![]() |
| Baraza jipya la mawaziri baada ya kuapishwa |
Na Kabuga Kanyegeri
Wale waliojitwalia madaraka nchini Misri yumkini walilazimisha mapinduzi bila kuwa na mipango na mikakati ya jinsi ambavyo wangeitawala nchi baadaye.
Kuna mantiki gani kumuweka kizuizini kwa siku 15 rais aliyeuzuliwa Muhammad Mursi? Kama ana hatia ya kutenda jambo fulani, kumuweka siku 15 kizuizini itakuwa sawa adhabu ya kosa la kusababisha ajali barabarani. Kama hana kosa, basi yumkini mtawala mpya, Jenerali Abdulfattah al-Sisi, alidhani kuwa anahitaji siku 15 tu kukamilisha mpango fulani alionao kichwani mwake.
Wakati wafuasi wa chama cha Udugu wa Kiislamu wakikusanyika katika viwanja mbalimbali, al-Sisi aliwatolea wito wale wanaomuunga mkono nao wamiminike mitaani. Kwa hali hiyo, makundi mawili yanayopingana yameendelea kujazana kwa wingi katika medani mbali mbali. Upande mmoja kuna wale wanaokiunga mkono chama cha Udugu wa Kiislamu na ambao wanataka Mursi arejeshwe mamlakani; na upande mwingine kuwa wale wanaotaka serikali isiyoegemeza mambo yake kwenye sera za Kiislamu.
Al-Sisi anatambua fika kiwango cha mvutano ulioitamalaki Misri, sasa kwa nini aliwataka wale wanaomuunga mkono kumiminika barabarani? Labda alitaka kuzusha mapigano na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe. Vita ikitokea, jeshi litalazimika kuchukua hatua kali, kutangaza vita au kuweka marufuku ya kutotembea na kutumia mwanya huo kuwakamata au kuwaua wale wanaolipinga. Lakini, mambo ni mazito na si rahisi kutokea kwa hali hiyo nchini Misri. Kwa nini nasema hivyo?
Kwanza kabisa, kuna watu wengi mitaani ambao marufuku ya kutotembea haitawafanya warejee majumbani. Kwa maneno mengine, jeshi halina uwezo wa kumlazimisha kila mtu. Aidha, inaonekana sio rahisi kwa jeshi kuwaita washirika wake wa nje kuja kuwasaidia kutuliza vurugu na ghasia.
Tatizo la pili ni kwamba wafuasi na wapinzani wa Mursi hawana mpango wa kuuana. Kwa maneno mengine, tushukuru Mungu kuwa ndani ya makundi hayo mawili kuna watu wenye busara, angalau kwa sasa, ambao wasingependa kukatana mashing yao. Labda ndiyo maana jeshi liliamua kumwaga damu za watu wake wenyewe na kuwaua, kwa sababu watu hao hawataki na hawana mpango wa kuuana.
Jeshi linaloua watu wake lenyewe linatarajia kupata faida gani ya kisiasa? Radiamali ya jeshi ya kumwaga damu ya wananchi wake imewaweka katika hali ngumu sana wale wanaoliunga mkono.
Mauaji hayawezi kusaidia lolote zaidi ya kuzidisha chuki, huzuni na kuibua hali ya visasi. Iwapo Misri itaamua kufanya uchaguzi huru na wa haki hivi karibuni, kipindi cha kampeni za uchaguzi yumkini nacho kikashuhudia umwagaji wa damu. Mivutano ikiongezeka, huwa ni ngumu kupata suluhu ya kisiasa. Yatakapoibuka machafuko hakuna atakayeweza kuandaa uchaguzi huru na wa haki wala kudhibiti hali ya usalama nchi nzima. Hivyo, kuna hatari ya kweli ya Misri kugeuka kuwa nchi isiyotawalika.
Hata hivyo, Misri sio nchi ya kawaida: mfumo wa kimataifa hauwezi kuruhusu nchi hii iendelee kuwa katika ghasia na machafuko yasiyokuwa na kikomo. Yumkini ‘wakubwa’ wa dunia wakajaribu kumtafuta mtu kama Rais wa Afghanistan Hamid Karzai kutuliza hali ya mambo; au huwenda wakajaribu kuidhibiti nchi kwa njia ya moja kwa moja ikifuatiwa na uingiliaji kati wa kijeshi (kwa malengo ya kibinaadamu, kwa mfano) kama walivyofanya Libya.
Vyovyote itakavyokuwa, mazungumzo baina ya Waisrael na Wapalestina yameanza upya. Huwenda ndani ya siku 15 zijazo, katika kipindi ambacho Mursi atakuwa kizuizini, huwenda mpango wa ramani kuelekea kwenye amani kwa ajili ya mazungumzo hayo ukawa umeshaandaliwa. Iwapo mambo hayatakuwa kama ilivyopangwa katika mazungumzo haya, kuna uwezekano wakatengeneza mashitaka mapya dhidi ya Mursi ili kumfunga na hivyo kuendelea kukaa gerezani.
Inaonekana kuwa makundi yote ya jamii ya Misri yanatambua uwezekano wa kutokea kwa mambo yote hayo. Hata hivyo, siku zote mapambano ya wananchi na maslahi ya watawala ni vitu ambavyo huwa vinapingana. Mara nyingi, watawala hutuliza mambo kwa kutumia jeshi ili kutotekelea matakwa ya wananchi.
Ngoja tusubiri na tuone mwisho wa hali hii…

0 comments:
Post a Comment