekwa mahakamani kwa tuhuma za kufanya uchochezi wa vurugu na mpaka leo kesi yao haijaanza kusikilizwa.

CHANZO: Fahamu
  

Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment