KIONGOZI WA UPINZANI AUAWA NCHINI TUNISIA

Mohamed al-Brahmi, leader of the Tunisia
Mohammed al-Brahmi, kiongozi wa chama cha Vuguvugu la Umma nchini Tunisia 



Watu wasiojulikana wamempiga risasi na kumuua kiongozi mashuhuri wa upinzani na mbunge wa Tunisia, Mohammed al-Brahmi, mbele ya nyumba yake mjini Tunis.


Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani, Mohammed Ali Aroui alisema kuwa Brahmi, ambaye alikuwa kiongozi wa chama cha Vuguvugu la Umma, alipigwa risasi nje ya nyumba yake Alhamisi asubuhi kwa majira ya nchi hiyo.


Aroud aliongeza kuwa Brahmi aliyekuwa na umri wa miaka 58, alipigwa risasi kadhaa akiwa kwenye gari yake.


Maelfu ya wafuasi wake waliokuwa na hasira walimiminika barabarani mjini Tunis na miji mingine katika maandamano ya kupinga mauaji ya kiongozi wao huyo. Waandamanaji walikusanyika mbele ya Wizara ya mambo ya ndani, wakitaka bunge lifungwe.


Aidha, mbali na kuwa kiongzi wa chama, alikuwa mbunge katika bunge la taifa na alikuwa katika tume ya uundwaji wa katiba mpya.


Haya ni mauaji ya pili dhidi ya viongozi wa upinzani baada ya mwanasiasa wa mrengo wa kushoto Chokri Belaid kuuawa mwezi Februari na hivyo kutishia kuitumbukiza nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kwenye mgogoro wa kisiasa.


Serikali ililaani mauaji ya Belaid na kuwatupia lawama watu iliowaelezea kuwa wenye msimamo mkali kwamba wamehusika na kadhia hiyo. 

Tunisia, ambayo ni chimbuko la maandamano ya kidemkrasia yaliyolitikisa eneo la Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati, inapambana kuleta mabadiliko ya kidemokrasia baada ya kuuondosha utawala wa kidikteta mwaka 2011.

Chama tawala chenye mrengo wa wastani cha Ennahda, kilichaguliwa baada ya kuangushwa kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Zainul Abideen Ben Ali, mwezi Januari 2011. 

Tunisia imeshuhudia ghasia, vurugu na makabiliano kadhaa wa kadhaa baina ya watawala na makundi yenye misimamo mikali kwa miezi kadhaa iliyopita. 
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment