![]() |
Wananchi wa Mali wakitazama mabango ya wagombe wa kiti cha urais katika uchaguzi ujao wa nchi hiyo. |
Mwishoni mwa mwezi huu, wananchi wa Mali watamiminika katika vituo vya kupiga kura katika uchaguzi wa urais miezi kadhaa baada ya nchi hiyo kuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mali inashinikizwa na nchi za nje kufanya uchaguzi Julai 28, lakini wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa na kidiplomasia wanaamini kuwa kutokana na maandalizi duni, huwenda suala hilo likazidi kuitumbukiza kwenye hali ya ukosefu wa amani na uthabiti.
Idadi kadhaa ya maafisi wa tume ya uchaguzi wameshatekwa nyara siku kadhaa kabla ya uchaguzi, hali inayoonesha kukosekana kwa usalama kabla ya zoezi hilo.
Mwaka jana jeshi lilifanya mapinduzi na kutumbukiza nchi hiyo katika mgogoro, hali iliyopelekea Ufaransa kuingilia kati kijeshi kwa kisingizio cha kuwadhibiti waasi waliokuwa wakiyashikilia maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Vita hivyo vimesababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu, hali iliyowafanya maelfu ya watu kukosa makazi, chakula, huduma za afya na za kibinaadamu na kuishi katika hali ya kukatisha tamaa.
Mwezi Aprili, waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian alisisitiza kuwa maelfu ya wanajeshi wake walioko Mali wataendelea kubaki huko licha ya kuwasili kwa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa.
0 comments:
Post a Comment