· Madarasa kidato cha V yakosa wanafunzi
· Nafasi 10,000 zakosa wanafunzi, kisa kufeli
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeweka historia baada ya kushindwa kujaza jumla ya nafasi 10,074 kati ya 43,757 za kidato cha tano zilizopo mwaka huu, kutokana na kufeli kwa wanafunzi wengi kufikia ubora wa ufaulu uliohitajika katika mitihani ya kidato cha nne iliyofanyika mwaka jana.
Hayo yalisemwa mbele ya waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Philipo Mulugo, alipokuwa akitoa taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi wa kuingia kidato cha tano, katika shule za sekondari za serikali na vyuo vya ufundi. Mulugo alisema jumla ya watahiniwa 431,650
walifanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012, wakiwamo watahiniwa 370,837 wa shule na watahiniwa 60,813 wa kujitegemea.
“Waliofaulu wote kati ya daraja la kwanza na la nne walikuwa 185,940 wakiwamo watahiniwa wa shule 159,747 na wa kujitegemea 26,193, sawa na asilimia 43.08. Kati ya hao, wanafunzi waliopata ufaulu wenye ubora, yaani daraja la kwanza na la tatu walikuwa 35,357,” alisema.
Alisema kati ya 34,599, wanafunzi 34,482 ndiyo waliokuwa na sifa za kuchaguliwa kuingia kidato cha tano na vyuo vya ufundi kwa mujibu wa vigezo vilivyopo.
SAYANSI ‘YAPETA’
Mulugo alisema kuwa kati ya nafasi 43,757 za kidato cha tano, masomo ya sayansi yalikuwa na nafasi 18,564 na sayansi za jamii nafasi 25,193. Kwa ujumla ni ongezeko la nafasi 3,757 ikilinganishwa na nafasi 41,000 zilizokuwapo mwaka 2012.
Alisema nafasi zote za masomo ya sayansi zimepangiwa wanafunzi, huku baadhi ya tahasusi (combination) zikipangiwa wanafunzi wengi, kutokana na wanafunzi wa masomo hayo kufaulu zaidi, tofauti na masomo ya tahasusi za sayansi ya jamii, ambapo nafasi nyingi zimebaki.
“Kwa mfano katika tahasusi ya PCB kulikuwa na nafasi 6,188, lakini wanafunzi waliopangwa ni 6,400 tofauti na tahasusi kama ya HKL ambapo nafasi 5,300 zilikuwapo, lakini zilizopangiwa wanafunzi ni 1,527 tu,” alisema.
WANAFUNZI WA KIKE WAFELI
Kati ya wanafunzi 33,683 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika shule za serikali, wavulana ni 23,383 wakati wasichana ni 10,300.
Wavulana 13,708 wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi sawa na asilimia 58.62 na 9,675 sawa na asilimia 41.38 wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi ya jamii.
Aidha, wasichana 5,038 kati ya 10,300 sawa na asilimia 48.91 wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi na wasichana 5,262 sawa na asilimia 51.09 wamepangwa kusoma masomo ya sayansi za jamii.
VYUO VYA UFUNDI NA TAASISI
Mulugo alisema wanafunzi 530, wakiwamo wavulana 416 na wasichana 114 wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya Ufundi na Taasisi ya Menejimenti ya Maendeleo ya Maji.
Alisema idadi ya wanafunzi wote waliojiunga na vyuo vya ufundi imepungua kutoka 564 mwaka 2012 hadi 530 mwaka huu.
Aidha alisema idadi ya wanafunzi wa kike waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya ufundi imeongezeka kutoka wanafunzi 47 mwaka 2012 hadi wanafunzi 114 kwa mwaka huu.
IDADI YA SHULE WALIKOPANGIWA
Mulugo alisema wanafunzi wamepangwa kujiunga kidato cha tano kwenye jumla ya shule 207, zikiwamo shule mbili zilizopangiwa wanafunzi wa kidato cha tano kwa mara ya kwanza, za Tandahimba mkoani Mtwara na Miono iliyoko Pwani.
Alisema kutokana na uchache wa wanafunzi wenye sifa za kujiunga na kidato cha tano na hasa katika masomo ya sayansi ya jamii, serikali haikuweza kuongeza zaidi shule mpya za kidato cha tano kwa mwaka huu.
SIKU ZA KURIPOTI
Mulugo alisema muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa kidato cha tano kuanzia mwaka huu, itaanza mwezi Julai na hivyo akaagiza wanafunzi wote kuripoti katika shule walizopangwa Julai 29, tayari kwa kuanza masomo.
Alisema orodha ya waliochaguliwa zinapatikana katika tovuti za wizara ya elimu (www.moe.go.tz), Tamisemi (www.tamisemi.go.tz) na ile ya Baraza la Mitihani Tanzania (www.necta. go.tz).
UHABA WA WANAFUNZI
Takwimu za wanafunzi wenye sifa na waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano kwa mwaka huu kama zilivyotangazwa na Waziri Mulugo zinaonyesha athari mbili.
Kwamba idadi ndogo ya wanafunzi wenye sifa kulinganisha na nafasi zilizopo, itafanya baadhi ya shule kukosa au zisiwe na wanafunzi wa kutosha.
Hii ni kwa sababu idadi hiyo ya wanafunzi wenye sifa inayotegemewa na serikali, ndiyo pia inategemewa na shule za binafsi zenye kidato cha tano na cha sita.
Aidha, upungufu huo uliojitokeza sasa unatarajiwa tena kuonekana kwenye udahili wa wanafunzi wa kuingia vyuo vikuu na vyuo vingine vya elimu ya juu, pale wanafunzi hao watakapomaliza masomo yao ya kidato cha sita.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment