SERIKALI YATANGAZA KIMA CHA CHINI MISHAHARA


Serikali imetangaza viwango vipya vya chini vya mishahara kisekta ambavyo vinatofautiana kati ya sekta moja na nyingine ambavyo ni kuanzia Sh40,000 hadi Sh400,000 kwa mwezi kuanzia Julai Mosi mwaka huu.

WAFANYAKAZI WA MAJUMBANI

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Wizara ya Kazi na Ajira, Ridhiwani Wema, watakaolipwa kima kidogo zaidi cha Sh40,000 ni wafanyakazi wa nyumbani ambao wameajiriwa na watu wa kawaida huku wakiishi kwenye nyumba za waajiri wao.

Katika viwango hivyo, mishahara kwa wafanyakazi wa nyumbani walioajiriwa na watu wa kawaida lakini ambao hawaishi kwenye nyumba za waajiri wao itakuwa Sh80, 000.
“Viwango vya chini vya mishahara kwa wafanyakazi wa nyumbani walioajiriwa na mabalozi wa kigeni na wafanyabiashara maarufu wanatakiwa kulipwa Sh150,000 kwa mwezi,” ilisema taarifa hiyo.

Wafanyakazi wa nyumbani walioajiriwa na maofisa wa Serikali watalipwa Sh130, 000 kwa mwezi.

MAWASILIANO
Kwa upande mwingine, katika viwango hivyo, kima kikubwa katika viwango hivyo cha Sh400,000 kitalipwa kwa wafanyakazi wa sekta za mawasiliano zikiwamo kampuni za simu, kampuni za kimataifa za nishati, madini na taasisi za fedha.

KILIMO NA AFYA

Kima cha chini cha mshahara katika huduma za kilimo ni Sh100,000 na huduma za afya Sh132,000.

VYOMBO VYA HABARI

Kwa upande wa wafanyakazi wa vyombo vya habari, posta na usafirishaji wa vifurushi ‘courier services’, kima cha chini kitaanzia Sh150,000.

WAHUDUMU WA BAA, GESTI NA MIGAHAWA

Viwango vya chini vya mishahara kwa wafanyakazi wa hoteli za kitalii kuanzia Julai Mosi, mwaka huu ni Sh250,000, wakati kwa hoteli za kati ni Sh150,000 na migahawa, nyumba za wageni na baa ni Sh130,000.

SEKTA YA ULINZI

Kampuni za ulinzi za kimataifa zitapaswa kulipa kiwango cha chini cha mishahara cha Sh150,000 kwa wafanyakazi wake sawa na kampuni ndogo za huduma za nishati.  Kampuni ndogo za ulinzi zitatakiwa kulipa Sh100,000.

SEKTA YA USAFIRI WA ANGA

Kima cha chini kwa wafanyakazi wa sekta ya usafiri wa anga kitakuwa Sh300,000, sawa na wale wa utoaji na uingizaji wa mizigo. Wafanyakazi wanaofanya katika sekta ya usafirishaji wa majini, uvuvi na nchikavu wakitakiwa kulipwa Sh200,000.

MAKANDARASI

Kima cha chini kwa kampuni za makandarasi daraja la kwanza kitakuwa Sh325,000, makandarasi daraja la pili hadi la nne Sh280,000 na makandarasi daraja la tano hadi saba Sh250,000.



KAMPUNI ZA MAGARI

Wafanyakazi katika kampuni za uuzaji wa magari watatakiwa kulipwa Sh300,000 na madalali wa bima watalipwa Sh200,000. Kampuni za wachimbaji wadogo wa madini zitalazimika kulipa mshahara usiopungua Sh200,000 kwa wafanyakazi wake.

ELIMU

Mishahara ya chini kwa wafanyakazi wa shule za awali, msingi na sekondari za binafsi ni Sh140,000 huku wafanyakazi wa viwandani wakipaswa kulipwa Sh100,000.


Taarifa hiyo ya Wizara ya Kazi imesema sekta ambazo hazijaorodheshwa, wafanyakazi wake watatakiwa kulipwa kuanzia Sh100,000.
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment