ERDOĞAN: HISTORIA ITAWALAANI MASHEIKH KAMA HAWA

Erdoğan says history will curse Al-Azhar Sheikh for endorsing coup
Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdoğan akizungumza kwenye chuo kikuu kimoja mjini Rize kilichopewa jina lake hapo jana Jumapili. 



WAZIRI Mkuu wa Uturuki, amemlipua kiongozi mkuu wa Kiislamu nchini Misri kwa kuunga mkono mapinduzi yaliyofanywa na jeshi nchini humo, akisema kuwa historia itawalaani wanazuoni mfano wake.

Ahmed al-Tayeb, Sheikh Mkuu wa Al-Azhar, aliunga mkono mpango wa kisiasa ulioshinikizwa na jeshi Julai 3 na kumuondoa madarakani Rais wa zamani Muhammad Mursi, kusitisha matumizi ya katiba na kuitisha uchaguzi wa mapema wa urais na bunge.

Kiongozi huyo wa kitovu maarufu na kikongwe cha taalumu za Kiislamu duniani alitoa taarifa iliyounga mkono mapinduzi ya kijeshi, kufuatia tangazo lililotolewa na mkuu wa jeshi la nchi hiyo la kumuondoa rais aliyechaguliwa na wananchi. 

Akizungumza kwenye chuo kikuu kilichopewa jina lake mjini Rize, Recep Tayyip Erdoğan alisema kuwa mwanazuoni ni yule asiyethubutu kuiuza heshima yake kwa hali yoyote ile, akionekana kumlenga Sheikh wa Al-Azhar. Alisema kuwa iwapo mwanazuoni ataambiwa na mwanasiasa kama yeye jambo ambalo si la haki, basi mwanazuoni huyo anatakiwa kulikataa.

Erdoğan alisema kukaa kimya mbele ya matukio yanayotokea nchini Misri ni sawa na kubeba mzigo wenye miba. Aliwalalamikia wasomi na vyuo vikuu kwa kushindwa kutoa sauti ya upinzani dhidi ya mapinduzi ya kijeshi nchini Misri, licha ya kwamba walitegemewa kufanya hivyo, huku akitolea mfano wa Sheikh wa Al-Azhar aliyeunga mkono na kuyaridhia mapinduzi yaliyofanywa na jeshi la Misri.

Erdoğan anasema alishtuka alipomuona Sheikh wa Al-Azhar akiunga mkono kilichofanywa na jeshi. “Unawezaze kufanya hivyo?” alihoji. Huyo mwanazuoni [Sheikh wa Al Azhar] amekwisha. Historia itawalaani watu wa aina yake kama ilivyowalaani wanazuoni kama hao hapo zamani hapa Uturuki.”

Aidha, Erdoğan aliyakosoa mataifa ya Magharibi kwa kushindwa kuuambia utawala unaoungwa mkono na jeshi: “acha” na kuwaua au kuwajeruhi watu 6,000 mpaka sasa tangu mapinduzi hayo yalipotokea. “Je, mapinduzi ya kijeshi yanaweza kuitwa kuwa ni demokrasia?”  alihoji kwa dhihaka akiwakosoa wale wanaolitetea jeshi kwamba linarejesha demokrasia. Akasema kuwa wale wanaonyamazia yale yanayotendeka nchini Misri, kesho hawatakuwa na haki ya kuuzungumzia udhalimu.

Kiongozi huyo, vilevile, aliwashutumu vikali wale waliomkosoa Mursi kwamba alifanya makosa wakati wa uongozi wake uliodumu kwa mwaka mmoja. Alisema kuwa ndani na nje ya Uturuki kuna wale “wanaojiliwaza” kwa kusema kuwa licha ya jeshi, lakini Mursi naye alifanya makosa.

“Nchi imetawaliwa kwa udikteta kwa miaka 70. Mliweza kulivumia hili, lakini mkashindwa kuvumilia utawala wa mwaka mmoja wa Mursi aliyechaguliwa kidemokrasia,” alisema  Erdoğan, akiwakusudia waandamanaji wanaompinga Mursi walioandamana katika Medani ya Tahrir na kupelekea Mursi kuondolewa madarakani.

Aliendelea kubainisha kuwa sio sahihi kusema kwamba Mursi alifanya makosa yanayohalalisha mapinduzi ya kijeshi na kwamba sio sahihi kabisa kuyazungumzia makosa ya rais aliyeondolewa madarakani ilhali mamia ya raia wanauawa “kushoto na kulia” nchini Misri.

Alizungumzia kwa urefu kuhusu sanduku la kura na uchaguzi na kusema kwamba haelewi kwa nini wale waliounga mkono mapinduzi ya kijeshi hawakuweza kusubiri miaka mitatu zaidi ambapo Mursi angekuwa amemaliza muhula wa utawala wake. Alisema kuwa viongozi waliochaguliwa kidemokrasia wanapofanya makosa wanapaswa kuondolewa kwa kura.

Kwa mara ya tutu, Erdoğan alirejelea msimamo wake wa kuikosoa Israeli kwamba ilikuwa nyuma ya mapinduzi ya Misri, akibainisha kuwa Israeli inaendesha kampeni ya kuushusha umuhimu wa chaguzi. Maelezo yake yalijikita katika kile kilichosemwa na mwanazuoni wa Kifaransa mwenye asili ya Kiyahudi katika madahalo mmoja tarehe 3 Februari kuwa Chama cha Muslim Brotherhood hakiwezi kukaa madarakani hata kama kitachaguliwa na wananchi.

Erdoğan alielekeza lawama zake pia kwa jeshi la Misri kwa unyama wa kuwakandamiza waandamanaji wanaomuunga mkono Mursi. Alisema kuwa waandamanaji hawana silaha wala mabomu ya petroli bali wanasimama mbele ya vifaru kulinda heshima na utu wao. “Unaweza kutosema kuwa haya ni mapinduzi?” alisema akizinyooshea kidole nchi za Magharibi.

“Ninalitolea wito jeshi la Misri. Ninawauliza hivi: Mnawajua hao mnaowaua? Je, mnapigana na wavamizi  wa nchi yenu au mnawapiga risasi ndugu zenu watakaopiga kura?” alisema.

Mbali na matukio ya Misri, Erdogan aliwakosoa wapinzani wa nchini mwake kwa kumuita “dikteta”, akisema kuwa wasingeweza kumuita hivyo kama kweli wangekuwa wanatawaliwa na dikteta. 

“Wale waliomnyonga Waziri Mkuu wa zamani Adnan Menderes walimuita dikteta. Sasa hivi wananiita dikteta,” alisema Erdoğan. “Kama mnataka kumuona dikteta nendeni Syria na Misri. Huko watawanyonga,” alisema.
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment