![]() |
Wafuasi wa Muhammad Mursi wakiandamana katika mji wa bandari wa Alexandria, Julai 26, 2013. |
Duru kutoka hospitali nchini Misri zinasema kuwa watu wasiopungua 120 wameuawa na wengine zaidi ya 4500 kujeruhiwa katika ghasia zilizotokea wakati wa maandamano ya makundi mawili hasimu ya wafuasi na wapinzani wa Rais aliyeouzuliwa, Muhammad Mursi nchini kote.
Ghasia hizo ziliibuka baada ya wafuasi wa Mursi kukusanyika katika wilaya ya Nasr jana Ijumaa, wakitaka kiongozi huyo arejeshwe madarakani.
Maandamano makubwa yalifanyika katika kuitikia wito wa chama cha Udugu wa Kiislamu wa "mshikamani wa amani" dhidi ya "mapinduzi" ya jeshi yaliyomuondoa Mursi madarakani. Katika taarifa iliyotolewa siku ya Alhamisi, kiongozi wa chama hicho, Muhammad Badie, aliwataka Wamisri kuandamana kwa ajili ya kutetea uhuru na uhalali wa urais wa Mursi.
Wakati huo huo, jeshi la Misri linasemekana kutumia risasi za moto dhidi ya waandmanaji wanaopinga hatua ya jeshi hilo kumuuzulu Mursi.
Ghasia katika mji wa bandari wa Alexandria zilisababisha watu saba kupoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Chama cha Udugu wa Kiislamu kinasema kuwa watu wasiopungua 31 wameuawa usiku wa kuamkia leo baada ya vikosi vya uslama kuwashambulia wafuasi wa Mursi mjini Cairo.
“Hawatufatulii risasi ili kutujeruhi, wanatufyatulia risasi ili kutuua," alieleza msemaji wa chama hicho Gehad El-Haddad na kuongeza kuwa waandamanaji wapigwa risasi za moto kichwani na kifuani.
Aidha, waandamanaji wanaompinga Mursi walikusanyika katika medani maarufu mjini Cairo ya Tahrir na jirani na ikulu ya rais.
Waziri wa mambo ya ndani wa serikali ya mpito, Muhammad Ibrahim alitishia kuyasambaratisha maandamano ya wafuasi wa Mursi na kwamba maandamano hayo "yatakomeshwa hivi punde na kwa njia halali."
Mkuu wa majeshi, Jenerali Abdul-Fattah al-Sisi, naye aliitisha maandamano ya nchi nzima siku ya Ijumaa. Katika hotuba yake wakati wa mahafali ya chuo cha kijeshi mjini Cairo, alisema kuwa maandamano hayo yatalipatia jeshi nguvu na mamlaka ya kupambana na kile alichokiita kuwa ni "fujo na ugaidi" vilivyouikumba Misri baada ya kung'olewa kwa Mursi hapo Julai 3.
Mapema Ijumaa, vyombo vya habari vya serikali viliripoti kuwa Mursi amewekwa kizuizini ambapo waendesha mashitaka wanachunguza tuhuma za kwamba "alikula njama" na kundi la Kipalestina la Hamas kufanya mashambulizi na kutoroka gerezani wakati wa mapinduzi ya mwaka 2011 yaliyomng'oa madarakani Husni Mubarak.
Hata hivyo, El-Haddad alizipuuza tuhuma hizo na kuziita kuwa ni "upuuzi," na kusema kuwa yote hayo ni ishara ya kurejea kwa "utawala wa zamani" wa Mubarak.
Ripoti zinasema kuwa makabiliano baina ya wafuasi na wapinzani wa Mursi yanaendelea kupamba moto na kusababisha maafa makubwa.
0 comments:
Post a Comment