Sheikh Ponda asakwa Zanzibar kwa tuhuma za uchochezi

Wakati Katibu wa Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda, akiwa kwenye kifungo cha mwaka mmoja nje, Jeshi la Polisi Zanzibar limetangaza kumtafuta kiongozi huyo kwa tuhuma za uchochezi.

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alitangaza jana kwamba kitengo cha upelelezi kinamsaka Sheikh Ponda kwa kuendesha mihadhara ya uchochezi inayoweza kuhatarisha amani na mshikamano kwa wananchi Visiwani humu.

“Tumenaza kumtafuta Sheikh Ponda, kutokana na vitendo vya uchochezi alivyovifanya kupitia mihadhara yake akiwa Zanzibar,” alisema Kamishana Mussa.

Kamishana Mussa aliwataka wananchi wa Zanzibar kuendelea kudumisha amani na misingi ya umoja wa kitaifa kwa kujiepusha na watu wanaotaka kutumia majukwaa ya dini kufanya kazi za kiharakati na siasa.

Awali, akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa Kamati Maalum ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM) Zanzibar Idara ya Itikadi na Uenezi, Waride Bakari Jabu, aliivitaka vyombo vya ulinzi na usalama nchini kumchukulia hatua za kisheria Ponda kufuatia kauli alizozitoa za kuwataka wananchi waingie barabarai na kufanya fujo kama zinazotokea nchini Misri.

Waride alisema Sheikh Ponda alikuwa akitoa kauli hizo kupitia nyumba za ibada ikiwamo misikiti ya Mbuyuni, Kwarara na Nungwi,  kauli ambazo alidai zinapandikiza chuki, kuondoa upendo, kuhatarisha amani na kuchochea umwagaji damu.

Msako wa Sheikh Ponda umekuja Zanzibar huku akiwa anatumikia adhabu ya kifungo cha nje cha mwaka mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kusababisha uharibifu wa mali na uchochezi mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment