![]() |
| Vifaru vya jeshi la Misri vikiweka kizuizi kwenye barabara ya Salah Salem katika mji wa Nasr, ambapo wafuasi wa Rais Mohamed Morsi wamekusanyika katika maandamano ya kumuunga mkono tokea Julai 3, 2013. |
Rais wa Misri Mohamed Morsi anashikiliwa na jeshi la nchi hiyo baada ya kuondoa madarakani, amesema afisa mmoja mwanadamizi wa jeshi.
“(Morsi) anashikiliwa kwa ajili ya maandalizi ya mwisho," alisema afisa huyo ambaye ripoti hazijataja jina lake.
Morsi huwenda akakabiliwa na mashitaka rasmi kufuatia tuhuma zilizotolewa na wapinzani wake.
Afisa mwandamizi wa chama cha Udugu wa Kiislamu (Muslim Brotherhood), Gehad El-Haddad amesema leo alhamisi kuwa, “Morsi ametenganishwa na wasaidizi wake na amepelekwa katika makao ya Wizara ya Ulinzi."
Mapema Jumatano, Jenerali Abdel Fattah al-Sisi, mkuu wa jeshi la Misri, katika hotuba yake kwenye televisheni ya taifa, alitangaza kuwa Morsi ameondolewa madarakani.
Baada ya hapo Polisi walianza kuwatia nguvuni wasaidizi wa Rais na viongozi wa chama cha udugu wa Kiislamu au Muslim Brotherhood.
Aidha, Sisi alisitisha katiba ya nchi hiyo na kusema kuwa uchaguzi mpya wa bunge utafanyika.
Mkuu huyo wa majeshi alimtangaza Mkuu wa Mahakama ya Katiba Adli Mansour kuwa rais wa mpito.
Morsi alikuwa ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kuwa hatua hiyo ya jeshi ni "mapinduzi ya kijeshi," na kuwataka wananchi wa Misri "kuitetea katiba na sheria na kutoyatambua mapinduzi haya."
KAMATA KAMATA YA VIONGOZI WA CHAMA CHA MURSI
Vikosi vya usalama vimewashikilia viongozi wawili waandamizi wa Muslim Brotherhood walio karibu na Morsi. Rashad Bayoumi, naibu kiongozi wa chama, na Saad al-Katatni, kiongozi wa tawi la kisiasa la chama, walikamatwa saa kadhaa tu baada ya Mursi kung'olewa mdarakani.
Vyombo vya habari vya serikali viliripoti pia kuwa kibali kimetolewa cha kukamatwa maafisa 300 wa chama cha Muslim Brotherhood.
Vikosi vya jeshi la Misri vimesambazwa nchini kote kufuatia makabiliano baina ya wafuasi na wapinzani wa Mursi.
Kwa mujibu wa maafisi usalama wa Misri, kwa uchache watu saba wamepoteza maisha katika makabiliano ya vikosi vya usalama na wafuasi wa Mursi katika mji wa Alexandria na katika mji wa mashariki wa Marsa Matrouh.
Kufuatia kuondolewa kwa Mursi, kiongozi maarufu wa upinzani Amr Moussa alisema kuwa mazungumzo kuhusu serikali mpya ya Misri yameanza.
“Mashauriano yataanza kuanzia sasa, kwa ajili ya serikali na maridhiano," alisema mkuu huyo wa zamani wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu. "Huu ni mwisho wa utawala wa Mursi. umefikia tamati."
KAULI YA MAREKANI
Katika kuelezea matukio yanayoendelea nchini Misri, Rais wa Marekani Barack Obama alielezea wasiwasi mkubwa juu ya hatua ya jeshi kumuondosha Mursi na kuwataka warejeshe haraka serikali ya kiraia.
“Ninatoa wito kwa jeshi la Misri kufanya haraka na kwa ustaarabu kurejesha mamlaka kamili kwa serikali ya kiraia itakayochaguliwa kidemokrasia mapema iwezekanavyo," ilisema taarifa ya Obama.
Aidha, taarifa hiyo ilisema kuwa Obama ameagiza kutazamwa upya athari za msaada wa dola bilioni 1.3 zinazotolewa na nchi hiyo kwa jeshi la Misri kila mwaka na mamilioni mengine ya msaada wa kiuchumi yaliyotolewa kabla ya kuondolewa kwa Mursi.
KAULI YA UMOJA WA MATAIFA
KAULI YA JUMUIYA YA UMOJA WA ULAYA
Mkuu wa sera za mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, naye alitoa wito wa 'kurudi haraka kwenye demokrasia' nchini Misri.
“Ninafuatilia kwa karibu sana matukio yanayoendelea nchini Misri na ninatambua vema mgawanyiko mkubwa katika jamii, matakwa ya wengi kutaka mabadiliko ya kisiasa na juhudi zinazofanywa katika kuleta muafaka na maridhiano," alisema Ashton katika taarifa yake.
“Ninazitaka pande zote wafanye haraka kurudi kwenye mchakato wa kidemokrasia, ikiwemo kufanya uchaguzi huru na wa haki wa urais na ubunge pamoja na kuidhinisha katiba," alisema.
KAULI YA SAUDI ARABIA
Mfalme wa Saudi Arabia, Abdullah, alimpongeza mkuu wa mahakama ya katiba, Adli Mansour, akisema kuwa uteuzi wake umekuja katika kipindi "muhimu" katika historia ya Misri.
“Kwa niaba ya wananchi wa Saudi Arabia, ninakupongeza kwa kuchukua uongozi wa Misri katika kipindi hiki muhimu katika historia yake," alisema Mfalme Abdullah katika ujumbe alioutuma haraka kumpongeza Mansour.

0 comments:
Post a Comment