
Kabuga Kanyegeri
Ukiwa mfuatiliaji wa masuala ya Mashariki ya Kati utabaini kuwa sio tu kwamba mipaka ya kisiasa ya nchi za eneo hilo ni zao la zama za ukoloni, bali pia uamuzi na maagizo ya kisiasa ya eneo hilo yanatoka kwa wakoloni.
Ramani ya eneo hilo ambayo majeshi ya nchi washirika katika vita vya dunia walikubaliana na Uingereza kuitambua mwezi Mei 1916 ndio ramani inayotumiwa leo na mataifa yaliyokoloniwa. Sio tu nchi na mipaka yake, bali pia tawala za kifalme zinazotawala nchi hizi, isipokuwa baadhi, ziliainishwa na kuamuliwa na makubaliano ya washirika hao. Falme za Ghuba zilitengenezwa na wakoloni badala ya wananchi wa Arabia, na zilitengenezwa kwa lengo la kulinda maeneo yenye mafuta katika nchi hizo.
Nguzo kuu iliyofanikisha kutambuliwa kwa mipaka hii iliyochorwa na kuainishwa kwenye meza hiyo ya makubaliano ni maasi ya Waarabu ya tarehe 10 Juni, mwaka 1916, muda mfupi tu baada ya mkataba maarufu unaojulikana kama Makubaliano ya Sykes-Picot. Katika maasi haya, makabila kadhaa ya Kiarabu yalifanya uasi dhidi ya serikali kuu ya Dola ya Uthamaniya. Familia zilizoongoza maasi hayo na kushirikiana na Waingereza ndizo zinazotawala sasa hivi. Waingereza waliwateua wale walioshirikiana nao kuwa viongozi wa himaya ndogondogo walizozitengeneza.
Jambo hili lilisababisha kuibuka kwa dola zilizoshabihiana na makampuni binafsi ya biashara yanayomilikiwa na familia fulani fulani. Waingereza walianza kumbadilisha mshirika wao mkubwa, Sharif Hussein, wakaiweka familia ya Saudi na kulidhibiti eneo lote la Mashariki ya Kati chini ya kanuni ya “wagawe uwatawali”. Unaweza kuona mafanikio ya mantiki na kanuni hii kwa kuangalia tu kile kilichotokea miongo miwili iliyopita nchini Kuwait pekee. Saddam alijaribu kufanya mabadiliko kidogo kwenye ramani hiyo, jambo lililosababisha kutokea kwa vita ya kwanza na ya pili katika eneo la Ghuba.
Kadhia ya Palestina ni zao la mipango hiyo iliyobuniwa na kusukwa katika zama za ukoloni. Jeshi la Uingereza, kwa msaada waasi wa Kiarabu, waliliondosha jeshi la Waturuki kutoka Palestina na kuuharibu vibaya sana ushawishi na nguvu ya ulimwengu wa Kiislamu kwenye eneo la Quds au Jerusalem. Hatua iliyofuata ilikuwa ni utawala wa Israeli na kadhia ya Palestina vilivyotengenezwa na tangazo au azimio maarufu linalojulikana kama Azimio la Balfour. Kabla ya Palestina kuwekw chini ya udhibiti wa Waingereza, azimio hili lilielezea uundwaji wa taifa la Kiyahudi. Katika miongozo hii hapakuwa na nafasi ya wananchi wa Mashariki ya Kati wala wawakilishi wao. Kwa kipindi chote cha karne moja sasa, watu na jamii za Kiislamu wamekuwa mateka wa mustakbali uliotengenezwa na watu wa nje. Kwa kweli chanzo cha yale yanayotokea sasa ni mataifa ya Magharibi yaliyotengeneza na kuuimarisha mfumo huu. Tunachokishuhudia leo ni kwamba mfumo huu sio imara tena. Tawala za kifalme serikali vibaraka haziwezi kuendeleza utawala wao.
Mfumo uliotengenezwa na wakoloni mwaka 1916 sasa unaporomoka. Sababu ya Saudi Arabia na tawala nyingine za Ghuba kuunga mkono mauaji yanayoendelea nchini Misri ni katika juhudi zao za kutaka kuzuia anguko hili. Wataalamu mbalimbali wa Kimarekani walitabiri kuwa utawala wa familia ya al-Saudi hauna muda mrefu tena wa kuendelea kutawala. Vuguvugu la Arabia ni nguvu thakili inayotaka kuuondosha mfumo huu katika jieografia ya Mashariki ya Kati. Demokrasia ikiimarika nchini Misri, utawala wa kifalme hauwezi kuendelea kuwepo nchini Saudi Arabia. Wale waliotengeneza mapinduzi ya kijeshi nchini Misri wana silaha na utawala wa Saudi Arabia unatoa fedha za mafuta ili kuhakikisha mfumo huo unaendelea kuwepo. Wote wanaungana na kufanya mauaji. Nchi za Magharibi zinauunga mkono ushirikiano huu ili kuendeleza uhusiano wao na tawala dhaifu.
Lakini wataendelea kufanya hivyo mpaka lini? Je, yawezekana kuendelea kuwakandamiza watu? Haiwezekani kuendelea kukandamizi utashi wa watu kwa lengo la kuendelea kuulinda utawala wa kidikteta wa watu wachache kwa sababu ya upinzani mkubwa katika zama hizi za utandawazi. Medani za maandamano nchini Misri zinatuambia kuwa hili haliwezekani kutokea tena.
Mabadiliko kuelekea kwenye demokrasia ni jambo lisiloepukika. Wale waliotengeneza mfumo wa tawala hizi karne moja iliyopita wataungana na mabadiliko haya au watu watauondosha mfumo huu, hata kama itawagharimu damu na uhai wao.
0 comments:
Post a Comment