MABOMU YARINDIMA DAR


JESHI la Polisi jijini Dar es Salaam, jana lililazimika kutumia mabomu ya machozi maeneo ya Manzese, kuwatawanya wafanyabiashara wadogowadogo (Machinga) waliogoma kupisha ujenzi unaoendelea wa mabasi yaendayo kasi (DART).
Polisi walishuhudiwa wakiwa katika magari yao wakiwatawanya wafanyabiashara hao waliokuwa wamegoma kutoka kutokana na kudai kuwa eneo hilo ni muhimu kwao kwa ajili ya kuendeshea biashara.

Polisi wakiwa na silaha mbalimbali, ikiwemo za moto, walifanikiwa kuwatawanya wafanyabiashara hao kwa kutumia mabomu ya machozi.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa operasheni hiyo ilianza tangu wiki iliyopita, kutokana na ujio wa Rais wa Marekani, Barack Obama, pamoja na familia yake.

“Tangu wiki iliyopita, zoezi hili lilikuwepo kutokana na ugeni wa Obama, lakini jana lilikuwa ni kuendeleza, kwani ujenzi hauwezi kuendelea kwa staili hii ya hawa wafanyabiashara, kwani wanaharibu,” alisema askari mmoja.

Shuhuda mwingine alisema kwamba operesheni ya kuwaondoa wafanyabiashara hao ilianza jana asubuhi na ilikwenda vizuri, baadaye baadhi ya askari walipungua na kubaki wachache, hapo ndipo wafanyabiashara walipopata mwanya wa kurudi barabarani na kufunga barabara kwa kuweka mawe ili magari yasipite.

“Kosa lilikuwa ni kupunguza askari, hapo ndipo wafanyabiashara tulijikusanya na kuweka mawe ili askari wasipite kuja kutuzuia wala magari yasipite,” alisema.

Mwingine aliyejitambulisha kwa jina Juma Mohamed, alisema wanashangaa askari kuendelea na operasheni hiyo kwa kuwa kama ni ujio wa Obama ulishapita, hivyo waruhusiwe kurudi katika maeneo hayo.

Magari ya Makamanda wa Polisi (OCD) wa vituo mbalimbali, ikiwemo Kimara na Kinondoni, yalishuhudiwa yakiwa na Makamanda wao, yakija kuongeza nguvu, huku gari jingine la polisi likiwasomba waliokamatwa katika oparesheni hiyo.

Aidha, maeneo ya kuanzia Darajani mpaka soko la Manzese kulikuwa  kumewekwa mawe barabarani, huku barabara inayojengwa ikiwa imevunjwa katika baadhi ya maeneo kutokana na vurugu hizo.

Maeneo hayo yote palikuwa kimya, tofauti na siku zote ambapo kunakuwa na biashara mbalimbali zikiendelea, huku polisi wakiwaaamuru watu wanaopita kutembea kwa mwendo wa haraka pamoja na kutosogelea eneo la tukio.

Pia maduka yote katika maeneo hayo yalikuwa yamefungwa na baada ya muda wa mapambano hali ilianza kutulia kuanzia saa 9:00 alasiri.

Operasheni hiyo inaelezwa kulenga kuwaondoa wafanyabiashara wadogowadogo ili kuweza kupisha ukamilishaji wa ujenzi wa Barabara ya Morogoro, inayojengwa kwa ajili ya mabasi yaendayo kasi (DART).


Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment